Demokrasia, Amani na Maendeleo

15Jun 2016
Bangila Balinsi
Nipashe
Demokrasia, Amani na Maendeleo

KUNA aina tatu za mifumo ya utawala wa nchi na himaya mbalimbali popote duniani.

rais john magufuli siku aliyoapishwa kuwa rais wa Tanzania

Utawala wa Kidemokrasia, Utawala wa kiimla au kidikiteta na Utawala wa kifalme.

Kwa bahati mbaya utawala wa kifalme mara nyingi umechukuliwa kuwa kama sehemu ya utawala wa kiimla ingawa ukichunguza kwa makini utabaini kwamba kuna tofauti kutokana na jinsi kila mfumo unavyopatikana.

Bila kuingia kwa undani katika kuchambua mifumo hii, itoshe tu kusema kwamba kwa madhumuni ya makala haya tutakubaliana na wale wanaougawa utawala wowote katika mifumo miwili tu kwamba au ni wa kidemokrasia au ni wa kidikiteta.

Tafiti zilizofanyika kuhusu mambo ya utawala bora zimebaini kuwapo kwa uhusiano mkubwa kati ya mambo matatu yaani demokrasia, amni na maendeleo bila kujali aina ya mfumo unaotumika kutawala.

Aidha, imedhihirika kupitia tafiti hizi kwamba nchi zenye mfumo wa utawala wa kidemokrasia zinafanya vizuri zaidi katika kupata maendeleo kuliko nchi zilizo katika utawala wa kiimla.

Imedhihirika pia kuwa nchi zinazoendeshwa kwa kufuata misingi ya utawala wa kidemokrasia zina amani na utulivu zaidi ya nchi zinazoendeshwa kwa mfumo wa kidikiteta. Hata hivyo, ni vyema kuweka mambo sawa kwa kuweka maangalizo.

Angalizo la kwanza naomba ifahamike kwamba demokrasia ina maana tofauti katika jamii mbalimbali ingawa misingi yake imefanana kwa kiasi kikubwa.

Angalizo jingine muhimu tunapojadili mifumo ya kiutawala ni kwamba hakuna utawala wa kidemokrasia uliokamilika yaani asilimia mia moja na vivyo hivyo kwenye utawala wa kidikteta.

Aidha, ni vyema tujue kwamba nchi zimegawanywa katika makundi kwamba kuna nchi zilizokomaa katika demokrasia hizi ni zile ambazo misingi ya demokarsia imjengeka vizuri na inafuatwa kwa kiasi kikubwa.

Mfano ni nchi ya Marekani na zile zilizokuwa zikijulikana kama za Ulaya magharibi.

Kundi la pili ni lile la nchi zenye demokradia changa, hizi ni zile ambazo bado misingi ya utawala wa kidemokrasia haijajengeka vizuri na kukomaa na kwa hivyo mara kwa mara zinajikuta katika matatizo ya migongano ya kutawala kwa kuchanganya utawala wa kiimla na utawala wa kidemokrasia. Mfano wanchi hizi ni Afrika na Asia.

Ili kuweza kwenda vizuri pamoja kwanza tuangalie misingi ya utawala wa kidemokrasia ni hipi. Wachambuzi wa mambo ya utawala wa kidemokrasia wanataja misingi ya utawala wa kidemokrasia kuwa ni uhuru, haki, utu, na uhuru wa kushiriki. Tutafafanua:

Uhuru kama msingi wa demokrasia una maana ya mtu au kikundi cha watu kuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yao bila kuingiliwa ili mradi hawavunji sheria. Haki kama msingi wa demokrasia ina maana ya kila mtu ana haki ya kupata haki ya kujitetea na kulinda haki yake kupitia mfumo wa kimahama (judiciary).

Utu kama msingi wa democrasia ina maana ya uwepo wa haki za binadamu kama zilivyo katika Tangazo la haki za binadamu la Umoja wa mataifa la 1948.

Aidha uhuru wa kushiriki katika demokrasia una maana ya wananchi kushiriki katika utawala kwa kuchagua serikali itakayo endesha mambo kwa niaba yao na kuchagua wawakilishi wa kuisimamia yaani wabunge ili isiendeshe mambo kinyume na makubaliano.

Ili misingi hii ya demokrasia iweze kuzingatiwa kunapaswa kuwe na nguzo au vyombo vinavyo saidia katika kutawala nchi kidemokrasia.

Nguzo hizi ni pamoja na kuwepo kwa katiba ya nchi, kuwepo na kutenganishwa kwa madaraka na majukumu ya mihimili ya dola yaani serikali, bunge na mahakama.

Nguzo ya demokrasia ni hati au sheria ya haki za wananchi (A bill of rights for citizen), hati hii ndiyo inayoorodhesha mambo yote ya haki za msingi za watu.

Hapa tunapata mambo kama uhuru wa kwenda unapotaka, wa kuabudu, wa kutoa mawazo yako, wa vyombo vya habari, uhuru wa kumiliki mali na mambo mengine kama hayo.

