Waziri Mwakyembe alete majibu ukatili wa kingono…

14May 2016
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
Waziri Mwakyembe alete majibu ukatili wa kingono…

KILA siku kuna habari mbaya za ukatili wa kijinsia kama ilivyosikika kutoka bungeni, wiki iliyopita Waziri wa Sheria na Katiba , Dk Harrison Mwakyembe, akiwaambia wabunge kuwa, matukio 19 ya wanawake na watoto kubakwa au kulawitiwa yanaripotiwa polisi kila siku.

Waziri wa Sheria na Katiba , Dk Harrison Mwakyembe.

Tena kuna mengine mamilioni hayafikishwi polisi kwa hiyo hali inatisha kwa vile ukweli halisi wa ukatili haufahamiki.

Sasa hakuna ubishi Tanzania inaelekea kuwa eneo hatarishi kwa maisha ya wanawake na watoto kwa vile, vitendo vya kubakwa, kulawitiwa pamoja na watoto kunajisiwa vinaongezeka kwa kasi ya kutisha.

Takwimu hizi zinazotolewa bungeni si suala la kupuuzwa, wanaharakati na wanawake wanatakiwa kuitaka serikali kuja na majibu ya ukatili wa jinsia, iache siasa na longolongo kwani wanawake wazee kwa vijana pamoja na watoto wanaumia na kuhatarishiwa maisha.

Hiki ni kitisho kingine cha karne , kwa vile ni visa 19 pekee ndivyo vinavyofahamika. Idadi ni kubwa mara kadhaa zaidi na haifahamiki kwani unyanyasaji mwingi kingono hauripotiwa na kesi nyingi humalizwa kidugu nyumbani bila wabakaji kuadhibiwa.

Kwa hiyo ukatili wa kijinsia sasa siyo suala la kushangaza ni kitisho na wanawake wanaendelea kuteseka na vipigo, kuwafukuzwa na kuwapora mali, wanawake wazee kubakwa na kulawitiwa kisha kuchinjwa huko kanda ya ziwa, mabinti kulazimishwa ndoa na mimba za utotoni, wengine wa kiume kulawitiwa na kunajisi tena na ndugu.

Waziri anasema hana cha kusema wala ufumbuzi na kwamba dawa ni kubadilisha sheria ya makosa ya kujamiina (SOSPA) ili kuongeza makali zaidi na kuwaadhibu wahusika. Kwa kifupi aache siasa aje na majibu na halo likomeshwe.

Haifahamika sheria hiyo itarekebishwa lini, lakini watu wanaifahamu? Kampeni za kuitangaza zimefanyika kwa kaisi gani? Ni wakati wa wanawake na watoto kukaa mkao wa kukabiliana na unyanyasaji huu wa kutisha.

KIINI

Tatizo la kudhalilishwa linakua na kukomaa kwa sababu za mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii lakini linalelewa na ukimya wa waathirika ambao ni wanawake. Wabakaji wanastarehe na kudumu kwa vile mwanamke akibakwa ananyamaza akihofia kuwa ataaibika, atakosa mchumba, ataachwa kama ana mume na pia atanyanyapaliwa na jamii.

Hali hii imelea wabakaji ndani ya familia, ujirani , sehemu za kazi, kwenye nyumba za ibada na shuleni kote mijini na vijijini, kisa watu wanaogopa kusema.

Waathirika wanafanya siri.Hilo limelea na kukuza tatizo kwa hiyo, sasa ni wakati wa kukataa kunyamazia ubakaji na unyanyasaji kingono.

Waathirika wazungumze hadharani bila kuficha siri eti ukieleza kuwa umebakwa na mjomba ama baba wa kukulea unaiabisha familia na utasababisha ndugu kusambaratika si kweli. Ni wakati wa kuchukua hatua wanaobakwa wawe wanawake kwa watoto wazungumze hadharani ili watuhumiwa wafahamike na waadhibiwe.

Ni wakati wa kuona kuwa kubaka mwanamke au kunajisi mtoto hakuna tofauti na kuibiwa simu ni lazima uripoti, uelezee aina yake, mahali ilipochukuliwa na unayemhisi. Kadhalika ukifanyiwa ukatili wa ngono ripoti, mtaje mhusika hatua zichukuliwe. Huo utakuwa mwanzo wa kupambana na uhalifu huu.

Wazazi wanawanyanyasa watoto kingono, kadhalika walimu shuleni na wa dini nao wamo, si hivyo tu ofisini rushwa ya ngono na unyanyasaji wa aina hiyo unakithiri.

