Mapango ya Amboni yalivyo na sinema iliyojaa hofu

09Jun 2016
Lulu George
Tanga
Nipashe
Mapango ya Amboni yalivyo na sinema iliyojaa hofu

Eneo yalipo mapango ya Amboni katika Kata ya Kiomoni wilaya ya Tanga. Ni umbali wa kilomita nane kutoka katikakati ya jiji la Tanga, kupitia barabara kuu inayoelekea Mombasa.

Asili ya mapango yanaelezwa kitaalamu kwamba yalitokana na mabadiliko ya nguvu ya asili zilizobadilisha miamba ya chokaa, wastani wa miaka 150 milioni iliyopita.

Utafiti uliofanywa katika eneo hilo la mapango, unaeleza asili yake ilikuwa chini ya usawa wa maji miaka milioni 20 iliyopita.

Eneo hilo lina ukubwa wa kilomita za mraba 234 lenye mazingira ya mawe ya chokaa. Ni mahali kunakopitwa na mito ya asili.

MAAJABU NDANI YA MAPANGO

Mapango hayo yamekuwa na maajabu mbalimbali yakiwemo kuwapo njia za kutokea Mombasa, Kenya kupitia ndani mapango hayo.

Aidha, ndani ya mapango kunaonyesha kuwapo njia panda. Mojawapo inasadikiwa kwenda eneo la Maweni Tanga na nyingine, Mombasa.

Zipo simulizi mbalimbali ikiwemo inalyohusu raia wawili wa Kizungu walioonekana mwaka 1941 wakielekea mapangoni humo. Inadaiwa wenyeji waliwashauri wasiingie na mbwa.

Walishauriwa waingie na mwongozaji anayejua njia za mapangoni, walipuuza ushauri huo na walivyoingia, hawakuwahi kuonekana tena wakitoka katika eneo hilo, bali mbwa wao alionekana kando mwa mlima Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro.

MAFICHO YA WAHALIFU

Hata hivyo, historia ya kujificha wahalifu nayo ipo ndani ya mapango hayo. Inadaiwa kati ya mwaka 1922 na, walikuwapo wanaharakati waliokuwa wakiendesha harakati za kupambana na walowezi waliokuwa wamewekeza katika maeneo ya Tanga.

Watu hao (majina tunayo) mmoja akidaiwa ni raia wa Kenya na mwingine Mtanganyika, wanadaiwa walipora mali na kutishia maisha za walowezi.

Katika kipindi hicho, serikali ya kikoloni iliwatambua kuwa wahalifu na kujaribu kuwakamata bila mafanikio kwa kipindi kirefu.

Pango ambalo watu hao walidaiwa kuishi, linaonekana mithili ya chumba kidogo chenye urefu kwenda juu ambako ndani yake. Walitengeneza chanja na kujificha humo, kiasi cha wana usalama wa kikoloni wasiwaone walipoingia mapangoni kuwasaka.

Hata hivyo, simulizi zinaonyesha kwamba mwaka 1957, mmoja ambaye ni Mtannganyika alipgiwa risasi katika maeneo ya Lushoto na kufariki na mwaka uliofuata (1958), Mkenya naye alipigwa risasi na kufariki hukohuko Lushoto, ambako makaburi yao yanadaiwa kuwako.

Wananchi wa kawaida wanawakumbuka wakiwatafsiru kuwa ‘mashujaa’.

Mapema mwanzoni mwezi Februari mwaka jana katika eneo la Amboni palitokea mapigano makali, baina ya watu waliosadikiwa kuwa na silaha za kivita na askari.

Ni sekeseke liliosababisha baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kukimbia nyumba zao na kusimamisha shughuli za kiuchumi.

Watu wanaodaiwa kuwa majambazi ambao walisababisha kutokea mashambulizi baina yao na askari Polisi na Jeshi la Wananchi (JWTZ), hata kuishia katika kifo cha askari mmoja na majeruhi watano, wana historia ya kuishi kama raia wema kwa kipindi chote kijijini hapo.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Majimoto walieeleza namna walivyoishi na watu hao kwa zaidi ya miezi sita, huku wakiwasifu jinsi walivyokuwa wachangamfu na wacheshi katika maisha yao ya kawaida.

Wanasema hawakuwa wakijumuika na wakazi wa maeneo hayo muda mwingi, licha ya kwamba walishirikiana na wanawataja walikuwa ‘wacheshi’ kila walipoonana.

Kwa mujibu wa wanakijiji, walijua watu hao ni vibarua wa kilimo katika mashamba yaliyoko kwenye Pori la Mbogo, ndani ya eneo hilo la Amboni.

Yahya Adam ni mkazi wa Majimoto anayeismulia kwamba, katika kipindi chote hicho, watu hao walipendelea kuvaa mavazi ya aina ya mashati ya mikono mirefu, suruali maarufu kama jeans ambazo zimekatwa chini (hazigusi kiatu) na wakati mwingine kanzu.

“Hawa bwana walikuwa wanavaa ‘short jeans’ yaani wamekaa kijihadi zaidi na yeboyebo chini, lakini mashati yao ni mikono mirefu na kanzu wakati mwingine walikuwa wanavaa na kofia juu ya Barakshia.

“Ni wachangamfu sana, ukikutana nao huwezi kuwashtukia kama ni wageni, kwani utahisi wanakujua tu kutokana na salamu za kuchangamka,” anasema Adam.

Naye Bakari Alli, anasema watu hao walikuwa wakionekana kwenye maeneo ya magenge kunapouzwa bidhaa kama unga, dagaa na nyanya wakinunua nyakati za mchana na kutoweka kusikojulikana.

