Matokeo ya juhudi hizo ni watuhumiwa kuchukuliwa hatua kama kufukishwa mahakamani.
Hatua hizo zimeonyesha kuungwa mkono na wasomi, wananchi, washirika wa maendeleo na mataifa mbalimbali ya nje.
Kutokana na juhudi hizo za Rais Magufuli, makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yameongezeka kutoka Sh. bilioni 900 hadi Sh. trilioni 1.3 kwa mwezi.
Pia, Serikali imeboresha ukusanyaji wa mapato katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuhimiza matumizi ya mfumo wa kielektroniki.
Pia serikali imeendelea kuokoa hasara ya fedha zilizokuwa zikisababiswa na watumishi hewa ambapo ilimeshapoteza zaidi ya Sh. bilioni 11.6 kutokana na kuwalipa mishahara watumishi hewa.
Staili hii ya utumbuaji majibu imeleta nidhamu ya maisha kama anavyoeleza Mbunge wa Jimbo la Mkuranga (CCM), Abdallah Ulega.
Ulenga anasema anaunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kutumbua majipu kwani zimekuwa zikimpa nguvu na moyo wa kuwatumikia wananchi wake na majukumu mengine ya serikali.
Anasema juhudi hizo za Rais Magufuli zinazolenga kuwainua wanyonge na wale wasiojiweza pia zinamfundisha nidhamu ya maisha.
“Utaratibu huu wa Rais Magufuli unanipa kuwa na nidhamu ya maisha kuanzia nyumbani kwangu namna ninavyopanga bajeti na mambo mengine.
Anasema akiwa kazini pia anafanya kazi kwa nidhamu ya hali ya juu ili kuhakikisha anatimiza wajibu wake na kutokuwa chanzo cha kukwamisha juhudi za Rais Magufuli.
Ulega pia anasema kuwa, Rais Magufuli anafundisha namna ya kuwa na maisha bora na siyo ya maisha ya anasa pamoja na kufanya kazi kwa bidii.
“Tunaweza kusema kuwa, ile dhana ya kuishi kwa ujanja ujanja imepitwa na wakati isipokuwa tumebaki na dhana ya kufanya kazi kwa bidiii ili kufikia malengo na kupata mahitaji yako,” anasema.
Kuhusu tofauti ya Serikali ya awamu ya nne ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na awamu ya tano ya Rais John Magufuli, anasema ipo kwenye usimamizi na utendaji kazi.
Awali ya nne ya serikali Kikwete kazi zilikuwa zikifanyika, lakini utiliaji mkazo haukuwa kama ilivyo sasa.
“Kama ilivyo Rais Magufuli amekuja na slogan mpya ya kuwa ‘hapa kazi tu’ hivyo kila Mtanzania anawajibu wa kufanya kazi ili kufikia malengo yake,” anasema.
Anasema tofauti kati ya serikali ya awamu ya nne na hii ya tano ni kuwa, watu walikuwa wakifanya kazi kwa mazoea hali hiyo imebadilika ghafla na kinachofanyika ni kufanya kazi kwa kasi ya ajabu.
“Ule utaratibu wa watu kufanya kazi kwa mazoea sasa umepitwa na wakati kama ni kazi unatakiwa kufanya kazi kweli kweli,” anasema Ulega.
Anasema Watanzania wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kutaka kuona nchi ikipiga hatua na kupunguza umasikini.
UTUMBUAJI MAJIBU
Ulenga anasema haoni sababu ya Rais Magufuli kusita kutumbua majibu kwa watendaji wasio waaminifu na kwamba azidi kuongeza juhudi za utumbuaji huo.
“Mimi naunga mkono utumbuaji majipu…akazane watu kama sisi tuko nyuma yake, tumefika mahali ambapo wala rushwa na mafisadi hawana tena nafasi katika nchi yetu,” alisema Ulega.
Anasema dawa ya watendaji wasio waadilifu katika nchi ni kutumbuliwa, kwani hawana huruma na maendeleo ya Taifa.
“Watu kama hawawezi watumbuliwe tu, hakuna namna ya kuwaacha,” anasema.
Kuhusu tofauti ya bunge lililopita na la sasa anasema: “Kipindi cha bunge lililopita nilikuwa nje ya bunge nikishuhudia kama Mkuu wa Wilaya, lakini sasa niko ndani ya bunge naona kuna tofauti kubwa sana.”
Anasema anajivunia kuwa mbunge katika bunge hilo na kwamba nidhamu na utumishi uliotukuka ndivyo ambavyo vinatawala.
Anasema bunge hilo lenye vijana weledi na wakada tofauti tofauti linawapa changamoto ya kuwa mtendaji na kutaka kutekeleza majukumu yake kwa wakati.
MIAKA MITANO INATOSHA
Ulega akizungumzia utumishi wake wa miaka mitano ya jimbo la Mkuranga, anasema anatarajia kuwafanyia kazi wananchi na kutekeleza yale waliyoyaahidi.
“Niliomba kuwa mbunge kwa miaka mitano na ninachofanya ni kutekeleza ahadi nilizozitoa kwa wananchi wangu kabla ya muda wangu kuisha, kama ni kuendelea wao ndio wataamua siyo mimi tena,” anasema.
Anasema anachokiona mbele yake ni kufanya kazi kwa bidii na kuwakomboa wananchi wa Mkuranga na mengine ni majaliwa na siyo mipango.
“Siwezi kusema nataka nifanye kazi ili nirudi tena bungeni, bali nafanya kazi ili wananchi wangu wapate kile walichokitarajia kutoka kwangu na wao ndio wataamua,” anasema Ulega.
MAJUKUMU YA JIMBO
Ulega anasema jukumu kubwa alilonalo kwenye jimbo lake ni kutatua kero zinazowakabili wananchi ambazo ni maji, barabara, huduma za afya na kilimo cha zao la korosho.
Anasema anampango wa kupandisha hadhi barabara ya Kisiju-Mkuranga ili kuwa ya mkoa kutokana na kuhudumia watu wengi.
Anasema barabara nyingine zinazotakiwa kufanyiwa ukarabati ni barabara ya Kimanzichana-Msanga, Vikundu-Mvinzi-Sambatini.
Anasema kwa upande wa vituo vya Afya na Zahanati bado vijiji vyake vingi havijapata zahanati.
Anasema kati ya vijiji 125 vilivyoko katika jimbo lake, vijiji 90 havina Zahanati wakati mpango wa serikali ni kuwa na zahanati katika kila kijiji.
Anasema ili kutekeleza mpango wa kujenga zahanati na vituo vya afya atajenga kwanza miundombinu ambapo wamepanga kununua magreda kwa ajili ya kuchonga barabara hizo.
Ulega anasema pia upande wa maji mchakato unaendelea wa kuchimba visima na kuvuna maji ya mvua.
Kuhusu kilimo ambacho wakazi hao wanategemea hasa kilimo cha korosho, ataendelea na jitihada za kuishinikiza serikali kupeleka pembejeo za kilimo.
Anasema pia kuwawezesha wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao na kuondokana na ulanguzi wa zao la korosho.










