Museveni, demokrasia na ‘mtangaze fulani’ mshindi

18May 2016
Bangila Balinsi
Dar es Salaam
Nipashe
Museveni, demokrasia na ‘mtangaze fulani’ mshindi

WIKI iliyopita kulikuwa na tukio maalum ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki la kuapishwa kwa rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni.

Rais John Magufuli akiwa na Rais wa Uganda Yoweri Museven

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na marais kadhaa kutoka barani Afrika akiwamo mkongwe wa wakongwe rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Kuapishwa kwa rais Museveni kunahitimisha uchaguzi mkuu wa Uganda uliofanyika Februari na Museveni kutangazwa mshindi kwa asilimia 60.8, akiendelea kubaki madarakani kwa awamu ya tano tangu mwaka 1986.

Hata hivyo, wapinzani nchini humo wakiongozwa na mpinzani mkuu, Kizza Besigye walilalamikia ushindi huo kwani wanadai uchaguzi haukuwa wa huru na wa haki.

Matukio ya kulalamikia matokeo ya chaguzi kuu za kuwapata marais wa nchi mbalimbali barani Afrika yamekuwa mengi na yanatolewa karibu kila mahali unapofanyika uchaguzi.

Hii inatokana na ukweli kwamba tume zinazoendesha chaguzi hizo zinakuwa si huru.

Matokeo yake zinashindwa kutenda haki na hivyo zina wabeba wagombea wa vyama vinavyokuwa madarakani.

Hii ni kwa sababu viongozi waandamizi wa tume hizo ni wateule wa watawala.

Ingawa wanaotangazwa washindi wanakanusha kutokuingilia tume, lakini kunakuwa na ushahidi mwingi wa jinsi mambo yalivyoendeshwa kuanzia kipindi cha kampeni hadi siku ya uchaguzi wenyewe na jinsi matokeo yanavopatikana na kutangazwa.

Mara nyingi wakati wa kampeni vitendo vya kuwaminya wapinzani vinakuwa vya wazi mno.

Tukichukulia mfano wa Uganda mpinzani mkuu wa nchini humo Besigye kipindi chote cha uchaguzi alikuwa akikamatwa mara kwa mara na kuwekwa ndani kwa muda.

Hili linachukuliwa kama la tume ya uchaguzi kwa sababu katika kipindi cha kampeni wagombea wote wanatakiwa kulindwa na kupewa haki sawa ya kunadi sera zao kwa wapiga kura.

Sasa kama mgombea anabugudhiwa na serikali halafu tume inakaa kimya hapo haki iko wapi?

Haya mengine ya tume zetu kuubeba upande moja tumeyashuhudia hapa kwetu Tanzania wakati wa kampeni kwa mgombea wa chama tawala alikuwa akipitiliza muda uliopangwa kufunga kampeni, lakini tume ilikuwa ikilifumbia macho tatizo hilo kana kwamba hawalioni wala hawalijui.

Lakini cha ajabu tatizo kama hilo lilipojitokeza kwa wapinzani basi lilikemewa na kutolewa onyo mara moja.

Mambo mengine yanayoonyesha udhaifu wa tume zetu ni pale ambapo vyombo vya habari vya umma vinapotumika vibaya kwa kutoa habari zinazoonekana kubeba wagombea wa chama kilicho madarakani.

Bila shaka haishangazi sana vyombo vya habari vya umma kuwabeba mabosi wake kwa sababu ndiyo waliowapa kazi kwa kuwateua katika nafasi za uongozi wakubwa wa vyombo hivyo.

Kinacholalamikiwa hapa ni kwanini tume zinakaa kimya upendeleo unapoonyeshwa na vyombo hivi?.

Kwa nini katika kipindi cha uchaguzi tume hazitoi ratiba na muda kwa vyombo hivyo unaotakiwa kutumika kuzungumzia kila chama au wagombea wote kupata nafasi ya kutumia vyombo hivyo kufafanua sera zao?.

Tume zina mamlaka ya kusimamia usawa na ni jukumu lake kuhakikisha uwanja wa kuchezea kwa wagombea uko sawa kwa wote.

Aidha, kunakuwa na malalamiko kwamba vifaa vya kupigia kura vinacheleweshwa sana kwa makusudi katika maeneo mbalimbali ambako inajulikana wazi kwamba wapinzani wana nguvu zaidi.

Mathalani, matatizo kama haya yalilalamikiwa katika uchaguzi wa Uganda. Na kwa hakika ni matatizo yanayojitokeza katika nchi nyingi barani Afrika wakati wa uchaguzi.

Kitu kingine kinacholalamikiwa ni tume kuwatangaza washindi pasipo kushinda.

Kuna mifano kadha ambapo waliotangazwa washindi walipingwa wazi wazi na wakati mwingine vurugu zimeibuka kwa sababu wapiga kura waliona kana kwamba wameibiwa haki yao kwa kutangaziwa mtu ambaye hawakumchagua.

Hapa inasemekana tume inafanya hivyo kwa shinikizo kutoka kwa viongozi walio madarakani, ambao wanalazimisha wao au mtu fulani wanayemtaka atangazwe kuwa ndiye mshindi tofauti na matokeo halisi ya kura zilizopigwa.

Mambo haya kwa hakika yanapotokea yanapoka na kuiua demokrasia katika bara la Afrika.

Kwa kuwa demokrasia ikishamiri mahali popote inakuwa ni chachu ya maendeleo basi kwa kuiua ndani ya bara letu maana yake ni kwamba tunazorotesha maendeleo yetu wenyewe.

Hili linatokana na ukweli kwamba muda mwingi na nguvu nyingi, vinatumika kutuliza ghasia na kusuluhisha migogoro inayotokana na watu kuichezea demokrasia.

