Niyonzima aliyekuwa anasumbuliwa na malaria na UTI, alikosa mechi ya Jumamosi pamoja na wakali wengine kadhaa wa Yanga wakiwamo kiungo Geofrey Mwashiuya na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' na kushuhudia timu yao ikipoteza mechi yao ya kwanza msimu huu baada ya kucheza mechi zote 15 za mzunguko bila kuacha pointi tatu kwa wapinzani.
Imeelezwa kuwa kiungo huyo wa kimataifa kutoka Rwanda ambaye hakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga katika 12 zilizopita za mashindano yote, wakishinda nane na kutoka sare mara tatu, amepona na anatarajiwa kuanza kesho.
Meneja wa Yanga, Hafidh Salehe, aliliambia Nipashe jana kuwa naodha huyo wa timu ya taifa ya Rwanda 'Amavubi' sasa yuko fiti.
"Tunashukuru Niyonzima amepona na jioni ya leo (jana) ataendelea na mazoezi na wenzake," alisema Salehe.
Niyonzima amekuwa nje ya kikosi cha Mdachi Pluijm baada ya kuwa na mvutano na uongozi wa Yanga ambao ulitangaza kuvunja mkataba wake kabla ya kumrejesha ukimtuhumu kwa utovu wa nidhamu.
Kiongozi huyo wa Jangwani (Salehe) alisema kikosi chao sasa kimeimarika zaidi kutokana na kupona kwa wachezaji wao waliokuwa wagonjwa na majeruhi.
Hata hivyo, Yanga itakosa huduma ya beki wake wa kati asiyekosa penalti, Kelvin Yondani ambaye atalazimika kuwa nje ya kikosi katika mechi mbili zijazo baada ya kulimwa kadi nyekundu na refa Andew Shamba dakika ya mwisho ya mechi yao iliyopita dhidi ya Coastal.
Licha ya kupoteza mechi ya Jumamosi, Yanga wameendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na pointi 39 baada ya mechi 16, pointi 12 mbele ya Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya saba, lakini timu hiyo ya Mbeya ina mechi moja ya kiporo dhidi ya Azam FC.
Niyonzima gado kuwavaa Prisons
02Feb 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Niyonzima gado kuwavaa Prisons
- *Kiungo huyo wa kimataifa kutoka Rwanda hakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga katika 12 zilizopita, wakishinda 8, sare 3 na kupoteza moja.
KIUNGO fundi Haruna Niyonzima alikuwa jukwaani wakati Yanga ikichapwa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union jijini Tanga Jumamosi kutokana na kuugua, lakini sasa yuko 'fiti' kusaka ushindi wa kwanza wa Wanajangwani mwezi huu watakapoikabili Prisons mjini Mbeya kesho.










