Yanga yatangaza vita

06Feb 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Yanga yatangaza vita
  • *** Timu hiyo iliyoambulia pointi moja katika mechi mbili zilizopita za ligi ya Bara, itakwea pipa kwenda Mauritius Jumatano.

WAKATI kukiwa na mambo mengi yanayosemwa kuhusu kuboronga kwa Yanga katika mechi mbili zilizopita za ligi ya Bara, kocha wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, amesema ulikuwa 'upepo tu' na watalithibitisha hilo katika mechi yao ya kesho dhidi ya JKT Ruvu.

Baada ya kufungwa 2-0 dhidi ya Coastal Union jijini Tanga kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya Tanzania Prisons mjini Mbeya, Yanga kesho itashuka kwenye Uwanja wa Taifa kuikabili timu 'kibonde' ya JKT Ruvu iliyoambulia pointi moja katika mechi tano zilizopita.

Na Yanga ambao walifunga mechi zote 15 za duru la pili bila kupoteza mechi hata moja (sawa na Azam FC), wamepanga kuifumua timu hiyo ya kocha mzawa Abdallah 'King' Kibadeni kabla ya kukwea pipa Jumatano kwenda Mauritius kuanza kampeni yao ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Cercle de Joachim.

Pluijm aliiambia Nipashe jijini Dar es Salaam kuwa katika ligi changamoto za vipigo na sare hazikwepeki na zimewakumbusha nyota wake kwamba "hakuna timu ndogo wala wachezaji walio bora kuliko wengine kwenye ligi moja".
Mdachi pia alisema pia mabadiliko ya safu ya ulinzi yalichangia kuwarahisishia kazi wapinzani wao kufunga magoli manne katika mechi mbili zilizopita, ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo ya Jangwani kuruhusu idadi hiyo kubwa ya mabao katika mechi mbili mfululizo tangu kuanza kwa msimu huu Septemba 12.
"Kwenye mpira huwezi kwenda vizuri bila kukutana na mabonde, kufungwa au kutoka sare ndio vikwazo kwenye mchezo huu, nimeshakaa nao (wachezaji) na kurekebisha pale tulipokosea, tunarejea tena kwenye ubora wetu, Yanga ni Yanga na itapambana kutetea ubingwa wake," alisema Pluijm.
Kocha huyo alisema mechi 13 zilizobaki ni ngumu kutokana kila timu kutaka ushindi ili kusaka ubingwa au kukwsepa janga la kuporomoka daraja.
Kuhusu maandalizi ya mechi yao ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huu, Pluijm alisema: "Niliwaambia viongozi tunatakiwa kwenda mapema ili kuzoea hali ya hewa na wachezaji kupata muda wa kupumzika, safari inaweza kuwa ni ya saa moja au mbili, lakini maandalizi yake huchukua zaidi ya saa sita, ukiondoka mapema inawapa nafasi wachezaji kupumzika na kufikiria mchezo unaowakabili."
Mechi ya Cercle de Joachim dhidi ya Yanga itachezwa Jumamosi Februari 13 kwenye Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe kuanzia saa 9:30 alasiri kwa saa za Mauritius .
Kutokana na Yanga kuanzia ugenini, mchezo wao wa ligi ya Bara dhidi ya Mtibwa Sugar uliopangwa kufanyika Jumamosi umepigwa kalenda.