Nguzo nyingine muhimu katika utawala wa kidemokrasia ni wa kujumuika katika vikundi mbalimbali kama kuanzisha ushirika au chama.

Ni katika nguzo hii tunapata vyama vya siasa na hivyo kuwa na utaratibu wa vyama vingi vya siasa katika nchi. Kutokana na vyama hivi tunapata ushindani wa kila chama kutaka kuongoza kwa kushika dola.

Nyingine ni utawala wa sheria. Hii ina maana kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria kwa maana kwamba watu wote wanafuata sheria bila kubagua na wote wako chini ya sheria.

Ni wazi kwamba kwa misingi niliyoeleza hapo juu, ili kupata maendeleo Tanzania tunahitaji nchi yetu iendeshwe kidemokrasia.

Kwa maana nyingine kama kuna kiongozi anayetaka kuleta maendeleo nchini mwetu au mahali pengine popote basi ajue na azingatie utatu wa Demokrasia, Amani na Maendeleo!

Haya ni mambo ambayo yanaenda pamoja na haiwezekani kuacha moja na kisha mtu akajigamba kwamba atafanikisha jingine.

Ili kupata maendeleo kunahitajika kuwepo amani na utulivu na ili kupata amani na utulivu kunahitajika kuwepo na utawala wa kidemokrasia.

Haya ni mashariti ya ili kupata kimoja lazima vingine viwili viwepo. Hii ni kama vile kutaka kupata hewa ukaa huku ukiwa na chokaa yakulazimu kuwa na tindikali!

Sasa katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na mambo yanayoashiria demokrasia kuminywa; kwa sababu hiyo ni vyema tukayatazama kwa ukaribu zaidi maana tunaweza kujidumbukiza katika ukosefu wa amani na hivyo kujikuta tunajicheleweshea maedeleo tunayoyataka.

Mathalani tumesema katika utawala wa demokrasia lazima kuwepo na uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kupata habari; hivyo kitendo cha kuzuia bunge ‘live’ ni wazi masharti hayo yamekiukwa na hivyo demokrasia imevurugwa.

Tumeona pia umuhimu wa uhuru wa mtu kwenda apendako (freedom of movement), uhuru wa kutoa maoni (freedom of speech), uhuru wa kujumuika na uhuru wa kusikilizwa. Kwa kadri mambo yanayofanywa na jeshi la polisi kwa hivi sasa ni vigumu kukubali kwamba nguzo hizi hazivunjwi.

Siku hizi tunasikia mikutano ya vya vya siasa ikipigwa marufuku kwa kisingizio ambacho hakina ushahidi.

Tunaambiwa tu kwamba kuna taarifa za kiintelijesia kutakuwa na uvunjifu wa amani. Ni vigumu kuamini maneno hayo kwa vile polisi ni chombo cha dola na viongozi wakuu wa dola wamesikika wakisema mikutano ya vyama vya siasa hawaitaki.

Lakini jambo lililoshangaza zaidi ni pale polisi ilipozuia kongamano la ACT- Wazalendo lilokuwa lijadili bajeti. Hili ni kongamano linalofanyika ukumbini na hakuna uwezekano wa watu kuwa wengi kiasi kwamba hata kama wangeamua kufanya fujo polisi ingeshindwa kuwadhibiti.

Kwa hiyo inaonekana wazi kwamba demokrasia imeminywa kwa kuvunja nguzo inayowapa watu haki ya kutoa mawazo.

Aidha, kumekuwa na mambo yanayoonyesha mhimili mmoja kuingilia mwingine.

Kama tulivyoona katika utawala wa kidemokrasia lazima madaraka ya mhimili moja yasiingilie uhuru na madaraka ya mhimili mwingine. Jambo hili limekuwa likikipigiwa kelele sana kwa mhimili wa dola kuingilia mahakama na hata bunge.

Jambo jingine na labda la hatari sana ni pale ambapo makundi ya wachache hayasikilizwi. Kitendo cha wabunge wa upinzani kuachwa kusikilizwa eti kwa kuwa ni wachache mpaka kufikia mahali pa kususia bunge ni jambo la kusikitisha sana.

Bunge ni chombo muhimu au nguzo muhimu katika utawala wa kidemokrasia. Hili ni jambo liliopaswa kutafutiwa ufumbuzi mara moja badala ya kila upande kuendeleza ubabe.

Kwa ushauri wa kumaliza mgogoro huu unaodhohofisha demokrasia pande zote katika mgogoro zizingatie yafuatayo. Kwanza upande wa walio wengi na ambao unamuunga mkono Naibu Spika uzingatie ukweli kwamba hata wachache wanastahili kusikilizwa.

Katika demokrasia, kuwapuuza kwa sababu tu ya wingi wa wabunge wa CCM na si kwa sababu ya hoja haileti maana. Hapo demokrasia inageuka kandamizi kwa kisingizio cha wingi.