Namna ya kuchagua rangi za sofa

14May 2016
Vivian Machange
Dar es Salaam
Nipashe
Namna ya kuchagua rangi za sofa

HUENDA ukiwa sebuleni umezoea kuliita kochi au sofa. Viti vikubwa vyenye sponji unavyokalia ama ukipumzika na familia, au ukikarimu wageni lakini pia, ukitazama runinga.

Hii ni fenicha muhimu inahitaji uwe makini kuichagua hasa kwa kuangalia rangi na umbo.Muonekano mzuri wa viti hivyo sebuleni kwako ni jambo la kuzingatia ili kuwa na eneo ama chumba maridadi.

Kama zilivyo fenicha nyingine kubwa unazonunua nyumbani, sofa unategemea kuishi nalo kwa miaka mingi kama ilivyo kwa kitanda na meza ya chakula , hizi ni fenicha kubwa ambazo zinachukua gharama kubwa kuzinunua.

Huenda unahamia kwenye nyumba mpya na sasa umeanza kuweka na kupanga vitu, ni muhimu kuchagua sofa kwanza kwani ni rahisi kupamba kulizunguka. Baadhi ya wenye nyumba wanapendelea rangi ya sofa kuwa ya jamii moja na ile ya ukuta ili kuleta mfanano wa chumba.

Hili ni wazo zuri lakini inaweza kuwa changamoto pale utakapotaka kubadili rangi ya ukuta. Uamuzi mzuri ni wa kuachagua rangi ya kochi ambayo itaendana na mapambo mengine yatakayokuwepo sebuleni.

Kwanza kabisa jiulize unataka liwe la rangi nzito au nyepesi? Wengi tunasahau kuzingatia rangi ya sakafu tunapochagua rangi ya sofa. Kwa mfano unapotaka lenye rangi nzito chunguza kama litashabihiana na zulia la rangi nzito utakaloweka sakafuni? Kwa sababu kawaida sofa ni kubwa na inajaa ikiwa na rangi nzito au giza inaweza kunyonya mwanga na kukifanya chumba kuwa giza au mwanga hafifu.

Unapotaka kufahamu zaidi ili kujiridhisha na rangi ya sofa anza kwa kununua kipande cha kitambaa chochote cha bei rahisi kinachofanana na cha rangi ya sofa unayohisi itapendeza ili ukalinganishe.

Chukua kiti ukiweke eneo unapotaka kupachika sofa halafu funika kwa kitambaa hicho.

Ndipo utaona muonekano wa rangi hiyo utakuwaje. Kumbuka kizuri ni gharama, unaweza kukata vipande vichache vya vitambaa vitatu tofauti kabala ya kufanya uamuzi.Hiyo itakupa picha ya rangi itakavyoonekana hapo sebuleni, kama rangi ya sofa itakuwa nyepesi sana au nzito sana kwa sebule.

Kama unaweka makochi myeusi kwenye sakafu nyeusi, rangi hii itafubaza chumba kisionekane vyema. Endapo utaweka sofa ya rangi nzito, hakikisha sakafu au zulia lina rangi nyepesi zaidi. Meza ya kahawa yenye rangi nyepesi au ya kioo ndiyo itakayofaa kuleta mng’aro kwenye weusi na kusaidia fenicha nyingine zionekane.

Makochi ya rangi nyepesi huonyesha madoa na uchakavu kwa urahisi. Kabla ya kuchagua sofa nyeupe au rangi nyingine nyepesi, fahamu namna sebule itakavyotumika kwa hali halisi na siyo ya kufikirika. Kama mkakati wako ni kama wa baadhi wanaochukulia kuwa kochi ni kitanda cha sebuleni basi rangi za nyepesi hazikufai.

Lakini ingawa sofa zako zitatumiwa na watoto, kulalia na kucheza, nunua vitambaa unavyoweza kuvisafisha kwa kufuta. Au pia sofa za kuvalisha kava au foronya za kuondoa na kufua hili litakuwa muafaka kwako.

Ukishaamua kuwa unataka sofa ya rangi nzito au nyepesi unakuwa ni wakati wa kufikiria rangi halisi.

Baadhi ya watengenezaji, watumiaji na wauzaji wa sofa nilioongea nao wanasema makochi ya za rangi zisizoegemea upande wowote au ‘nyutro’ ndiyo chaguo la wengi. Makochi haya ni rahisi kupamba chumba na zinaonekana kutokupitwa na wakati hata baada ya miaka kadhaa.

Sofa za rangi zisizoegemea upande wowote ni pamoja na rangi za krimu, kijivu na ugoro. Fenicha hizi zinaweza kuendana na mapambo yoyote na bado zikawa na mvuto wa kisasa.

Usisahau rangi za mito na mitandio utakayotupia kwenye sofa zako mpya.

Mawasiliano: www.vivimachange.blogspot.com Simu 0755