Katika zama za vita vya ‘ukombozi’ wakiwa porini hadi kuweza kuingia madarakani mwaka 1986, watu hawa walikuwa marafiki na nyendo zao zilikuwa moja katika harakati hizo, kabla ya kutibuana mbele ya safari.
Hivi sasa Dk. Besigye yuko gerezani katika msukosuko wa kisiasa unaohusiana na matokeo ya uchaguzi ya hivi karibuni, lakini hii si mara ya kwanza, ni jambo lililozoeleka kila wakati wa kampeni za uchaguzi au matokeo yanapotangazwa.
Itakumbukwa katika uchaguzi wa mwaka 2001, Dk. Besigye akiwa mgombea anayepeperusha bendera ya muungano wa vikundi vya upinzani waliyojiita kama ‘Movement for Change’ au maarufu Movement, alimtikisa sana Museveni, ingawaje hata hivyo, katika matokeo ya mwisho aliambulia kura zisizozidi asilimia 30.
Nyendo za Movement zinawasifu unaoshabihiana na Ukawa ambao tumeushuhudia kwenye uchaguzi nchini hivi karibuni, ikiwamo kaulimbiu yao waliyotamka ‘Movement for Change’ huku Ukawa wakitamka ‘M4C’ lakini zote zikibeba ujumbe mmoja wa kutaka mabadiliko.
Wakati wa kampeni, Dk. Besigye alikumbwa na misukosuko itokanayo na kauli zake ikiwamo kusakwa na polisi, kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani kwake na mara kadhaa alishikiliwa na polisi.
Aidha, katika maisha hayo hayo ya kuwa ‘wanted’ kuna wakati alilazimika kukimbilia ughaibuni ikiwamo nchini Misri na baadaye alirejea nchini Uganda na daima hajawahi kujiengua kutoka katika harakati za kisiasa na hususani zinazolenga kumwondoa madarakani Museveni.
UCHAGUZI 2016
Besigye, ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu, safari hii mara tu baada ya uchaguzi amejikuta anadondokoea mikononi mwa polisi na simulizi hizo hivi sasa zimeshamfikisha gerezani.
Ilikuwaje? Mara tu baada ya uchaguzi kufanyika na matokeo kutangazwa, mshindi akiwa ni Yoweri Museveni (71), Dk. Besigye aliibuka na mbwembwe zake mbele za umma akijitambulisha kuwa mshindi, na akaona hiyo haitoshi, alipiga hatua zaidi ya kujiapisha kuwa rais.
Lilikuwa ni tukio linalofanana na kukanyaga mkia wa nyoka dhidi ya mpinzani wake, kwani mamlaka za dola mara moja zilichukua hatua za kisheria na kutafsiri vifungu vya sheria vilivyokiukwa na Dk. Besigye, ambaye sasa ana hadhi ya ‘mshtakiwa’.
Anachodaiwa kukiuka hadi kuwekwa ‘sero’ ni uhaini uliosababishwa ni kitendo chake cha kujiapisha ‘kinyemela.’
Kitendo hicho kilimpeleka katika gereza la Moroto Kaskazini Mashariki mwa nchi, lakini amehamishiwa kwenda gereza la Luzira lililo jijini Kampala, ambalo linatajwa kuwa ndilo gereza kubwa zaidi nchini humo.
Kisa cha Dk. Besigye kuingia kwenye msukosuko huo ni kusambaa kwa video moja mitandaoni inayomwonyesha akijiapisha kuwa rais.
MUSEVENI
Wakati swahiba wa zamani akiwa gerezani, Rais wa Yoweri Museveni ameapishwa ‘chini ya ulinzi’ Alhamisi iliyopita kuongoza kwa miaka mingine mitano.
Museveni aliapishwa huku Dk. Besigye akikamatwa na mitandao ya kijamii kuzimwa na wadadisi wa mambo walitafsiri mikakati hiyo kuwa ni ‘mwendelezo’ wa misukosuko.
Kuapishwa kwa Rais Museveni (71), kunamaanisha kwamba atakuwa madarakani kwa miaka 35 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mwingine baada ya miaka mitano.
“Waganda wamekuwa wakishiriki uchaguzi wa vyama vingi kwa miaka kadhaa sasa na katika uchaguzi wa mwisho aliyeshinda ni mgombea Museveni na ndiyo maana anaapishwa," alisema Badru Kiggundu, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Uganda.
Dk. Besigye aliye kada na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC), aliingia kwenye msukosuko mpya baada ya kuapishwa siku moja kabla ya hafla ya kuapishwa kwa Rais Museveni.
Kabla ya kutuhumiwa kwa uhaini, wakati wa kampeni za uchaguzi, Dk. Besigye alishakamatwa mara kadhaa na baada ya kumalizika kwa uchaguzi, aliwekwa kifungo cha nyumbani, akizuiwa kabisa kutoka eneo la nyumbani kwake.
Katika tukio hilo, Dk. Besigye aliwekwa kizuizini nyumbani kwake kwa siku 55, lakini hata hivyo alijitangazia ushindi.
Wakati wanaharakati wa haki za binadamu wakiona anachofanyiwa Dk. Besigye ni uonevu na unyanyasaji, Polisi inasema ilimzuia kama njia ya ‘kumsaidia’ asitende makosa ambayo yangemtia kwenye matatizo zaidi.
Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa baada ya video ya kuapishwa kwake kutolewa, Dk. Besigye aliwapiga chenga walinzi wake na kuingia mitaani, hatua iliyolilaazimu jeshi la polisi kumkamata.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, Patrick Onyango, alikaririwa akisema kuwa kilichosababisha mpinzani huyo kutiwa nguvuni ni kwa sababu alikaidi amri halali na kuwaongoza kundi la watu kuvuruga amani.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali ni kwamba Dk. Besigye alijiapisha siku ambayo Serikali iliizima mitandao ya kijamii ya Facebook, twitter na WhatsApp, ambapo watumiaji walishindwa kuingia kwenye akaunti zao za mitandao hiyo.
Mbali ya hilo, Polisi wa kutuliza ghasia walisambazwa katika maeneo mengi ya mji wa Kampala ambako maduka mengi yalifungwa; tukio lililofuatiwa na kichapo kwa wafuasi wanaomuunga mkono Dk. Besigye.
Kabla hata ya kujiapisha kwa Dk. Besigye, mpinzani mwingine, Amama Mbabazi, alijaribu kuzuia ushindi wa Museveni mahakamani, lakini aligonga mwamba baada ya Mahakama ya juu kabisa nchini humo, kuhalalisha ushindi wa asilimia 60 kwa muhula mwingine.
Katika hukumu yake, Mahakama hiyo ilisema kuwa uchaguzi wa Februari umempa ushindi Museveni na pia ulikuwa huru na wa haki.










