Mahakama hii imekuwa ikishughulika zaidi na watawala. Hii haishangazi kwa sababu wenye uwezo, nia na sababu ya kutenda makosa hayo ni watu wa tabaka hilo.
Vile vile, watu wa tabaka hilo wa Afrika wanalalamika kwamba ICC iko kwa ajili yao zaidi. Kisayansi, hili linaweza kuwa kweli kwa sababu watu wa tabaka hilo wa bara hili ndiyo wenye mambo ya ajabu ukiwalinganisha na wa mabara mengine.
Ni Afrika ndiko kiongozi anapoongoza milele, ni barani humu unapokuta mabeberu wakubwa wa dunia wanamshambulia mwenzao hata kufikia kumuondoa madarakani kwa kumuua lakini wengine hawathubutu hata kuwagunia mabeberu hao, wanaendelea na mambo yao kama hakuna linalotokea!
Afrika ndiko utakuta kiongozi anashirikiana na wezi wa ndani na nje ya nchi kuiba rasilimali ya taifa lake.Ni barani humu ambapo hukishinikizwa uchaguzi, kiongozi aliyepo madarakani analazimisha kubaki madarakani kwa njia yoyote ile. Hulazimisha ushindi kwa mipango ya uchaguzi na hata akishindwa uchaguzi hutangazwa mshindi.
Watu wa akili hizo kwa nini wasitazamiwe kufanya uhalifu dhidi ya watu wao kama uhalifu huo utawafagilia njia ya kuendelea kutawala (siyo kuongoza)?
Hivi sasa kuna mkakati mkubwa wa Waafrika wa tabaka la watawala kufikiria kujitoa ICC Wanailaani kuwa inawaonea. Inawaoneaje? Mbona si watu wa mataifa yote ya Afrika wa tabaka hilo wanaoshughulikiwa na mahakama hiyo?
Wapo wakatili pia wenye upendo wa dhati kwa watu wao. Kwa maana hiyo wanaoipigia kelele mahakama hiyo ni wale wakatili.
Jambo la kujiuliza hapa ni kwamba, kama hawa wakatili hawajafanya ukatili kwa watu wao, wanaipinga kwa nguvu mahakama hiyo. Ina maana wanapanga kuwafanyia mabaya yapi watu wao baada ya kujitoa?
Ukilitazama vizuri suala hili la Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Binadamu, utaona kuwa ni suala la pande tatu. Mahakama yenyewe ambayo ni mdhibiti wa uhalifu, watuhumiwa wa tabaka la watawala ambao ni wadhibitiwa na watu wa tabaka lisilo la watawala ambao ni walindwa.
Katika utatu huo, ni wazi Mahakama itapenda kutimiza wajibu wake kwa maslahi ya watu wasio wa tabaka la watawala, watu wasio wa tabaka la watawala watapenda kulindwa ambapo baadhi ya watu wa tabaka la watawala wataichukia mahakama hiyo kwa kuogopa kudhibitiwa.
Kuna watakaosema kwamba mahakama hiyo ikichukuliwa inawadhibiti watuhumiwa, tafsiri itakuwa kama kesi zinaamuliwa dhidi ya watuhumiwa kabla ya kusikilizwa. Hapana, kesi zitasikilizwa na haki si tu itatendeka bali pia itaonekana kutendeka.
Udhibiti unaoelezewa hapa ni hali ya mtawala kujua kwamba akifanya ukatili kwa watu wake, atashtakiwa. Kuelewa hivyo ndiyo udhibiti wenyewe bila kujali matokeo ya kesi kwa sababu mtu atajihoji kwamba mpaka kufikia kushtakiwa, maana yake alilotenda lilikuwa baya na mwisho wa kesi chochote kinaweza kutokea.
Hata hadhi kushuka kwa mtu mkubwa kusimama kizimbani kunatosha kumdhibiti dhidi ya ukatili kwa watu wake
Kwa mantiki hiyo,inaposemwa wananchi wa taifa fulani wanaipinga ICC wale wasio kwenye tabaka la watawala wanapaswa wajitoe kwenye utoaji kauli hiyo kwani kimantiki kama una akili timamu huwezi kupinga kinachokulinda.
Kwa mtazamo huo, kama uamuzi wa kujitoa kwenye mahakama hiyo unapaswa kujadiliwa bungeni, wabunge ambao ni wawakilishi wa watu wengi wasio katika tabaka la watawala wapinge kwa kauli moja kujitoa kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kuifanya nchi igeuke uwanja wa damu.
Kwa faida ya nani? Hilo linapaswa lipingwe kwa maswali mawili ya msingi.Kwanza, kama leo tuna viongozi waadilifu, wapenda wananchi na tuna mifumo mizuri ya vyombo vya kutenda haki kwa nini tuiogope mahakama hiyo isiyowalenga viongozi wa aina hiyo wa nchi zenye utaratibu huo?
Pili,kuipinga leo mkiwa na kiongozi mzuri,siku mtakapotawaliwa na mkatili, mtaufutaje chini yake uamuzi huo?
Mambo ya nchi si ya kuyaamua kwa kuangalia hali ya leo na watu wa leo. Nchi ni ya kudumu itakayopitia hali tofauti tofauti chini ya viongozi wa hulka tofauti.Inawezekana hata hao wanaoonekana wana kiwango cha kutosha cha utu, wako hivyo kwa sababu ya kuiogopa mahakama hiyo.
Hatujui bila mahakama hiyo watakuwa viongozi wa namna gani. Kwa upande mwingine, hawa wakatili wa leo wangekuwa na kiwango gani cha ukatili kama ICC isingekuwepo?
Kwa usalama wetu, tuache Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Binadamu iendelee kuwa na nguvu katika nchi zote za Afrika ili iwadhibiti viongozi wakatili.Leo ipo, hali ni hii, je isipokuwepo mambo yatakuwaje ?










