Kwa msingi huo serikali yoyote hufanya kila juhudi kuimarisha uchumi pamoja na mambo mengine, kujenga uhusiano mzuri na wadau wenzake wa uchumi ndani ya nchi.
Hao ni kama wapanga sera, wadau wa kilimo na mifugo, wafanyabiashara na waendesha shughuli zinazotoa msaada kwa kufanikisha biashara kama nishati, usafirishaji, mawasiliano na utangazaji, miongoni mwa shughuli nyingine.
Hata hivyo, ni wazi wadau wakubwa wa uchumi ni wafanyabiashara wa biashara tofauti wanaojumuisha wauza bidhaa, watoa huduma, makandarasi wa ujenzi,wenye viwanda, wasafirishaji na wengine.
Ukweli huu unathibitishwa na maana ya neno uchumi kwenye kamusi nyingi za lugha tofauti kuwa “mfumo ambao ndani yake fedha, viwanda na bishara ya nchi au eneo fulani vinaendeshwa kwa utaratibu maalum”.Hapo imetajwa fedha,viwanda na biashara.
Fedha inamilikiwa na serikali lakini inazungushwa ndani ya mfumo wa matumizi wa nchi au eneo, zaidi, kwa njia ya biashara za wafanyabiashara.
Biashara na viwanda ni shughuli za wafanyabiashara. Kwa maana hiyo uchumi ni biashara na biashara ni uchumi. Hata kilimo na mifugo haviwezi kuchangia uchumi wa nchi visipoingizwa kwenye biashara kwa pande zote; mazao ya chakula na ya biashara.
Kujitosheleza kwa chakula ni moja ya njia za kufanikisha malengo sahihi ya kiuchumi. Kujitosheleza kwa chakula hukamilika kwa taratibu za kibiashara.
Kwa hiyo kwenye mipango ya uchumi, kila sehemu wafanyabiashara wapo.
Kwa hiyo ukitaka kufanikiwa kiuchumi unapaswa usiwabane sana wafanyabiashara kwa mambo ambayo ukiyalegeza hakuna uvunjifu wa sheria wala hasara na usiwalegezee sana kiasi cha kuwafanya wavuruge mipango ya nchi.
Usiwe moto wala baridi kwao, kuwa wa uvuguvugu. Kwa mfano, kama taasisi za umma zinataka kufanya majadiliano yoyote yenye tija kwa maendeleo ya taasisi hizo na taifa na zinahitaji kufanya majadiliano hayo sehemu tulivu yenye vifaa vya kufanikisha vikao hivyo, taasisi hizo ziruhusiwe kufanya majadiliano hayo hotelini.
Mazungumzo hayo, kwa maana ya mafunzo, semina, utayarishaji wa sera na kuandaa mipango yafanyike huko kwa kibali cha bodi ya wakurugenzi ya taasisi baada ya kuridhika kwamba ni magumu kufanyika pengine popote isipokuwa hotelini, yawe ya kuleta tija kwa taasisi na taifa pia bajeti yake itoshe kwa shughuli hiyo.
Baada ya mazungumzo hayo, lazima taarifa yake iwasilishwe kwa bodi ya wakurugenzi ikionesha gharama iliyotumika na faida inayotarajiwa kupatikana toka mazungumzo hayo.
Kwa njia hii, taasisi za umma zitanufaika kihalali kupitia huduma za hoteli.
Wafanyabiasha watanufaika kihalali kupitia kipato halali cha kuwawezesha kuongeza faida kuimarisha biashara zao. Wananchi watanufaika kwa kulindiwa ajira zao mahotelini.Mifuko ya hifadhi ya jamii itanufaika kwa kuwa na wanachama wa kutosha toka mahotelini.
Serikali itanufaika kwa kupunguziwa changamoto ya ajira, kuongezeka kwa makusanyo ya kodi ya mapato kupitia kipato kikubwa cha biashara ya hoteli na mishahara ya wafanyakazi wengi wa hoteli pamoja na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha.
Ukizuia kabisa majadiliano hayo mahotelini, utakachopata ni kinyume cha hayo yote; ajira mahotelini zitaathirika, mifuko ya hifadhi ya jamii itapoteza wanachama wengi, changamoto ya ajira itaongezeka, makusanyo ya kodi ya mapato toka mahotelini itapungua na mzunguko wa pesa utapungua.
Kama majadiliano hayo yatafanywa kwenye kumbi za taasisi za umma tu maana yake ni kwamba taasisi hizo zitakazopata pesa za kuhudumia majadiliano hayo zitatunza pesa hiyo na hazitaizungusha kwa sababu si taasisi za kibiashara.
Aidha, taasisi hizo hazitaongeza ajira bali zitabaki na waajiriwa wale wale watakaochangia kodi ya mishahara ile ile.
Jambo la kuzingatia hapa ni ukweli kwamba kama ni matumizi yaliyopangiwa bajeti, matumizi hayo yatabaki yale yale semina ikifanyika hotelini au kwenye ukumbi wa taasisi kwani kote malipo yatakuwepo. Kitakachoyatofautisha ni kiwango cha malipo hayo, suala linalohitaji mjadala kibiashara wa kiasi cha malipo.
Kuruhusu mikutano ya taasisi kufanywa mahotelini kihalali naona ni njia ya kuwawezesha wafanyabiashara wa mahoteli kupanua biashara zao pamoja na kuinua uchumi wa nchi.
Vipato hivyo hivyo ndivyo vitakavyowawezesha kuanzisha viwanda, mpango mkubwa kuliko yote tuliyonayo kwa sasa.
Picha inayojaribu kujichora sasa kwamba serikali inapambana na wafanyabiashara, si picha nzuri kwa maendeleo ya kiuchumi.
Hatari ni kwamba wafanyabiashara wakishashawishika kwamba hali ni hiyo watafanya mambo kadhaa ya kuihujumu nchi kiuchumi ili kuikwamisha serikali. Matokeo yake uchumi utayumba na wananchi watateseka.
Ni ushauri wangu serikali ianze utaratibu rasmi wa kukutana na wafanyabishara mara kwa mara kubadilishana mawazo ya yapi yafanyike bila kuathiri pande hizo mbili ili kila upande unufaike na uchumi uwe imara.










