Ni wakati wa kuishi kama mashetani kwa kukatwa kodi ya kiinua mgono

12Jun 2016
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Ni wakati wa kuishi kama mashetani kwa kukatwa kodi ya kiinua mgono

BAJETI ya serikali kwa mwaka huu imewasilishwa bungeni wiki hii na kuainisha vyanzo vya ukusanyaji wa kodi kuwa ni pamoja na vinywaji baridi na vilevi, miamala ya simu, gesi, mafao ya wabunge, ada za usajili wa magari kwa namba za kawaida pamoja na majina binafsi.

rais john magufuli

Kinachowaumiza wawakilishi ni kuguswa mafao yao, hatua hiyo sasa ni kidonda kilichochomwa na mwiba, wabunge wanalalamika hawataki kusikia.

Bunge limeanza kuijadili bajeti hiyo lakini kikubwa ni pale walipoguswa panapouma kwa kutakiwa kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo jambo ambalo limewafanya wawe wakali katika kuchangia hoja hiyo.

Siku ambayo Waziri aliwasilisha bajeti hiyo aliposoma kipengele hicho wabunge walianzisha minong'ono iliyomlazima Naibu Spika, kuwatuliza kwa kuwaeleza kuwa watakuwa na nafasi ya kuijadili hivyo watulie Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, amalize kuwasilisha bajeti hiyo.

Katika mjadala ulioanza mwishoni mwa wiki baadhi ya wabunge walisema haikubaliki kukatwa kodi kwenye mafao yao kwa kuwa kazi yao siyo ajira bali ni ya kujitolea zaidi na katika majimbo yao wamegeuzwa kuwa mashine za kutoa fedha au ATM, kwa kuhudumia watu pamoja na shughuli za maeneo na kijamii.

Walisema hawatakubali suala hilo kwa kuwa linapunguza fedha zao ambazo wameziita ni kidogo na kuilamu serikali kuwa inataka wanapostaafu waanze kuwa ombaomba na kwamba tangu serikali zilizopita hawakuwahi kukatwa kodi na sasa hawatakubali.

Wabunge wanakuwa na kawaida kuwa linapokuja suala la kugusa mafao yao wanakuwa wakali na kuacha yanayogusa wananchi wengi yaende kama yalivyo jambo ambalo linaonyesha kiwango cha ubinafsi walichonacho.

Mathalani, katika bajeti hiyo wananchi wa kawaida wameguswa na kodi katika miamala ya simu, unapotoa fedha katika ATM huku wafanyakazi wakiwa na kodi mara mbili, lakini huwezi kuwasikia wakilitilia mkazo hilo zaidi ya kupigia kelele kukatwa kodi.

Waheshimiwa wanapigia kelele kipengele kimoja cha bajeti na kuacha kujadili hoja nzima kwa maslahi ya taifa.

Tena mbunge aliyejitahidi sana huanzisha matatizo ya wananchi wake kwenye jimbo kwa uchache na humsikii akishawishi wengine kukataa suala hilo ila la kukatwa kodi wanataka kuungana.

Imekuwa kawaida kwa wabunge kuweka mbele maslahi yao na yanapoguswawanakuwa wakali kama nyuki, mathalani wakati wa mjadala wa posho za vikao, mafao yao katika Bunge la 10 jambo ambalo linaonyesha kuwa cha kwanza ni maslahi yao binafsi na si ya wananchi waliowatuma, inashangaza waheshimwa.

Wanapaswa kuwa mfano kama kweli wanamuunga mkono Rais John Magufuli, katika ukusanyaji kodi ili kuiwezesha nchi kujiendesha kwa fedha zake yenyewe na kupunguza au kuondokana na utegemezi kabisa, wakubali kulipa kodi hiyo.

Vinginevyo, wapinge suala hilo kwa watumishi wote kwa kuwa wenye ajira za muda mfupi ni wengi, kama wenye mikataba ya muda mfupi na wengine na siyo kujionea huruma wenyewe kwa kisingizio wao ndiyo wanagharamia mambo mengi kwenye majimbo.

Kisingizio kuwa ni kazi ha kujitolea zaidi hakina msingi kwa kuwa ingekuwa hivyo kusingekuwa na mpambano mkali kwenye majimbo wakati wa uchaguzi, kiasi cha wengine kutumia fedha nyingi ili kutinga bungeni na hata kutoana roho na kukimbilia mahakamani wanaposhindwa..

Kwa Tanzania zipo kazi nyingi za kujitolea lakini ubunge umekuwa kimbilio la wengi hata wasomi wabobezi kuacha taaluma, wapo ambao wamepata maradhi ya moyo baada ya kuukosa ubunge na wametumia fedha nyingi, hivyo uhalisia ni kuwa ni kazi yenye maslahi mengi manono kwao ndiyo maana hakuna anayekubali kuacha uheshimiwa kirahisi.

Tunahitaji kuona mjadala wa bajeti wenye afya kwa wananchi wote tena wabunge kupaza sauti kwa niaba ya wananchi wao juu ya namna bajeti itakavyotekelezwa akiakisi maisha halisi ya wapiga kura.

Mathalani, serikali inasema itahakikisha maji safi na salama yanapatikana kwa wananchi wote, lakini bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ni ndogo na haina tumaini la kupeleka miradi ya maji itakayoondoa kero zilizopo.

Licha ya bajeti kuwa na vyanzo vile vile ambavyo wengine huviita vya’ dhambi’kutokana na ulevi kusababisha matendo yasiyokubalika kama fujo na vipigo, sigara nazo zinasababisha magonjwa kama saratani. Na kwamba maeneo haya ni sehemu zinazotumiwa miaka yote kukusanya kodi, lakini ni lazima wabunge wakubali kuwa nchi hii ni ya wote na kila mmoja achangie maendeleo hata akiwa mheshimiwa.

Sawa, hakuna ubunifu wa kukusanya mapato kwenye nyanzo vingine kama vya uvuvi, mafuta ghafi ya kula, ardhi pamoja na nyumba, lakini waheshimiwa wanatakiwa waviibue , tena wakatwe kodi kuongeza mapato.

Ikumbukwe kuwa mjadala wa bajeti mwaka huu utahusisha wabunge wa CCM pekee , baada ya wale wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, kususia vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson, kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wake.