Mkuu wa wilaya hii Farida Mgomi na moja ya mikakati yake ni kuhakikisha kuwa shule zote wilayani humo hakuna watoto wa shule za msingi na sekondari wanaokaa chini kwa kukosa madawati ili kukukuza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi hao.
Wanafunzi wengi katika wilaya hiyo, hawafanyi vizuri kielimu miongoni mwa sababu hizo ni mazingira magumu ya kujifunzia ikiwemo kukaa chini darasani.
Mkuu huyo wa wilaya hivi karibuni alitembelea msitu uliopo Chamwino katika kijiji cha Chamwino Ikulu, ili kwenda kujionea miti inavyovunwa ili zitumike kutengenezea madawati.
Farida akiwa katika eneo hlo aliwaambia wahusika atahakikisha hadi kufikia Juni 30 mwaka huu hakuna mwanafunzi atakayekuwa anakaa chini.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa wilaya ya Chamwino ina misitu ya mbao nyingi, hivyo haoni sababu ya wanafunzi kukaa chini.Watatengeneza madawati yatakayomaliza tatizo hilo.
Uamuzi huo anasema kuwa inalenga kwenda sambamba na kauli ya Rais Dk John Magufuli na Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene kwamba ifikapo Juni 30 mwanafunzi asikae chini.
"Msitu huu utanihakikishia kwenda sambamba na agizo la Dk Magufuli kwamba ifikapo Juni 30, mwaka huu kusiwe na mwanafunzi atakayekuwa anakaa chini.
Wingi wa miti ya mbao unanipa imani kuwa hilo linawezekana.Nimekuwa kushiriki uvunaji ili kupata mbao za kutengezea madawati" alisema.
Kimsingi alisema kuwa, hafurahishwi wanafuinzi kukaa chini hali inayochangia wasielewe haraka kile anachofundisha mwalimu.
Ukosefu wa madawati pia umekuwa ni miongoni mwa sababu za utoro kwa wanafunzi hivyo kushusha kiwango cha ufaulu katika wilaya hiyo.
"Haiwekani mtoto akae chini akiwa amepinda mgongo wake halafu mtegemee alama za ziro zitaondoka.Hata kama atakuwa na akili kiasi gani, jambo hilo haliwezekani " alisema.
Wilaya ikitekeleza azma yake ya kuhakikisha kuwa kila shule inakuwa na madawati alama za ziro katika mitihani hazitaonekana.pamoja na kuondolewa kisingizio cha mtoto kukaa nyumbani kwa kisingizio cha hofu ya kuchafuka nguo zao sababu ya kukaa chini.
Mkuu huyo anasema, pamoja na uvunaji wa msitu wa Chamwino pia katika misitu mingine kama vile ya Itiso na Mvumi Mission ambazo kwa ujumla wake zitatosheleza upungufu wa madawati katika shule zote za wilaya hiyo.
Anasema “ nawaomba wasimamizi wangu kusimamia kikamilifu mpango huu ili kuepusha hujuma ya wajanja wachache wanaoweza kuhujumu mpango huu hata kukwamisha malengo yanayotarajiwa yasifikiwe ,” alisema.
Farida aliomba ushirikiano kutoka kwa wananchi ili kuhakikisha kuwa madawati yanapatikana kwa wakati.
"Ushirikiano kwa wananchi ni muhimu, ikiwemo kubeba mbao katika vituo vya kukusanyia ili kuhakikisha kuwa zinawafikia mafundi kwa wakati na kufanikisha utengenezaji wa madawati kwenye vituo vilivyoteuliwa," anasema
Anasema zoezi hilo wataanza katika vijiji vyenye mapato mazuri kama Itiso, Mvumi Mission, Manchali na Chamwino Ikulu lengo ni kuwa vijiji vya mfano ili watu wengine waige kutoka kwao.
Farida aliyetokea katika wilaya ya Masasi na kuhamishiwa Chamwino, alibadilishana na mkuu wa wilaya ya Mtwara mjini Fatuma Ally.
Anasema alipohamishiwa hapa na kufanya ziara alikutana na changamoto nyingi sana ikiwamo madawati hivyo watoto wengi wanakaa chini na wachache wanakaa katika madawati.
"Lazima nisema ukweli, jambo hili liliniumiza kichwa changu jinsi gani nitaweza kulitatua.Hata hivyo, nilijipa moyo na kuapa kupambana na sasa nimekuja na hili wazo kwamba hadi mwezi wa sita hakuna mtoto atakayekuwa anakaa chini kama agizo la Rais linavyotaka," anasema.
Farida anawaomba madiwani wa wilaya hiyo na viongozi mbalimbali kumuunga mkono katika zoezi hilo.
Kwa upande wake, Ofisa Misitu wa Wilaya hiyo, Said Msemu anasema mbao zilizovunwa hadi sasa ni 4,715 ambazo zinaweza kutengeneza madawati 1,200.
