Mbeya City FC yabadili kikosi ikiivaa JKT Ruvu leo

04Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Mbeya City FC yabadili kikosi ikiivaa JKT Ruvu leo
  • **Timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya imeshinda mechi tatu tu kati ya 16 ilizocheza msimu huu.

BAADA ya kuambulia pointi nne katika mechi tano zilizopita, benchi la ufundi la Mbeya City FC limeamua kufumua kikosi ili kupata matokeo mazuri katika mechi yao ya leo dhidi ya JKT Ruvu jijini Dar es Salaam.

City inayonolewa na meja mstaafu, Abdul Mingange, inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu baada ya kushinda mara tatu tu na kuambulia sare mara tano katika mechi 16 ilizocheza hadi sasa.
Kutokana na kuruhusu mabao sita na kufunga goli moja katika mechi mbili zilizopita ilizopoteza dhidi ya Ndanda FC na 'vibonde' Kagera Sugar, kocha msaidizi wa City, Mohamed Kijuso, ametangaza kukifumua kikosi chake ili kukinusu kuporomoka daraja akianzia na mechi yao ya leo kwenye Uwanja wa Karume dhidi ya JKT Ruvu.
“Tulikuwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye majeraha kikosini huku pia kikosi chetu kikiingia kwenye mtihani wa wachezaji kupata adhabu za kadi," Kijuso alikaririwa kwenye mtandao rasmi wa klabu hiyo jana.
"Tumeliweka sawa hili na Alhamisi hii baadhi watakuwa sehemu ya mchezo, lengo letu ni kuhakikisha tunapata matokeo ndiyo maana tumeamua kubadili kikosi ili kuongeza nguvu."
Kabla ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Jumapili, City ilikumbana na kipigo kikubwa zaidi (4-1 dhidi ya Ndanda) tangu ipande Ligi Kuu msimu wa 2013/14 huku Haruna Shamte akilimwa kadi nyekundu na kuungana na Haruna Moshi 'Boban' aliyetolewa kwa adhabu hiyo katika ushindi wao wa 1-0 nyumbani dhidi ya Mwadui FC Januari 16.
“Haikutarajiwa, morari imeshuka kabisa kutokana na matokeo hayo, kama kocha, ninayo nafasi ya kuwatuliza vijana wangu na kuwarudisha kwenye ushindani. Nataka kuingia uwanjani nikiwa na wachezaji wenye ari,' aliongeza kocha huyo.
City imeyumba kutokana na kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu,Juma Mwambusi na nyota wao wengi wakiwano Deus Kaseke aliyetimkia Yanga, Peter Mwalyanzi (Simba), Paul Nonga (Mwadui & Yanga), Antony Matogolo (Mwadui) huku mkali wa vichwa Mwagane Yeya akijikita kwenye fani yake ya ualimu.
Kikosi cha Abdallah 'King' Kibadeni ambacho hakijaonja utamu wa ushindi wa Ligi Kuu tangu Desemba 26 kilipoitungua Ndanda FC mabao 3-1 mjini Mtwara, kitaingia uwanjani leo kikiwa na kumbukumbu ya kuambulia pointi moja katika mechi tatu zilizopita ambazo kilipoteza dhidi ya Mgambo (5-1) na Simba (2-0) kabla ya kutoka suluhu na Majimaji FC Jumamosi.
Timu hiyo kimeshinda mechi tatu tu msimu huu (sawa na City) kikiwa na pointi 13 kwenye nafasi ya 13, moja mbele ya janga la kuporomoka daraja.
Mechi nyingine ya raundi ya 17 leo itawakutanisha Coastal Union na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.