“Walikuwa wakitembea wawili wawili na walikuwa wakija gengeni wananunua nyanya,dagaa na hata unga, halafu wanashika njia ya porini na kutokomea. Kusema kweli wote wananchi wa hapa tulikuwa tukijua ni wakulima,“ anasema Alli.

Anaongeza kuwa watu hao walionekana kila siku kuanzia saa 12.00 asubuhi wakitokea eneo la mashambani na wakidhani ni wakulima waliohamia eneo hilo.

“Kusema kweli mimi ni mpasua mawe, ndiyo shughuli yangu kubwa ya kiuchumi. Sasa kila siku alfajiri tunapotoka na wenzangu kwenda kazini, tunakutana na hawa watu tukawa tunajua kuwa ni wakulima.

“Kwani kwenye Pori la Mbogo ambako kuna shamba kubwa na ndipo tukikutana nao na wanatembea wawili wawili. Leo unakutana na wengine na kesho unakutana na wengine,” anasema Alli.

Kuhusu mwonekano wao, walikuwa i watu wa kawaida na tabia ya uchangamfu, ka,a vile waliishi maeneo hayo kwa muda mrefu, hali iliyowafanya wakazi kutokuwa na shaka nao.

SIKU YA TUKIO

Nini kilitokea siku ya tukio?
Kwa mujibu wa viijana wa Kijiji cha Majimoto ambao kazi yao kubwa ni kupasua mawe, wanasema walikuwa wamekaa kijiwe chao cha kila siku.

Walishangazwa kuona majira ya saa 5.00 asubuhi, gari mbili za Polisi maarufu kama FFU zikipita kuelekea kwenye eneo la machimbo, jambo lililowafanya nao wakimbilie huko wakijua kumepatikana madini.

Wanasema wakati wakiongozana kukimbilia kwenye eneo hilo wakiwa wanane, ndipo askari mmoja alipowafuata na kuwataka wawasaidie kuwaelekeza njia kwenye eneo la mapori ambako watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walikimbilia.

“Alikuwa askari Polisi mmoja, wakati sisi tunaelekea kule walipoelekea wao. Akili yetu ilituambia pengine kuna madini yamevumbuliwa na ndipo akatuomba tuongozane na tugawane njia watano wakae upande wa Mashariki wa pori watatu wakae Magharibi, halafu twende hadi tuje kukutana katikati,” anasema Saidi.

“Ghafla si ndio tunasikia milio ya risasi, heee! wenzetu wawili wakatukimbia tukabaki sita,” anasema Said.

Anasema waliendelea chini ya maelekezo ya Polisi, lakini kilichowatisha ni baada ya kuona wameachwa peke yao porini bila silaha yoyote ya kujitetea, huku wakiagizwa kupiga simu kwa askari huyo iwapo watamwona mtu ambaye si mkazi wa eneo hilo.

“Kauli hizo zilitutisha, tutakaaje porini peke yetu bila hata silaha yoyote ya kujikingia na hatujui hao tunaoambiwa tuwaangalie ni kina nani,” anasimulia Saidi na kuendelea:

“Kweli tuliwekwa kati tena katika wakati mgumu sana mpaka inafika saa 11.00 jioni, njaa zimetuzidia.

“Tukaamua kumpigia simu yule askari akasema hatuwezi kuondoka ni lazima tulale nao huko porini kuwasaka hao watu na walituma Sh. 30,000 za chakula,” anasema.

Kwa mujibu wa Said, baada ya kuchachamaa sana kutaka kuondoka ndipo askari walipowataka waongozane hadi kwenye pango ambalo wahalifu walikuwa wakiishi na ndiko kulikopatikana pikipiki mbili, unga, dagaa, sufuria na baiskeli tatu.

“Pale walipiga mabomu kwanza, tuliambiwa tuache midomo wazi ili tusipate madhara na baada ya mabomu hayo, ndiyo wakaingia kwenye pango na kukatolewa vitu hivyo.

“Kusema kweli sisi tulikuwa tumechoka sana na tulikuwa na wasiwasi na familia zetu, kwani hakuna aliyekuwa anajua tumepotelea wapi na hali mirindimo ya risasi na mabomu ikiendelea,” anasimulia.

Saidi anasema kutokana na hali hiyo, yeye na wenzake watano walilazimika kuwakimbia askari kurudi makwao, ili kuondoa hofu kwa familia zao ambao walihisi tayari walishauawa.

HISTORIA YAJIRUDIA

Hivi karibuni, serikali mkoa wa Tanga ilitoa ufafanuzi kuhusiana na watu waliojificha kwenye mapango ya Amboni, kwamba ni wahamiaji haramu walioingia nchini na kutumia mapango hayo kama maficho.

Wahamiaji wanaotuhumiwa kuhusika na matukio ya uhalifu na mauaji.
Aprili mwaka huu, waliuawa watu watano kwa kupigwa risasi na wanasaidikiwa kuwa ni majambazi, baada ya kuvamia duka la bidhaa za jumla.

Pia siku chache zilizopita, watu wanane kutoka familia tatu tofauti waliuawa kwa kuchinjwa na mapanga na watu wanaosadikiwa majambazi katika kitongoji cha Mabatini, kata ya Mzizima wilaya ya Tanga.

Ni tukio lililotokea usiku wa Mei 31 mwaka huu.

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela anasema kwa sasa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza mauaji hayo na anawataka wananchi kuondoa hofu, kutokana kwani ulinzi umeimarishwa kwenye makazi hayo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Ernest Mangu, ni miongoni mwa waliofika kushuhudia hali halisi na kuwapa pole wafiwa.

Wakati hayo yakiendelea, kikosi kazi cha pamoja cha Polisi na Jeshi la Wananchi (JWTZ), wanaendelea na doria kuwasaka wahusika.