Mgambo wakubali kasi ya Ajibu, Majabvi

05Feb 2016
Nipashe
Mgambo wakubali kasi ya Ajibu, Majabvi

KOCHA wa Mgambo Shooting, Bakari Shime hatawasahau mshambuliaji wa Simba Ibrahim Ajibu na kiungo mkabaji, Justice Majabvi, kwani ndiyo walikuwa kiini cha timu yake kuchapwa mabao 5-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara katikati ya wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Shime alisema mipango ya wachezaji wake kwenda kuzifumania nyavu ilikuwa ikivurugwa mara kwa mara na Majabvi aliyekuwa akiwalinda vizuri mabeki na kutibua mashambulizi yao.
"Na Ajibu aliivuruga kabisa safu yangu ya ulinzi, yeye ndio alikuwa chachu ya Simba kupata magoli yote yale," alisema Shime.
Alisema kiwango kizuri cha Ajibu kwenye mchezo huo ndicho kilichomfanya kumpa mkono wa pongezi wakati mshambuliaji huyo alipoifanyikwa mabadiliko.
"Mimi ni Mtanzania na Ajibu pia ni Mtanzania, nilimpa mkono kwa sababu ya uwezo alioonyesha kwenye mechi yetu," alisema.
Katika mchezo huo, Ajibu mbali na kutengeneza magoli mawili yaliyofungwa na Hamis Kiiza na Mwinyi Kazimoto, pia alifunga goli moja la kiufundi na kuifanya timu hiyo kupishana na watani zao Yanga kwa pointi moja baada ya kufikisha pointi 39, huku Yanga ikiongoza kuwa kuwa na pointi 40 baada ya kubanwa kwa sare ya 2-2 dhidi ya Prisons.