Mayanja awapa rungu Kiiza, Ajibu usukumani

06Feb 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Mayanja awapa rungu Kiiza, Ajibu usukumani

HAMIS Kiiza amefunga katika mechi zote tano zilizopita chini ya Jackson Mayanja na kocha mkuu wa huyo wa Simba amempa rungu Mganda mwenzake huyo kuwaua Kagera Sugar usukumani mjini Shinyanga kesho.

Mayanja, kocha mkuu wa muda Msimbazi, aliiambia Nipashe jana kuwa ameridhishwa na ushirikiano kati ya Kiiza na straika Mtanzania Ibrahim Ajibu na anatarajia kuwaona wakali hao wakiitungua Kagera kwenye uwanja wake mya wa nyumbani wa Kambarage.
Wawili hao kwa pamoja wamefunga magoli 21 katika ligi ya Bara ikiwa ni zaidi ya nusu ya magoli yote (32) ya Simba, Kiiza akifunga 14 sawa na Amissi Tambwe wa Yanga lakini Mganda huyo ametupia mara saba katika mechi tano zilizopita (moja ya Kombe la FA).
"Kikubwa nafurahi sina majeruhi wengi zaidi ya (Rapahel) Kiongera, Ajibu na Kiiza walicheza vizuri katika mechi zilizopita na nategemea wataendeleza kasi yao," alisema Mayanja.
Kagera Sugar ambayo ilishinda katika mechi zote mbili zilizopita tangu iuhame mji wa Tabora, itaingia uwanjani kesho ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 3-1 katika mechi ya duru la kwanza ambayo Kiiza alipiga 'hat-trick'.