Wabunge CCM walivyogeuka mbogo kodi ya kiinua mgongo

15Jun 2016
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wabunge CCM walivyogeuka mbogo kodi ya kiinua mgongo

WASWAHILI wanausemi usemao ‘Ukitaka kujua ukali wa nyoka mkanyage mkia’, usemi huu umejionyesha wazi kwa wabunge wakati wakichangia mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2016/17.

Mwenyekiti wa Kamati, Hawa Ghasia

Hii ni kwa sababu serikali imependekeza kufanya marekebisho kwenye sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332, kwa kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano.

Akiwasilisha mapendekezo Jumatano iliyopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, anasema lengo la wabunge kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chao ni kujenga misingi ya usawa na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi.

Wakati wabunge wakibanwa kwenye maslahi yao, mapendekezo hayo kwenye sheria hiyo pia yamedhamiria kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato yanayotokana na ajira kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9.

Dk. Mpango anasema hatua hiyo inachukuliwa ikiwa ni sehemu ya dhamira ya serikali ya kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyakazi hatua kwa hatua hadi kufikia kiwango cha tarakimu moja.

Hatua hii ya serikali imeonekana kuwa mwiba kwa wabunge; wachache wakiunga mkono huku wengi wakipinga mapendekezo hayo.

Hata hivyo, Katika kile kinachoonekana kuwaunganisha wabunge wa upinzani na CCM, ni hatua ya kupendekeza kiinua mgongo cha Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kukatwa kodi, ambapo Kamati ya Bunge ya Bajeti na Kambi ya upinzani wameshauri makato hayo pia yafanywe kwa viongozi wakuu wa kisiasa.

KAMATI YA BAJETI

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Ghasia, akiwasilisha maoni ya kamati yake, anasema kwa miaka mingi Bunge limekuwa mstari wa mbele kujadili na kupendekeza watumishi wa umma kusamehewa kodi kwenye malipo yao ya kiinua mgongo wanavyolipwa.

“Bunge limekuwa likishauri hivi ukizingatia kuwa mishahara ya watumishi wa umma na hata viongozi wa siasa imekuwa ikikatwa kodi, hivyo hatua hii inayopendekezwa na Serikali inakuwa ‘double taxation’ (ikimaanisha kutozwa kodi mara mbili),” anasema Ghasia ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM).

Anasema ni muhimu Serikali ikafikiria suala hilo upya kwa kurekebisha kodi hiyo na kama iishindikana ijumuishe viongozi wote wa kisiasa na si wabunge pekee.

KAMBI RASMI YA UPINZANI

Akiwasilishwa hotuba ya maoni ya kambi hiyo, Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde, anasema wapinzani hawana tatizo na pendekezo hilo la serikali, ila inaitaka serikali kwenda mbali zaidi kwa kuifanyia marekebisho sheria ya mafao ya viongozi ambayo kwa sasa imewapa misamaha ya kodi ya kiinua mgongo.

“Kambi ya Upinzani inaunga mkono serikali kukata kodi asilimia 5 katika kiinua mgongo cha wabunge na kwamba katika jitihada za kuongeza mapato, kambi hiyo haina tatizo na pendekezo hilo la serikali,” anasema Silinde ambaye pia ni mbunge wa Momba (Chadema).

“Kambi hii inataka serikali kwenda mbali zaidi kwa kuifanyia marekebisho sheria ya mafao ya viongozi wa kisiasa ambayo kwa sasa inawapa misamaha ya kodi ya kiinua mgongo viongozi wakuu wa kisiasa kama Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Spika, Naibu Spika, Wakuu wa mikoa na Wilaya ili sasa nao walipe kodi hiyo.”

WABUNGE WAGEUKA ‘MBOGO’

Wabunge wanasema uamuzi huo siyo sahihi kwa kuwa utaminya maslahi yao na kulenga kuwasukuma kuwa ombaomba baada ya kustaafu.

Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, anaeleza hatua hiyo ya Serikali haiwatakii mema kwa sababu imelenga kukipunguza hata kile kiasi kidogo wanachojidundulizia ili kiwasaidie wakiwa wamestaafu ubunge.

Kwa mujibu wa Lugola, fedha wanazopata huishia kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo mara nyingi wabunge huombwa kuchangia michango ya wananchi wanaopatwa matatizo majimboni.

“Waziri wa Fedha anapaswa kufahamu kuwa sisi wabunge mshahara wetu ni mdogo sana kuliko wake na hatuna pensheni. Anapaswa kutambua kuwa, kule mitaani wabunge wamegeuzwa ATM kwa kuombwa fedha karibu na kila mtu, hivyo kuhitaji kuachiwa kiinua mgongo chetu kama kilivyo,” anasema Lugola.

Hata hivyo, wadadisi wanapinga hoja ya Lugola kwa kuwa kila mtu huwajibika kuchangia misiba, harusi, ujenzi wa miradi ya maendeleo kama zahanati au shule.

Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, anasema Ofisi ya Mbunge ni taasisi inayojitegemea na kwamba fedha zinazoonekana nyingi si za mbunge, bali ni za jamii, hivyo kukata kodi katika kiinua mgongo cha mbunge ni kumuumiza.

Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Lucy Mahenga anasema suala la kiinua mgongo cha wabunge serikali imegusa pabaya na kama inawezekana liwekwe vizuri.

Hata hivyo, Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Faustine Ndungulile, anasema Waziri wa fedha awasaidie nini lengo la kuweka hoja hiyo ya kiinua mgongo kwenye bajeti hiyo kwa sababu wameingia 2015 na kumaliza 2020.

“Inabidi utuambie lengo ni nini, au kama alivyosema Lugola ni kuwabipu wabunge, lakini huwezi ukaweka usawa katika kuwapofua wenzako kama kuna watu vipofu na wewe unawapofua ili muwe sawa nadhani hii si mantiki sahihi, kama ni masuala ya kiinua mgongo tusilenge kikundi kimoja tuangalie kote,” anasema Mbunge huyo.

Anasema unapolenga kundi moja unaleta mashaka kwa lengo hilo.

Akitoa maoni nje ya Bunge kuhusu Bajeti hiyo, Mbunge wa Igunga (CCM), Dalaly Kafumu, anasema wanashangazwa kwa nini kodi hiyo imetangazwa sasa hivi, wakati wabunge wanamaliza muda wao 2020/21 na kwamba wataangalia na mihimili mingine kama inakatwa kodi kwenye mafao yao.

Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, anasema eneo hilo kutakuwa na ubishani mkubwa kwanza ni kwa nini wabunge na mbunge hapati mafao bali anapata kiinua mgongo na kwa kawaida mafao hayatozwi kodi.

Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, anasema: “Hakuna sababu ya kutendewa tofauti na Watanzania wengine, hili suala la sisi kukatwa kiinua mgongo linaweza kuleta mjadala, lakini sisi ni sehemu ya Watanzania tunapaswa kulipa kodi na kama kuna maboresho yatafanyika.”