Yanga isibweteke kwa ushindi, ijiandae mechi ya marudiano

09May 2016
Mhariri
Nipashe
Yanga isibweteke kwa ushindi, ijiandae mechi ya marudiano

KWANZA tungependa kuwapongeza wawakilishi wa nchi katika mashindanio ya Kombe la Shirikisho, Yanga kwa kupiga hatua moja kuelekea kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Ushindi walioupata wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Sagrada Esperanca kutoka Angola ni hatua muhimu ya kwenda kuandika rekodi katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho ambayo ni ya pili kwa ukubwa baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa.

Ushindi huo mzuri wa Yanga, siyo kwamba umekuja kwa sababu walikuwa wakicheza dhidi ya timu dhaifu, la hasha, ni ushindi uliotokana na dhamira ya kujituma kutoka kwa wachezaji.

Ikumbukwe kwamba, Angola ni moja ya nchi ambazo zimekuwa zikifanya vizuri kwenye michuano mbalimbali kutoka ngazi ya klabu hadi taifa.

Nchi hii pia imewahi kuiwakilisha Afrika katika mashindano ya Kombe la Dunia.Hivyo basi, tunaamini hata timu zinazotoka nchini humo zina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kwenye mashindano wanayoshiriki.

Sisi kama wanamichezo , tungependa kuchukua nafasi hii kuipongeza Yanga kwa mwanzo mzuri wa kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo.Ushindi wao unawapa nafasi rahisi ya kusonga mbele kwenye mechi ya marudiano wiki mbili zijazo.

Hata hivyo, tunachukua pia nafasi hii kuishauri Yanga kuwa bado haijapita hatua ya mtoano ili kwenda kucheza makundi.
Ushindi walioupata nyumbani uwe chachu na kiini cha kujituma zaidi kwenye mechi ya marudiano huko ugenini mjini Luanda.

Haitakuwa na maana na haitawasaidia kama watakwenda Angola kucheza mechi ya marudiano wakiamini kuwa tayari wameshafuzu makundi kwa sababu tu ushindi walioupata nyumbani.

Katika mashindano makubwa kama hayo, hakuna timu dhaifu. Hatua hiyo inaonyesha kuwa kila timu imejipanga vizuri kwa ajili ya kushinda.

Wawakilishi wetu Yanga wanapaswa kuelewa hilo, kwani hata wapinzani wao wanakwenda kujiandaa vizuri kuutumia uwanja wa nyumbani kupata ushindi.

Tunachoamini katika soka ni kwamba, hakuna lisilowekezaka. Yanga wanaweza kusonga mbele, lakini pia wanaweza kuondolewa kwenye mashindano pamoja na ushindi wa mzuri walioupata nyumbani.

Yanga iepuke hadithi ya timu ya Wolfsburg ya Ujerumani iliyoshinda nyumbani 2-0 dhidi ya Real Madrid katika mechi ya mechi ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya, kisha kujiamini wanaweza kuitoa timu hiyo ya Hispania kwa sababu tu walishinda mchezo wa kwanza. Hata hivyo waliishia kufungwa 3-0 na kuondolewa kwenye mashindano.

Wanachopaswa kufanya Yanga kwa sasa ni kujiandaa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo ya marudiano ili siyo tu iende kutafuta sare, bali kushinda ugenini.

Wanamichezo tunaamini kuwa, timu inayojiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano, ndiyo inayokuwa karibu zaidi na mafanikio kuliko kinyume chake. Yanga wana nafasi ya kusonga mbele, lakini tu kama watajipanga vizuri kushinda mechi ya marudiano na siyo kwenda kuchezwa kwa lengo la kutafuta sare.