Siasa za jino kwa jino zimerudi Zanzibar ?

18May 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Siasa za jino kwa jino zimerudi Zanzibar ?

WAKATI wananchi wanahitaji maendeleo na wana shauku kuona ahadi walizoahidiwa na wanasiasa wakati wa kampeni zinatekelezwa, Zanzibar imejikita katika mvutano ambao wafuatiliaji wa mambo wanahoji mvutano huo mpaka lini.

maalim seif hamad.

Hii ni kwa sababu kiongozi wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharifu Hamad na Dk. Ali Mohamed Shein wanatoa hotuba zinazodhihirisha mvutano mkubwa.

Wanasiasa kutoka pande zote za vyama vikuu vya CCM na CUF pamoja na vyama vyingine walitoa ahadi kibao kuwatumikia wananchi ikiwa pamoja na kuondosha au kupunguza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Miezi kadhaa tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar hali imekuwa tofauti na matarajio ya wananchi waliokuwa wengi bado hayajafikiwa.

Kila kukicha unasikia mvutano kuanzia ngazi ya familia, mitaa, vijiji hadi taifa ambapo baadhi ya watu bado wanaonyesha uhasama wa kisiasa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein tayari ameunda Serikali yake ambayo pamoja na mambo mengine imeahidi kutekeleza ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana.

Dk. Shein anaonekana kutaka kusonga mbele bila ya kusikiliza malalamiko kutoka kwa washindani wake chama cha wananchi CUF, kutokana na mvutano wa kisiasa uliojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ambao ulifutwa.

Katika hutuba zake kuu tatu tangu kuunda Serikali yake mpya, Dk. Shein amewataka wananchi kupuuza maneno ya wapizani na kujikita katika harakati za maendeleo ili kujenga Taifa jipya la Zanzibar na kuondosha umasikini.

“Mimi ndie rais wa Zanzibar ambae nimechaguliwa na wananchi na kupata ushindi wa asilimia 90 sasa wale wanaosema kuwa hawanitambui kazi kwao,” alisema Dk. Shein katika moja ya hotuba zake baada ya kutangazwa mshindi.

Dk. Shein alisema mambo yanayosemwa hayamnyimi usingizi kwani yeye ndie rais wa Zanzibar ambaye alichaguliwa katika uchaguzi wa Machi 20, mwaka huu na kwamba Zanzibar hakutakuwa na uchaguzi mkuu mwingine hadi mwaka 2020.

Alisema hana wasiwasi na uongozi wake huo na atamaliza kipindi chake cha pili cha uongozi kwa mujibu wa katiba kwa salama na amani.

Alisema hana sababu ya kubishana na wanaodai kuwa hawamtambui kuwa ni rais wa Zanzibar licha ya kushinda kwa kishindo kikubwa katika uchaguzi wa Machi 20.

“Asotambua sawa na wanaonitambuwa alhamdulilahi, wananchi ndio waliokuwa waamuzi mimi sikujiamulia mwenyewe, mimi kura yangu ilikuwa moja tu, nyingi walipiga wananchi wote sasa kama leo kuna viongozi wa chama cha siasa wanasema hawanitambui mie niwaambie nini si tutaanza kugombana bure, huo ni uamuzi wao na chama chao na mimi siuingilii,” alisema.

Aidha alisema Serikali anayoiongoza itasimamia misingi ya haki, uwajibikaji, uwazi na usawa kwa wananchi wote, bila ya kumbagua mtu yeyote kutokana na itikadi yake, dini yake, jinsia au eneo analotoka.

Alisema kuwa yeye ndie Rais wa wananchi wote wa Zanzibar hivyo atashirikiana na viongozi mbalimbali, wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, na kadhalika katika kuiletea maendeleo Zanzibar.

“Zanzibar ni yetu sote, viongozi wa vyama vya siasa tuna jukumu la kushikamana na kuwatumikia wananchi kwa ajili ya maendeleo yao,” alisema.

Kwa upande wa mpinzani wake, Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na washauri wake wameapa kumwondoa Dk. Shein madarakani bila ya kumwaga damu, lakini kwa msaada wa ushauri wa washirika wa maendeleo bila ya kutoa ufafanuzi wa kutosha.

Maalim Seif ambaye ni mtu mwenye ushawishi mkubwa kwa siasa za Zanzibar; na viongozi wezake wanasema ushindi wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana ulikuwa ni wa CUF na walinyang’anywa na Dk. Shein kupitia chama chake cha CCM ambaye wanasema ni lazima achie madaraka kutokana na mbinu mbalimbali zinazoendelea kutumika ili warejewe CUF utawala wa Zanzibar.

Maalim Seif anasema Serikali ya Dk. Shein haitamaliza miaka mitano madarakani kama inavyotakiwa kikatiba.

Mwanasiasa huyo ambaye chama chake kilisusia uchaguzi wa marudio wa Machi 20, alisema CUF inaungwa mkono na mataifa makubwa Duniani na zipo hatua mbalimbali ambazo wameelezwa wakizifuata wataiondoa Serikali ya Dk. Shein madarakani.

Alisema hatua hizo watahakikisha wanazifuata ili kuiondoa Serikali ya Dk. Shein madarakani kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020 na kuongeza kuwa wanaosema hakuna uchaguzi mwingine hadi mwaka 2020 wanajidanganya.

Maalim Seif ambaye pia ni katibu mkuu wa CUF, alisema kuwa watahakikisha wanapata nchi yao ambayo ana imani kuwa walishinda Oktoba 25, mwaka jana.

Alieleza kuwa Serikali atakayoiongoza itakuwa na kazi na sio kupita na ving’ora huku hali ya maisha ya wananchi ikiwa ngumu kama ilivyosasa.

“Ninawahakikishia kuwa tutaipata nchi yetu salama usalimini bila ya kumwaga hata tone la damu ili kila mtu awe hai na afurahie serikali yake,” alisema Maalim Seif.

Katika hali kama hiyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakijiuliza masuala mengi na kushindwa kupata majibu baada ya miaka mitano ya furaha na maelewano chini ya mwamvuli wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

“Kwa kweli tunachanganyikiwa kiongozi mmoja anatwambia tusijali tusonge mbele, mwingine anasema tuigomee serikali tusifanye chochote na sote jamii moja kwa kweli ni kazi kubwa sana ingekuwa vyema viongozi wa juu wakatafuta suluhu ya kudumu,” anasema Omar Khamis Ali, mwananchi wa kijiji cha Dunga wilaya ya Kati Unguja.

Anasema ni vyema viongozi wa vyama vya siasa kukaa pamoja na kujadiliana kuhusu mustakabali wa hali ya kisiasa Zanzibar ili wananchi waweze kuendelea na harakati zao za kijamii.

“Wanapolumbana wao viongozi wa juu na wananchi wanapata mwanya wa kuendeleza siasa za chuki na uhasama ambazo hazina tija,” anasema Omar.

Baadhi ya wananchi wamechukizwa watu kugomeana kufanya ibada misikitini, kuhudhuria harusi, mazishi, kukaa pamoja na kushiriki katika harakati za kimaendeleo kwani ni kinyume na mafundisho ya dini pamoja na utamaduni wa Zanzibar.