Halmashauri hiyo imejidhatiti kukabiliana na changamoto ya madawati pia kupanda miti ili kuhakikisha kuwa miti inakuwepo kwa miaka mingi ijayo.
"Ili jambo hili liweze kufanikiwa kwa asilimia mia moja tutahakikisha tunaunga mkono jitihada za mkuu wetu wa wilaya kuhakikisha kuwa madawati yanapatikana kwa kukata miti na kupanda miti ili kuendelea kutunza mazingira,’’ anasema.
Msemu anasema hadi sasa wamepanda miche 4,246 aina ya mikongoro iliyogawanywa katika shule za Wilaya hiyo.
Pia anasema, wametenga miche ya miti zaidi ya 5,000 aina ya mikongoro kwa ajili ya kufidia misitu wanayoivuna sasa.
“ Tumeamua kupanda miche hii ya mikongoro kwa sababu ukikata tawi lake na kulipanda linaota mti mwingine ambao utatuzalishia mbao kwa ajili ya kutengenezea madawati miaka ijayo,"anasema.
Msemu anasema mategemeo yao ni kupata miti ya kutosha ili kuziba pengo la miti iliyovunwa kwa ajili ya kutengenezea madawati katika awamu ya kwanza.
Naye Ofisa Elimu Ufundi na Taaluma wa Wilaya ya Chamwino Abbubakary Ibrahim, anasema kuwa kaatika wilaya yake ina shule za msingi 119 zina upungufu wa madawati 10,518.
"Mahitaji ya madawati ni 19,383. Upungufu tulionao ni madawati 10,518 na tuliyonayo ni 8,865. Tunawaomba wadau wamuunge mkono mkuu wa wilaya yetu ili tuweze kupata madawati hayo ,"anasema lbrahim.
Wabunge wa jimbo la Chilonwa na Mtera kwa upande wao wanamuunga mkono Mkuu wa Wilaya. Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde anaahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chilonwa, Joel Mwaka ameahidi kutoa fedha kwa ajili ya kutengenezea madawati ili kuhakikisha kuwa wilaya hiyo wanafunzi wanaondokana na kero ya kukaa chini.
Kwa upande wa madiwani wa Halmashauri ya Chamwino, wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Buigiri (CCM) Kenneth Yindi ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa kushirikiana na marafiki zake.
"Kwa niaba ya wenzangu nasema kuwa suala hili alilolianzisha Dc wetu Farida linatakiwa liungwe mkono na viongozi hata kwa wananchi kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa watoto wetu hawakai chini," anasema.
Baadhi ya wanafunzi wanasema kuwa, wanafurahia zoezi hilo kwa kumpongeza Rais kuwataka wakuu wote wa wilaya kuhakikisha kuwa mwisho wa kukaa kwao chini ni Juni mwaka huu.
Pendo Mathias anasema kuwa, tunaamini Juni mwaka huu katika wilaya yetu kutokana na zoezi hili kusimamiwa na mkuu wa wilaya Farida, hatutafanya vibaya katika taaluma ya elimu kwa kuwa wataondokana na kero ya kukaa chini.
Pendo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Buigiri Mission, anasema wamekuwa wakikaa chini kwa muda mrefu, hivyo kushindwa kufanya vizuri darasani.
"Shule nyingi katika wilaya yetu ni wanafunzi wachache wanaokaa kwenye madawati lakini wengi wao wanakaa chini hasa kuanzia darasa la kwanza la tano hadi la sita," anasema Pendo.
Naye Petro Mazengo wa shule ya msingi Chamwino, Chamwino Ikulu Wilayani hapo, anasema tabia ya utoro wa kuingia madarasani imekuwa ikisababisha na hofu ya kuchafuka kwa sababu ya kukaa chini.
"Nilikuwa nikifika shuleni roho ya kuifurahia shule sikuwa nayo.Nilikuwa natoka nyumbani nikiwa msafi lakini ninaporudi utafikiri nilikuwa ninagalagala chini, kisa ni ukosefu wa madawati, lakini kwa mpango huu ninaamini kila mwanafunzi atafanya vizuri kimasomo,"anasisitiza.
Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda anasema kuwa maono ya Mkuu wa wilaya yanatakiwa yaungwe mkono na wadau wote.
Kaponda anasema suala la mwafunzi kusoma katika mazingira mazuri ni la jamii nzima
.
"Nikiwa Ofisa elimu wa mkoa wa Dodoma, ninamuunga mkono kwa nguvu zote.Tunatakiwa tumpe ushirikiano ili watoto wetu wasikae chini, kwani suala la elimu ni la kila mmoja," anasema Kaponda.
Imeandikwa na Peter Mkwavila na Shekha Shaily, Chamwino.










