Sababu za TFF kuipokonya Azam FC pointi tatu imedaiwa ni kumtumia beki Erasto Edward Nyoni katika mechi hiyo namba 156 ya Ligi Kuu akiwa ana kadi tatu za njano.
TFF imesema kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 37(4) ya Ligi Kuu Toleo la 2015 inayoelekeza kuwa mchezaji atakayeonywa kwa kadi ya njano katika michezo mitatu hataruhusiwa kucheza mchezo unaofuata wa timu yake, hivyo Azam ilikiuka Kanuni husika.
Kwa kuzingatia Kanuni ya 14(37) ya Ligi Kuu Toleo la 2015, TFF imeipa timu ya Mbeya City ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.
Pamoja na hayo, katika taarifa yake juu ya maamuzi hayo, TFF pia imelionya Benchi la Ufundi la Azam kuongeza umakini katika utunzaji wa kumbukumbu za kadi za wachezaji wake.Na TFFpia imezikaribisha timu zote wakati wowote kuomba kumbukumbu zozote kila wanapozihitaji.
Lete Raha hatuna shaka na adhabu waliyopewa Azam FC kwa kukiuka kanuni za Ligi ambazo zimeanishwa wazi tu na zinaeleweka.
Lakini tatizo letu ni kwamba, Azam FC walifanya kosa Febauri 20 na maamuzi yamekuja kutolewa Mei mwanzoni – je hapa katikati kipindi chote kwa nini suala hilo halikutolewa uamuzi.
Haya ni makosa ambayo yanaweza kuzalisha dhana nyingine tofauti katika wakati huu, ambao Ligi Kuu inaelekea ukingoni na timu zinawania ubingwa, na nyingine zinataka kuepuka kushuka daraja
.
Wazi maamuzi ya aina yanakuwa na faida kwa baadhi ya timu katika ligi hiyo, ikiwemo Mbeya City yenyewe – lakini pia yanaziumiza timu nyingine, ikiwemo Azam yenyewe ambayo kwa kipindi chote tangu Februari imeendelea kujihesabia pointi zake zikiwemo hizo ilizovuna Mbeya kwa jasho.
Ipo haja ya TFF kuziagiza Kamati yake ya Mashindano pamoja na Bodi ya Ligi kuwa na utaratibu wa kupitia taarifa za michezo kila wiki, ili kutoa maamuzi ya mapema, kuliko ilivyojitokeza katika suala la Azam FC na Mbeya City.
Na Lete Raha tunasema hivyo kwa sababu tunaona kabisa kuweka viporo kiasi hiki juu ya adhabu kama hizi ni hatari kwa afya ya Ligi Kuu.










