Gia kwa gia hadi makundi Kombe la Shirikisho

23May 2016
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Gia kwa gia hadi makundi Kombe la Shirikisho

ILIKUWA hoi hoi nderemo na vifijo wakati mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga walipogusa ardhi ya nchi yao, wakitokea Angola licha ya kufungwa bao 1-0, walifanikiwa kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe Shirikisho Afrika (CAF).

kikosi cha yanga wakiwa mazoezini.

Wanachama na mshabiki wa Yanga walimiminika kwa wingi Ijumaa mchana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakiimba na kucheza, wakichagizwa na ushindi wa mabao 2-0 ilioupata nyumbani kabla ya mechi hiyo ya ugenini.

Yanga imeweza kuingia hatua ya makundi ya michuano ya Afrika kwa mara ya pili baada ya miaka 18.

Mwaka 1998, klabu hiyo ilifanikiwa kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini miaka 18 baadaye imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Lakini pia Yanga imekuwa timu ya kwanza Tanzania kuweza kuingia kwenye makundi Afrika baada ya miaka 13.
Mara ya mwisho timu ya Tanzania kufanya hivyo ilikuwa Simba ilipotinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.

Haikuwa kazi rahisi kwa Yanga kuweza kutinga hatua hiyo, kwani ilibidi itokwe machozi, jasho na damu.

Ilipitia kwenye njia zenye miiba, miamba, milima na mabonde hadi kuingia hatua hiyo.
Imecheza mechi nane, imeshinda nne, sare mbili na kufungwa mbili.

Mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma, anaongoza kwa kufunga magoli matatu kwenye michuano hiyo ya kimataifa, huku mwenzake kiungo Thabani Kamusoko akifunga mawili.

Mwandishi wa makala haya anakukumbusha safari nzima ya Yanga hadi kufikia hapo.

1. Cercle de Joachim 0-1 Yanga

Safari ndefu ya Yanga ilianza Februari 13 mwaka huu, ilipocheza mechi ya awali na timu ya Cercle de Joachim ya Mauritius.

Ilikuwa ni michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipokwenda ugenini na kushinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe, nchini Mauritius.

Bao pekee kwenye mechi hiyo lilifungwa na mshambuliaji hatari wa timu hiyo Donald Ngoma dakika ya 17 ya mchezo.

2. Yanga 2-0 Cercle de Joachim

Timu hizo zilirudiana tena Februari 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, Yanga iliendeleza ushindi kwa kuichapa Cercle de Joachim mabao 2-0. Yalikuwa ni mabao ya Amissi Tambwe dakika ya tatu ya mchezo, kabla ya Thabani Kamusoko kuongeza goli la pili.

Ushindi huo uliifanya timu hiyo kufanikiwa kuingia hatua ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-0.

3. APR 1-2 Yanga

Yanga iliendelea na safari yake, ilipocheza dhidi ya APR ya ugenini Uwanja wa Amahoro jijini Kigali Machi 12, 2016.
Ilikuwa ni mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na ikaibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Alikuwa ni Juma Abdul aliyefunga bao dakika ya 20, kabla ya Kamusoko kuandika bao la pili dakika ya 74.
Kwenye dakika ya majeruhi APR ilifanikiwa kupata bao pekee lililofungwa na Patrick Sibomana.

4. Yanga 1-1 APR

Mabingwa wa soka Tanzania Yanga walilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya APR nyumbani Uwanja wa Taifa na kuifanya kusonga mbele kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2.

Kwenye mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza iliyochezwa Machi 19 mwaka huu, Fiston Nkinzingabo alianza kuiandikia APR bao la kwanza, kabla ya Donald Ngoma kusawazisha dakika ya 28 na mechi ikamalizika kwa idadi hiyo ya magoli.

5. Yanga 1-1 Al Ahly

Yanga ikaendelea na safari yake na sasa ikalazimika kupambana na vigogo Al Ahly kutoka Misri kwenye mechi raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa.

Mechi ya kwanza ilichezea Aprili 9 mwaka huu Uwanja wa Taifa na timu hizo zote zikatoka sare ya bao 1-1.

Al Ahly ilianza kupata bao dakika ya 11 lililofungwa na Amri Gamal, kabla Yanga haijasawazisha bao hilo ambalo Wamisri hao walijifunga wenyewe kupitia kwa Ahmed Hegazy, aliyeshindwa kuokoa vyema krosi ya Issoufou Boubacar.

6. Al Ahly 2-1 Yanga

Mechi ya pili ya raundi ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika ilichezwa mjini Alexandria Misri na Yanga ilipoteza kwa kuchapwa mabao 2-1. Mechi ilichezwa Aprili 20 mwaka huu.

Al Ahly ilianza kupata bao dakika ya 51 kupitia kwa Hossam Ghaly, kabla ya Donald Ngoma kusawazisha bao hilo dakika ya 66.

Ilikuwa ni dakika ya mwisho kati tano za nyongeza, Al Ahly ilipata bao la pili kupitia kwa Abdallah Said.
Matokeo ya mechi hiyo ya jumla ya mabao 3-2 yakaitoa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa na kuitupa kwenye Kombe la Shirikisho.

Ikumbukwe kuwa timu nane zilizotolewa kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa zinapelekwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na kukutana na timu nane zilizoingia hatua hiyo kucheza mechi za mtoano ili kupata timu nane.

7. Yanga 2-0 Esperanca

Yanga ilikuwa ni moja kati ya timu nane zilizotupwa kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kupigwa kumbo Ligi ya Mabingwa.

Ikapangwa kucheza na Grupo Desportivo Sagrada Esperanca ya Angola.

Mechi ya kwanza ilichezwa jijini Dar es Salaam Mei 7 mwaka huu, na Yanga ikaondoka na ushindi wa mabao 2-0.
Ilibidi isubiri hadi dakika ya 71, Simon Msuva alipofunga bao la kwanza na Matheo Anthony kupachika goli la pili dakika ya kwanza kati ya tatu za nyongeza.

8. Esperanca 1-0 Yanga

Licha ya kufungwa bao 1-0, Yanga ikafanikiwa kufuzu hatua ya makundi kutokana na ushindi wake wa mabao 2-0 ilioupata nyumbani.

Ikiwa nchini Angola Mei 18, ilichapwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Love Kabungula dakika ya 24.

Shukrani zimuendee kipa Deogratius Munishi aliyeokoa penalti ya Kabungula dakika ya 87 na kuifanya Yanga kukamilisha safari yake ndefu ya kutinga hatua ya makundi Afrika.