Taarifa hizo zilithibitishwa juzi na Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipokuwa akizindua Chama cha Wabunge cha Kupambana na Rushwa (APNAC), na kusema amepata ujumbe kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwamba wana nia ya kupeleka muswada huo bungeni.
Tunaelewa kuwa serikali ina nia nzuri ya kutunga sheria hiyo, lengo likiwa ni kuwafanya viongozi wa umma kuzingatia na kufuata maadili ya uongozi.
Ni jambo lililo wazi kwamba bila kutenganisha mambo hayo mawili, viongozi wengi wa umma wamekuwa wakijikuta wakiingiza maslahi ya biashara zao katika uongozi wa kisiasa, hivyo, kukiuka maadili ya uongozi ikiwamo kupata kashfa za ufisadi.
Miaka ya nyuma wakati wa utekelezaji wa itikadi ya Ujamaa kupitia Azimio la Arusha, sheria ziliwabana sana viongozi wa umma kiasi kwamba walishindwa kufanya shughuli za kujiongezea kipato.
Kwa mfano, hawakuruhusiwa kumiliki nyumba za kupanga, kuwa na hisa katika makampuni na fursa nyingine za kujipatia kipato.
Pamoja na viongozi wa umma kuishi maisha ya kutegemea mshahara pekee, lakini utendaji kazi zao ulitawaliwa na uadilifu, uaminifu, kuheshimu na kufuata maadili ya uongozi.
Hata hivyo, baada kulegezwa masharti ya uongozi wa umma na kuwaruhusu viongozi wa umma kufanya shughuli za kuwaongezea kipato, fursa hiyo ilanza kutumika vibaya kutokana na viongozi wengi kutozingatia maadili na miiko ya uongozi.
Kuna matukio mengi ya kashfa za ufisadi ambazo zimewakumba viongozi wengi wa umma nchini. Kashfa zote hizi zinaendelea kuwakumba viongozi wengi wa umma kila uchao na sababu kubwa ni kutotenganishwa kwa siasa na biashara.
Makundi kadhaa nchini yamekuwa yakipendekeza kutungwa kwa sheria hiyo ili kudhibiti mmomonyoko wa maadili miongozi mwa viongozi wa umma, lakini serikali imekuwa ikiahidi kulifanyia kazi suala hilo bila utekelezaji.
Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, alipoingia madarakani aliahidi kuwa serikali ingeandaa muswada huo. Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilipokutana katika Kijiji cha Butiama, mkoani Mara mwaka 2008, moja ya ajenda zake ilikuwa ni kutenganisha siasa na biashara.
Baada ya kikao hicho, miongoni mwa maazimio yaliyotolewa lilikuwamo la kuweka utaratibu wa kuandaa sheria ya kutenganisha siasa na biashara.
Kwa sababu zisizojulikana, ahadi hiyo iliishia hapo bila utekelezaji hadi leo. Tunafahamu kuwa kuna wanaonufaika kutokana na kutotenganishwa kwa nafasi hizo na watapinga kwa nguvu zao zote ili sheria hiyo isitungwe.
Sisi tunaunga mkono kuwapo kwa sheria hiyo na sasa ndio wakati mwafaka kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuelekeza jitihada zake katika kupambana na ifisadi pamoja na kurejesha maadili katika uongozi na utumishi wa umma.
Tunawashauri viongozi wa umma wakiwamo wabunge kuunga mkono uwapo wa sheria hiyo kwa kuwa lengo lake ni zuri, hivyo wasiwe na hofu.
Sheria hiyo inatumika katika nchi kadhaa ambako mfanyabiashara anapoingia katika uongozi wa kisiasa anakabidhi biashara halafu na akimaliza siasa anarudi katika biashara zake. Sheria hiyo inaweza kutungwa na kutekelezeka nchini iwapo tu kutakuwapo na utashi wa kisiasa.