ATHARI

Ubakaji na aina zote za unyanyasaji kingono au kijinsia si suala la kupuuzwa kwa vile lina athari kubwa kwa wanawake. Ni chanzo cha maambukizi ya maradhi ya kujamiiana mfano VVU, kisonono na homa ya ini (hepatitis B).

Pia ni mwanzo wa mimba zisizotakiwa , utoaji mimba unaosababisha vifo vya wanawake na watoto wachanga. Pia huongeza idadi ya watu bila mipangilio na wengine huwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Hiki ni chanzo cha mimba za utotoni ambazo pia husababisha vifo vya wazazi wadogo na watoto wao. Unaleta pia fistula na ulemavu kwa wazazi hawa wadogo.

Unyanyasaji huu unaathari kisaikolojia, unaleta shinikizo la damu, unyonge na kuchangia kuongeza umaskini kwenye jamii, hivyo ni lazima kuanzisha mikakati ya kukabiliana nao.

KAMPENI

Bunge na wadau wa harakati za kijinsia kama Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa), Mtandao wa Jinsia (TGP) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),wasiipuuze taarifa Waziri Mwakyembe bungeni.

Wahamasishe kuanza kampeni za kuhimiza wanawake na watoto kujitokeza wanapobakwa na kuwataja watuhumiwa hata kama ni wazazi ama kaka zao na kuhimzwa waache aibu na kuumia mioyoni.

Wanaume wengine wanatumia ngono kama silaha ya kuwakomesha na kuwakandamiza wanawake. Wanafahamu kuwa kinamama wakibakwa ama watoto wao watanyamaza na kuficha siri na huo kwa mbakaji ni ushindi ‘amemkomesha’. Habari hizo sasa ziishe.

Wanawake wamekaa kimya kwa miaka mingi na hicho kimekuwa chanzo cha ukatili huo kuwa sugu kwenye jamii na watu wemeathirika kimaisha kutokana na kufanyiwa ukatili huo.

Kuna ubakaji wa kuchangia unaofanywa na genge la wabakaji. Watu hawa wamekuwa wakiwanywesha pombe wanawake na kuwabaka, pia wananajisi watoto wavulana kwa wasichana. Hawaishii hapo wanabaka na kuwaua wazee. Yote haya yamedumu kwa sababu hakuna anayewasema wala kuwaripoti. Kampeni ya kufunguka na kupinga ubakaji imalize jeuri ya magenge ya wauaji kama hawa.

Ili kufanikisha mkakati wa kuripoti ubakaji serikali isaidie kuwafunza maofisa Ustawi wa Jamii na kuwafikisha vijijini na ofisi za kata mijini. Kwa kuanza wawepo katika kila kata. Kiasi fedha zinavyopatikana wafikishwe vijijini ili wanawake na makundi ya wanyonge yatoe taarifa za unyanyasaji, uwe wa ngono, mali, ndoa na mimba za utotoni.

Hatua hiyo itawezesha kuwadhibiti wabakaji mitaani na kupunguza mazoea ya kumaliza kesi hizo kindugu majumbani.

Kama serikali inaweza kuajiri ofisa ugani kwa kila kijiji ni dhahiri inaweza kuwa na maofisa hao kwa kila kijiji pia.

Lakini katika jitihada za kupunguza gharama inaweza kuwafunza walimu vijijini na mijini wakafanya kazi ya maofisa ustawi ili kupokea taarifa za ubakaji na kufuatilia wahusika ili washitakiwe na waathirika ili kupata ushahidi na haki.

Mwishoni mwa mwaka jana Tamwa, ilifanya utafiti katika mikoa 15 ya Bara na Visiwani kuangalia hali ya ukatili wa kijinsia nchini kwa kuchunguza ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni, vipigo, kutelekeza familia na ubakaji.

Ilibaini kuwa tatizo limeshamiri na kuongezeka Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kufanya utafiti huo. Licha ya kuchapisha ripoti na kutoa taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari , serikali haijajitutumua na kuchukua hatua kupinga unyanyasaji huo wa kijinsia.

Bunge liishinikize serikali iache siasa na ifanyie kazi ripoti na taarifa zinazotolewa kuhusu unyanyasaji kijinsia na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kutenga fedha za kutosha na kupambana na uhalifu huo unaoathiri maisha ya mamilioni ya wanawake na watoto nchini.

Kadhalika iwajibike kikamilifu kuwalinda wanawake na watoto ambao kwa miongo mingi wanateseka na ukatili, unaoleta vifo, ulemavu, umaskini na hisia za unyonge kwa kuzingatia kuwa wanawake, ambao ni zaidia ya asilimia 51 ya Watanzania wote ndiyo waathirika.