Taarifa iliyotolewa na TMA imeeleza kuwa kuna uwezekano wa kuwapo kwa upepo mkali unaozidi kasi ya kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita 2.0 wakati wowote kuanzia jana.
Maeneo yaliyotajwa akuwa huenda yakakumbwa kubwa na hatari hiyo ni mwambao wa mikoa ya Tanga, Pwani (ikijumuisha Mafia), Dar es Salaam, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Kutokana na uwezekano huo, wakazi wa maeneo husika hawanabudi kuchukua tahadhari kukabiliana na hali hiyo kwa kuzingatia kuwa upepo mbali na mawimbi makubwa kwa asilimia kubwa vitaambatana na mvua kubwa.
Katika miezi ya karibuni, TMA imekuwa ikitoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua, upepo na mawimbi yasiyo ya kawaida na kuwataka wananchi wa maeneo husika hasa wa mabondeni kuchukua tahadhari ikiwamo kuhama maeneo hatarishi.
Januari mwaka huu, TMA ilitoa taadhari ya uwapo wa mvua nyingi ya kiwango cha Tsunami na kuwataka wananchi wa mabondeno kuyahama makazi yao.
Ilieleza kuwa mvua hizo zitaendelea hadi Machi mwaka huu, na kwamba kukiwa na uwezekano mkubwa wa kutoke Tsunami.
Baadhi ya maeneo nchini yameathirika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha yakiwamo mafuriko na kuharibika kwa mazao na miundombinu hususani ya barabara na madaraja.
Tahadhari hiyo kuhusu upepo mkali na mawimbi makubwa isipuuzwe bali ichukuliwe kwa umakini mkubwa na hatua kubwa ya kuchukua ni kwa wakazi wa mikoa hiyo kuhakikisha wanahama maeneo hatarishi hususani ya mabondeni ambayo ni rahisi kuathirika kutokana na mafuriko.
Hatua nyingine inayopaswa kuchukuliwa na wakazi wa mikoa iliyotajwa kukumbwa na hatari hiyo ni kuhakikisha wanaimarisha nyumba zao zisiezuliwe na upepo.
Tunaishauri Manlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kuhakikisha inachukua tahadhari kwa kusitisha safari za vyombo vya majini pale zitakapoonekana dalili za kuwapo upepo mkali na mawimbi makubwa.
Nao wananchi wanaofanya shughuli zao ndani ya baharini na karibu na bahari zikiwamo za uvuvi wanapaswa kuwa waangalifu, vinginevyo wanaweza kuathirika.
Kwa kuwa tahadhari hiyo imetolewa kipindi ambacho msimu wa mvua za masika unakaribia kuanza, serikali kwa upande wake iimarisha miundombinu ya barabara na madaraja kwa kuwa bila kuwa imara ni rahisi kukatika pale zinaponyesha mvua kubwa.
Katika miaka ya nyuma wakazi wa maeneo hatarishi hususani wa mabondeni walikuwa wanakaidi maagizo ya kuhama na kujikuta wakiathirika kwa mafuriko wakati wa mvua. Kwa mfano, mwaka 2012 watu zaidi ya 40 walifariki dunia kutokana na mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam na wengine kukosa makazi.
Hata hivyo, serikali ya awamu ya tano imeonyesha umakini mkubwa kwa kutekeleza operesheni ya kuzibomoa nyumba zote zilizojengwa maeneo yasiyofaa, zikiwamo za mabondeni nchi nzima.
Ni matumaini yetu kwamba kila mmoja amesikia tahadhari iliyotolewa na TMA na bila shaka wakazi wa maeneo yaliyotajwa watachukua hatua stahiki kuhakikisha kwamba hawaathiriki.










