Mwongozo huo uliowasilishwa juzi bungeni na kuainisha maeneo mbalimbali, ambayo matumizi yatadhibitiwa. Pia unaonesha mwaka ujao wa fedha, serikali imepanga kutumia Sh. trilioni 22.9 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
Serikali ya awamu ya tano inaandaa bajeti ya kwanza baada ya kuingia madarakani.
Katika kudhihirisha imedhamiria kuliletea taifa maendeleo, tayari imefanya mabadiliko kwenye uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na pia kudhibiti ukusanyaji wa mapato.
Jambo hili ni la kupongezwa kutokana na ukweli kwa miaka mingi viongozi walijenga dhana kuwa Tanzania ni nchi masikini na ilikuwa haina uwezo wa kujitegemea.
Kwa mujibu wa mwongozo huo uliosomwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango, ni kuwa asilimia 9.3 tu ya bajeti hiyo itatokana na misaada ya washirika wa maendeleo na mikopo.
Matokeo yake wananchi wamekuwa wakiishi kwa mateso makubwa kwa kuaminishwa kuwa nchi kama Tanzania ni masikini na ilipaswa kutegemea misaada ya nchi za nje.
Na hiyo ndio ikawa staili ya viongozi wengi kuhalalisha safari za kwenda katika nchi za kigeni ili kusaka misaada `eti’ kwa kuwa nchi yetu ni masikini.
TRA imepata mafanikio haya baada ya serikali kubana eneo moja tu la bandari katika kuhakikisha watu wanalipa kodi kihalali.
Tunaupongeza uongozi wa TRA na serikali katika kuhakikisha kiwango kikubwa cha mapato kinakusanywa.
Serikali imepanga kubana matumizi na imetoa maelekezo kwa maofisa masuhuli kuhakikisha mikutano yote ikiwa ni pamoja na ile ya bodi, mafunzo na semina inatumia kumbi za serikali.
Mambo mengine ambayo serikali imejielekeza katika usimamizi na kudhibiti matumizi yake, ni pamoja na kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Waasisi wa taifa hili, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Karume, ndoto yao kubwa ilikuwa kuifanya nchi yetu kujitegemea.
Mwalimu Nyerere aliweka mkazo katika kilimo na ujenzi wa viwanda kwa kuamini vingechochea maendeleo na kuifanya nchi kutotegemea misaada kutoka nje.
Karume naye alitumia zao la karafuu kuiendeleza Zanzibar ndiyo akaanza mradi wa ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watu wake na miundombinu.
Bahati mbaya katika miaka ya karibuni, viongozi wengi waliopewa dhamana ya kuongoza nchi yetu walijielekeza zaidi katika kujineemesha, badala ya kuandaa mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuondokana na aibu ya kuomba omba misaada nchi za nje.
Serikali ya awamu ya tano imepata mafanikio kwa kudhibiti eneo moja tu la Bandari.
Mathalan, serikali ikianza kubana zinazokusanywa na halmashauri mbalimbali nchini ina maana mapato ya serikali yanaweza kupanda maradufu au zaidi. Hapo bado hatujazungumzia kampuni mbalimbali za uwekezaji ambazo zimekuwa zikipewa misamaha ya kodi.
Pia kuna maeneo mengine, ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kama yale ya masuala ya gesi na madini.
Hata hivyo, tunaomba serikali katika mwaka ujao wa fedha ihakikishe inapeleka fedha za maendeleo mapema katika maeneo husika. Moja ya udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa bajeti imekuwa kucheleweshwa kwa fedha za maendeleo katika wizara na taasisi husika.
Hakuna maajabu yoyote kwa nchi kupiga hatua kimaendeleo kwani vitu vinavyohitajika ni watu kujituma, nidhamu na dhamira thabiti.
Bajeti ijayo ijielekeze kuipeleka Tanzania kujitegemea
03Feb 2016
Mhariri
Nipashe
Bajeti ijayo ijielekeze kuipeleka Tanzania kujitegemea
SERIKALI juzi iliwasilisha mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 ambao pamoja na mambo mengine, umejielekeza kubana matumizi.