Si hivyo tu, maendeleo yanadhorota kutokana na ukweli kwamba kwa kuvuruga demokrasia wahisani wetu wengi na washirika wetu katika maendeleo wanajiondoa katika mipango ya maendeleo tuliyokuwa tushirikiane au watusaidie kwa sababu hawawezi kutoa fedha za walipakodi wao kuchangia uongozi wanaodhani haukuchaguliwa kihalali.

Hapa mfano hautafutwi mbali maana yametupata wenyewe kwa MCC.

Ni jambo la masikitiko tukikumbuka machafuko yaliyotokea Kenya baada ya rais Mwai Kibaki kutangazwa mshidi katika uchaguzi wa mwaka 2007.

Tume ilimtangaza katika mazingira yaliyoashiria kwamba ilikuwa imeshinikizwa kufanya hivyo pasipo uhalisia wa kura zilivyopigwa.

Matokeo yake yalikuwa ni machafuko yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000 na wengine wengi wakikosa makazi na hivyo kuwa wakimbizi.

Kule Zimbabwe pia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2009 yalisababisha vurugu zilizoiacha nchi hiyo katika matatizo mengi mpaka ikalazimu rais Mugabe akubali kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na aliyekuwa mpinzani wake mkuu Morgan Tsvangirai.

Hii ikiwa ni miaka miwili tu tangu Kenya ilipolazimika kufanya hivyo kwa Kibaki kuunda serikali na waziri mkuu Raila Odinga kwa matatizo yanayofanana.

Swali la kujiuliza hapa ni je, wapinzani wanapolalamika kuhusu ‘kuibiwa’ ushindi wanakuwa wanamadai ya kweli? Ingawa hatuwezi kupata jibu la moja kwa moja kwa swali hili kutokana na ukweli kwamba wanaojua ukweli hasa ni tume za uchaguzi na waliowalazimisha kutangaza hivyo, lakini tunaweza kudodosa viashiria kadhaa katika jambo hili.

Kiashiria cha kwanza ni viongozi wetu Afrika wanavyong’angania madaraka na kupenda kutawala maisha. Mifano imetuzunguka.

Tarehe 29 Februari 1986 yaani miaka 30 iliyopita rais Museveni aliapishwa kwa mara ya kwanza kuwa rais wa Uganda baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomg’oa Tito Okelo.

Katika hotuba yake ya kwanza kama rais wa nchi hiyo alisema yafatatayo:

“The people of Africa, the people of Uganda are entitled to a democratic government. It is not a favor from any regime.” Mwisho wa kunukuu. Kwa tafasiri yangu isiyo rasmi Museveni alisema watu wa Afrika, watu wa Uganda wanastahili/ wanahaki ya kuwa na serikali ya kidemokrasia. Na hayo si matakwa ya watawala wowote.

Aidha katika hotuba hiyo maarufu na ya kihistoria rais Museveni aliendelea kusema na nanukuu: “The main problem of Africa is of leaders who don’t want to leave power”. Mwisho wa kunukuu. Kwa tafsiri yangu anasema:

Tatizo la Afrika ni viongozi wasiopenda kuachia madaraka. Kauli hizi mbili ni nzito na nzuri. Hizi ni kauli zilizotolewa na kiongozi mwanamapinduzi mzalendo wa Afrika.

Kusikiliza aliyoyasema rais Museveni miaka takribani 30 iliyopita na ukaangalia anavyotenda leo unapata kiashiria kwamba huyu ni kiongozi aliyekwisha kunogewa madaraka na hata hakumbuki aliyoyasema.

Kwa hiyo akipita mtu akakwambia huyu kalazimisha atangazwe kuwa mshindi unakuwa na sababu ya maana ya kumsikiliza kama siyo kumwamini kabisa.

Kwa bahati mbaya viongozi wa aina ya rais Museveni ni wengi sana Afrika tunao akina Paul Kagame, Robert Mugabe, Piere Nkrunzinza, kwa kutaja wachache.

Kwa bahati mbaya zaidi kama inavyoonekana Afrika Mashariki tumekuwa vinara katika hili ikijumlisha pia mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar na ukweli kwamba hata uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wapinzani hadi leo wanaamini walishinda.

Kiashiria kingine tunachoweza kutazama kubaini kama kuna ukweli katika demokrasia kubakwa kwa kutumia tume kutangaza mshindi ni ukweli kwamba baadhi ya nchi katika Afrika zimeng’ang’ania sheria ya kuzuia matokeo ya kura za urais yasihojiwe mahakamani.

Hii ni sheria inayoonyesha kwamba wanaotaka ibaki wanajua wanavyofaidika nayo kwa vile wanatumia fursa hiyo kuiba uchaguzi huku wakiwa na uhakika wapinzani wao hawana njia nyingine bali kukubali.

Kwa kujua kwamba kuna sheria mbovu inayoweza kuwalida katika uovu wa kuiba uchaguzi viongozi wetu wemeendelea kuhakikisha sheria hii inabaki.

Moja ya mifano hai kwamba tume inaweza kutumiwa vibaya na watawala ni ule wa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wa Kenya ya mwaka 2007.

Inasemekana na ililipotiwa katika vyombo vya habari kwamba mwenyekiti huyo alikiri kwamba alilazimishwa atangaze kwamba Kibaki ndiye alikuwa mshindi.

Kwa vyovyote vile kama Afrika inataka maendeleo ya haraka ni lazima viongozi wake waheshimu uchaguzi kama kielelezo halisi cha demokrasia na watambue sasa kwamba mchezo wa kuiba uchaguzi ni hatari kwa ustawi wa demokrasia.