Tumechangia sana harusi ni wakati wa kugeukia elimu

12Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Tumechangia sana harusi ni wakati wa kugeukia elimu

HIVI karibuni wakazi wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera waishio maeneo mbalimbali nchini, walikutana jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuchangia madawati ikiwa ni kuunga mkono agizo la Rais John Magufuli, la kuhakikisha kila mwanafunzi anakalia dawati ifikapo mwishoni wa mwezi huu.

madawati

Mkutano huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa kwani kwa muda wa saa tano pekee ahadi za madawati 400 zilitolewa na wajumbe walioshiriki.

Uamuzi huo uliochukuliwa na wakazi wa Kyerwa ni wa busara ambao ungefaa kuigwa na Watanzania wengine, ambao wengi wana kawaida ya kukutana kwa ajili ya kuchangia harusi na hafla mbalimbali.

Kuchangia elimu ni jambo la msingi ambalo Wanakreywa wameliona na kuamua kuhamasishana kwa ajili ya kufikia lengo lililowekwa na Mkuu wa nchi kwamba mwishoni mwa mwezi Juni, kuwe na madawati ya kutosha kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Imekuwa kawaida kuona vikao vya harusi kila kukicha lakini ni nadra kusikia aina ya mikusanyiko kama hii iliyofanywa na wananchi hawa wa Kyerwa waishio jijini Dar es Salaam ya kuchangia elimu.

Wametoa somo kwa jamii kwamba sasa kuna haja ya kutafakari njia zao na kubadili mtazamo ili kujielekeza kuchangia elimu kama inavyofanyika kwenye harusi, kipaimara, ubatizo na mahafali na wakati mwingine misiba.

Kuitisha mkutano kama huo wa Wanakyerwa si utamaduni wa Watanzania wengi kwani imezoeleka vikao kama hivyo vya kuchangia elimu hufanywa katika nchi jirani za Kenya na Uganda.

Wanakyerwa wamekuwa wa kwanza kuonyesha mfano kwamba inawezekana Tanzania nayo ikaanzisha zama mpya za vikao vya kuchangia elimu hivyo bila shaka wengine wataiga utamaduni huo mpya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo, , Albert Katagira, alipokuwa akifungua mkutano aliwaambia kuwa kuna haja ya kubadilika na kuanza kuona umuhimu wa kujitoa kwa ajili ya elimu kama ambavyo watu wamekuwa wakijitoa kwa ajili ya harusi.

Katagira alisema kwa muda mrefu kumekuwa na kawaida ya kuitegemea serikali katika kuleta maendeleo katika jamii dhana ambayo alisema imewafanya watanzania kuwa wagumu hasa pale wanapotakiwa kuchangia mambo yenye tija kama elimu.

Alisema watu wengi wamekuwa wepesi kuchangia harusi na sherehe kuliko kuchangia elimu, wagonjwa na watu wenye uhitaji tofauti na jirani zetu Kenya na watanzania wa maeneo ya Kaskazini.

Aliwasifu Wazanzibari kwa kujenga utamaduni wa kuchangishana kwa lengo la kuinua jamii zao hasa kielimu hivyo ni vyema Watanzania wakaiga jambo hilo jema.

“Wakati umefika nasi kubadilika na kutambua kuwa maendeleo ya kweli katika jamii na taifa lazima yaletwe na sisi wenyewe na mara zote tukumbuke Kyerwa ya leo na ijayo itajengwa nasisi wanakyerwa wenyewe, na katika muktadha huo Tanzania yetu lazima ijengwe nasisi wenyewe,” alisema Katagira.

Msisitizo kama huo wa Mwenyekiti huyo ulirudiwa pia na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Philip Mpango, wakati akiwasilisha bungeni bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, aliposema kuwa kumekuwa na kawaida ya kuchangia shughuli za starehe lakini masuala ya maendeleo kama elimu hayachangiwi.

Waziri Mpango alisema Watanzania wanapaswa kubadilika na kutoa kipaumbele kwa michango inayohusu masuala ya maendeleo kama elimu kwa uzito ule ule wanaoutoa wanapochangia shughuli kama harusi, kipaimara na sherehe za siku za kuzaliwa.

Ingawa ukweli ni kwamba harusi zitaendelea kuwepo na zitachangiwa lakini kinachosisitizwa hapa ni kwa watanzania kubadilika na kuipa michango ya elimu uzito uleule kama wanavyochangia harusi na hafla mbalimbali.

Ni kawaida kupita kwenye kumbi za sherehe na kukuta vikao lukuki vingi vikiwa ni kwa ajili ya kuchangia harysi na sherehe mbalimbali lakini sasa kwa uzito kama huo tugeukie elimu.

Mojawapo wa kumbi hizo ni Msimbazi Center siku za Jumamosi na Jumapili , mambo ni ya kushangaza utaona namna uwanja ule mkubwa ulivyojaa pomoni kiasi cha wakati wengine watu kukosa viti, na ukiuliza kinachoendelea kwenye mikusanyiko hiyo, utashangaa vingi ni michango ya harusi.

Si jambo baya kuchangia harusi lakini kuna umuhimu ifike wakati kumbi na viwanja kama Msimbazi Center vijae pia kwa ajili ya kuchangishana kwa ajili ya maendeleo ya elimu ili Tanzania ifikie wakati majirani waone fahari kusomesha watoto wao hapa.

Kama ambavyo miaka ya nyuma Watanzania walikuwa wakiona fahari kuwapeleka watoto wao kusoma nchi za Uganda na Kenya, ufike wakati sasa iwe kinyume chake, yaani wazazi wa nchi hizo waone fahari kuwaleta watoto wao kusoma nchini Tanzania.

Hilo linawezekana na wala si ndoto ya mchana, linawezekana iwapo Watanzania watakuwa pamoja kimoja na watashikamana na kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya elimu ya nchi yao kama walivyoanza wakazi wa Kyerwa na viongozi wao.