Majaribio ya Misri yamponza Maguli

06Feb 2016
Nipashe
Majaribio ya Misri yamponza Maguli

ELIAS Maguli wa Stand United ameingia kwenye mgogoro na kocha wa timu hiyo, Patrick Liewing, kutokana na straika kwenda Misri kufanya majaribio katika klabu ya Zamalek pasi na idhini ya kocha huyo.

Maguli, mchezaji wa zamani wa Ruvu Shooting na Simba, alitua Misri mwezi uliopita kwa idhini ya uongozi wa Stand, lakini Liewing hakuwa na taarifa za kuondoka kwa nyota huyo aliyetisha kwa mabao duru la kwanza la ligi ya Bara msimu huu.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Vicent Aman alisema jana kuwa uongozi ulikuwa na taarifa ya safari ya Maguli, lakini kocha amekasirishwa na kitendo hicho kwa "hakupewa taarifa rasmi ya safari hiyo".
"Sina uhakika kama hiyo ndio sababu ya kocha kutompa nafasi Maguli kwenye michezo mingi iliyopita, lakini alituambia hajafurahishwa na kitendo cha maguli kwenda Misri," alisema.
Alisema kuwa hata kitendo cha wachezaji, Haruna Chanongo na Abuu Ubwa kwenda kufanya majaribio kwenye klabu ya TP Mazembe nacho hakikupokewa vyema na Mfaransa huyo.
Maguli hajacheza mechi hata moja ya Ligi Kuu tangu Desemba 19 walipofungwa 4-0 dhidi ya Yanga jijini Dar es Salaam. Straika huyo aliingia kipindi cha pili katika mechi yao ya Kombe la FA waliyopoteza 1-0 dhidi ya Mwadui FC mjini Shinyanga Januari 24.