Jiji msipokuwa makini mtaogelea kwenye siasa miaka mitano'

15May 2016
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
Jiji msipokuwa makini mtaogelea kwenye siasa miaka mitano'

UPO mgogoro unaofukuta katika Jiji la Dar es Salaam, umeingiza siasa kwa kiasi kikubwa ndani ya mipango ya maendeleo, natabiri utatumia muda mrefu wa mabishano na kusahau mambo ya msingi ambayo Baraza la Madiwani linapaswa kutekeleza ndani ya miaka mitano.

meya wa jiji la Dar es Salaam

Kinachofanyika kwa sasa ni kufukua ‘makaburi’ ambayo mengine ni ya muda mrefu na hakuna uwezekano wa haraka ambao siyo wa gharama kwa kupata kitu ambacho kitakuwa na manufaa endelevu kwa wakazi wa Dar.

Bila kujijua baraza hilo linajiingiza kwenye mgogoro wa muda mrefu ambao ulifanyika miaka mingi ikiwa ni makosa ya kiufundi ya kuruhusu uwepo wake kisheria na sasa wanataka kurekebisha, huku, jambo lenyewe likiwa katika hatua ya mbali na ambayo wasipokuwa makini itawaingiza katika hasara ya mabilioni ya fedha ambazo zingetumika kwa maendeleo ya wananchi.

Mgogoro huo ni baina ya Jiji na Kampuni ya Simon Group Ltd ambaye aliuziwa hisa za Jiji asilimia 51 katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), huku asilimia 49 zikishikiliwa na Msajili wa Hazina kama mwanahisa mwenza.

Uongozi mpya wa jiji chini ya Meya wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Isaya Mwita, umekutana katika kikao cha kwanza cha madiwani na kutoa maazimio mbalimbali ikiwamo kutaka kurudisha hisa zake na kuzimiliki ili waendelee kusimamia usafiri jijini huku wakifananisha majiji ya Pretoria na Nairobi ambayo usafiri unasimamiwa na Halmashauri.

Hakuna ubishi kuwa jiji 'lilichemka' kwa kuingia kwenye kitanzi, kwani ni sawa na mtu aliyeona mali yake anayomiliki na mtu mwingine ameshindwa kuiendesha akauza umiliki wake wote na kumfanya kukosa nguvu yoyote ya kumuhoji wala kuchukua hatua kwa aliyenunua, sasa anatamani kuwa sehemu ya mmiliki na hawezi kufanya hivyo.

Jiji linasema limebaini madudu mengi ikiwamo uuzaji wa hisa haukufuata taratibu na limeunda kamati ya kuchunguza na wanamuomba Msajili wa Hazina kutoa hisa zake kwa mwekezaji huyo.

Wakati jiji linafanya maamuzi kama hayo tayari aliyeuziwa ameshawekeza kwa asilimia kubwa ikiwamo kulifufua shirika ambalo lilikuwa taabani na sasa serikali inapata kodi kutoka hapo, kinachofuata ni kuburuzana mahakamani baina ya Jiji na Simon Group na mwisho wa siku watajikutana wanatakiwa kulipa mabilioni ya fedha.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mvutano baina ya Simon Group na Jiji, na hadi mwanzoni mwa mwezi huu lililipwa Shilingi bilioni 5.5 baada ya amri ya mahakama kuamuru zitolewe kama manunuzi ya hisa, lakini kwa kipindi chote cha nyuma kutokana na mikataba tata limejikuta halipati hata senti.

Mikataba ya aina hiyo ni mingi katika halmshauri kwa kuwa wakati wa uingiaji wake waliweka mbele maslahi binafsi, mathalani mkataba wa Osterbay Villa na Manispaa ya Kinondoni, miaka sita manispaa haijawahi kukusanya hata senti moja katika nyumba zilizojengwa na mbia kwa makubalino maalum naye (mwekezaji) ameendelea kuzipangisha na kujizolea fedha asiyoilipia kodi kokote huku halmashauri ikipigwa marufuku kufika eneo hilo.

Kwa hili jiji litafute njia nyingine za kidiplomasia kuweza kuwa na haki na usafiri wa mabasi yaendayo haraka yanayoendeshwa na kampuni ya UDA -RT na kukiri kuwa walikosea kugawa mali ya wana Dar es Salaam pasipo kuangalia maslahi ya wengi na malengo ya muda mrefu.

Madiwani wa sasa wasipokuwa makini watajikuta wanaingizwa kwenye siasa ambazo zitapoteza muda mrefu na miaka mitano itakwisha hawatakuwa na la kuwaeleza wananchi, wasikubali hilo bali walitazame jambo lenyewe kwa undani na kupima nguvu zake kisheria kama wanaweza kujinasua au la na kuacha kuwaweka wananchi njiapanda kwa taarifa za kwenye vyombo vya habari.

Yapo mambo mengi ambayo wananchi wa Dar es Salaam wanatamani yatekelezwe na halmashauri zao, mfano miundombinu mingi ni duni na michafu , masoko yapo katika hali mbaya, huduma za jamii kama zahanati na vituo vya afya vinavyosimamiwa na halmashauri vipo taabani.

Halmashauri zijifunze kupitia makosa ikiwamo kuwatafuta kokote waliko walioingiza hasara na kusababisha wananchi wakose haki ya mali yao, badala yake kikundi cha watu binafsi kimenufaika kwa niaba ya umma.

Wananchi wanataka kusikia dampo limejengwa na uondoaji wa taka katika maeneo yao unafanyika kwa wakati, barabara za mitaa zinajengwa na kupitika muda wote , vituo vya mabasi vinajengwa kama Mbagala ambako hadi leo kuna kigugumizi cha ujenzi wa kituo cha kutosheleza mahutaji.

Kituo kikuu cha mabasi kiko taabani na sasa wametenge fedha za kukikarabati kiendelee kutumika kwa kuwa halmashauri haina Shilingi bilioni 50 za kujenga kituo hicho na kile cha Boko.

Hii inaonyesha kuwa huko nyuma mambo yaliendeshwa kwa mfumo wa chukua chako mapema hakuna kuweka mbele maslahi ya waliowapa nafasi hizo na mwisho wa sikj ikawa ni ulaji na ufisadi hivyo manispaa hasa zinazoongozwa na Ukawa zisikubali kuingia kwenye mtego huo.
Tutafakari