Timu hiyo ya Chamazi haikucheza mechi zote mbili zilizopita za duru la pili la ligi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons na Stand United baada ya kuwa imealikwa Zambia kushiriki michuano maalum ya timu nne ambayo wamerejea na taji.
Katika kuhakikisha kinafanya vizuri na kuzipiku Simba na Yanga katika mbio zilizokolea za ubingwa wa VPL msimu huu, kikosi cha mabingwa hao wapya wa Kombe la Kagame kilichowasili jijini Dar es Salaam jana saa 10.45 alfajiri, kiliingia kambini moja kwa moja kujiandaa kwa mechi yake ya keshokutwa dhidi ya Mwadui FC.
Stewart Hall anatambua kwamba timu hiyo inayonolewa na mzawa Jamhuri Kihwelo 'Julio' inafukuza mwizi kimyakimya katika mbio za ubingwa na inahitaji ushindi dhidi ya Azam FC Jumatatu ili kufuta mwenendo mbovu baada ya Jumatano kulala 1-0 dhidi ya African Sports jijini Tanga.
Muingereza huyo pia anakumbuka namna timu yake iliponusurika kuacha pointi kwenye Uwanja wa Mwadui walipopata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya timu hiyo huku beki wa kati anayesumbuliwa na majeraha ya goti ya mguu wa kulia, Aggrey Morris akilimwa kadi nyekundu baada ya kusababisha penalti ambayo hata hivyo, kipa Aishi Manula aliipangua.
"Kutokana na umuhimu wa mchezo ujao wa VPL dhidi ya Mwadui ya Shinyanga utakaofanyika Jumatatu ijayo, kikosi cha Azam FC kimefikia moja kwa moja kambini ndani ya viunga vya Azam Complex.
"Kwa mujibu wa programu ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Stewart Hall, kikosi cha Azam FC leo (jana) kitapumzika kabla ya kesho saa 2.30 asubuhi kuanza mazoezi ya kujiandaa kwa mchezo huo," ilieleza taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao rasmi wa klabu hiyo jana.
Azam imetwaa ubingwa nchini Zambia ikicheza dhidi ya timu ngumu za Zesco United ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Zambia waliomaliza katika nafasi ya tatu kwa pointi nne, Zanaco FC walioshika ya pili kwa pointi tano, huku mabingwa wa Zimbabwe, Chicken Inn wakikamata mkia kwa pointi moja.
Matajiri hao wa Tanzania walianza kukinukisha kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa jijini Ndola kwa kuishika Zesco kwa sare ya bao 1-1 kabla ya kuinyuka Chicken Inn mabao 3-1 na kumaliza michuano hiyo kwa kutoa suluhu dhidi ya Zanaco.
Kwa sasa mabingwa hao wa VPL msimu wa 2013/14 wako nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 39 sawa na Simba kwenye nafasi ya pili, pointi moja nyuma nyuma ya vinara Yanga. Hata hivyo, Azam FC ina mechi mbili za viporo.
Azam yapania kuzipoteza Simba, Yanga
06Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Azam yapania kuzipoteza Simba, Yanga
- *** Timu hiyo ya Chamazi italianza duru la pili la ligi ya Bara msimu huu keshokutwa ikiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza mechi hata moja katika duru la kwanza.
KUYUMBA kwa Yanga kuna faida kubwa kwa Azam FC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu.










