Umakini uongezeke mechi za mwisho Ligi Daraja la Kwanza

06Feb 2016
Mhariri
Nipashe
Umakini uongezeke mechi za mwisho Ligi Daraja la Kwanza

RUVU Shooting imekuwa timu ya kwanza ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kukata tiketi ya kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ilijihakikisha kushiriki Ligi Kuu msimu wa 2016/17 baada ya Jumapili kushinda 2-1 ugenini dhidi ya Lipuli FC mkoani Iringa.
Ushindi huo ulikifanya kikosi cha kocha mkuu Mkenya Tom Olaba kufikisha pointi 31 kileleni mwa Kundi B baada ya mechi 12, pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu zingine zote saba za kundi hilo baada ya mechi za raundi mbili zijazo.
Tukiwa wadau namba moja wa michezo nchini, Nipashe tunaipongeza Ruvu Shooting kwa kurejea Ligi Kuu, hasa ikizingatiwa kuwa timu hiyo ilishushwa 'kibabe' na marefa waliochezesha mechi yao ya mwisho ya ligi ya Bara msimu uliopita dhidi ya Stand United mjini Shinyanga Mei 9 mwaka jana.
Ingawa safari yao haikuwa rahisi, wakiianza FDL msimu kwa kufungwa 1-0 dhidi ya Mlale JKT kabla ya kutoka sare na Njombe Mji kisha kushinda mechi zote 10 zilizofuata, tunaamini uwezo, mipango inayofanyiwa kazi na kusimama imara kwa uongozi wao baada ya kuporomoka daraja msimu uliopita, ndiyo umeisadia timu hiyo kurejea tena Ligi Kuu.
Mbali na pongeza hizo kwa Ruvu Shooting, Nipashe tunatoa rai kwa wasimamizi wakuu wa FDL, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kamati yake ya uendeshaji wa ligi kuwa makini kuhakikisha mechi zilizobaki kabla ya kumalizika kwa msimu huu zinachezwa kwa haki.
Mchuano mkali umebakia kwenye makundi mawili ya FDL - Kundi A linaloongozwa na African Lyon na Kundi C ambalo Geita Gold FC wako kileni - huku pia kukiwa na 'vita' nyingine kwa timu zilizo mkiani mwa makundi yote zikipambana kuukwepa mstari wa kuporomoka hadi Ligi Daraja la Pili.
Kutokana na hali hiyo, tunafikiri kuna haja ya kuwa na usimamizi makini wa ligi hiyo hasa katika mechi za mwisho zilizobaki ili kupata timu bora zitakazoleta ushindani Ligi Kuu badala ya kupeleka timu dhaifu ambazo zinapanda na kushuka Ligi Kuu.
Baada ya kila timu kucheza mechi 12, Geita Gold FC na Polisi Tabora (zote zikiwa na pointi 24) pamoja na JKT Oljoro yenye pointi 22 zinachuana vikali kuwania nafasi moja ya kukwea Ligi Kuu kutoka Kundi C lenye timu nane wakati Kundi A lenye timu nane pia, kuna 'vita' kali kati ikizihusisha African Lyon (23), Ashanti United (22) na KMC FC (21).
Nipashe tunaishauri kamati ya uendeshaji wa ligi kuhakikisha mechi zote za kila raundi zinachezwa kwa wakati mmoja kuhakikisha hakuna timu inayopanga matokeo.
Pia tunatoa rai kwa marefa wa ligi hiyo kuhakikisha wanasimamia mechi za ligi hiyo kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2015 na Sheria 17 za Soka kwa manufaa ya soka la Tanzania na maendeleo ya taifa kwa ujumla.