Hatua ya Serikali ya kudhibiti uingizwaji wa sukari nchini ilikuwa na nia njema ya kulinda viwanda vya sukari nchini, kwani ukosefu wa soko kwa sukari inayozalishwa ndani ulianza kuathiri viwanda hivyo na pia kuwakosesha mapato wakulima wa miwa nchini.
Juzi, Rais John Magufuli alitangaza kuchukua hatua kali kwa wafanyabiashara wote walioficha sukari kwa kutaifisha tani zote za sukari zitakazokamatwa na kuigawa kwa wananchi bure.
Aidha, Rais alitahadharisha kuwa wafanyabiashara wanaoagiza sukari toka nje na kuuzwa kwa bei rahisi, sukari hiyo inakuwa imeisha muda wake wa matumizi, jambo ambalo alisema ni hatari kwa afya za watumiaji wake hapa nchini.
Nipashe tunaamini kuwa kuna njama zinazofanywa na wafanyabiashara wa bidhaa hiyo nchini, za kuficha sukari, na kwamba zina lengo la kutaka kujitajirisha kwa haraka na kusababisha wananchi waanze kuitupia lawama Serikali pia.
Tunaamini hivyo kwa sababu wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia Bunge la Bajeti mwezi uliopita, alisema mahitaji halisi ya sukari nchini ni tani 420,000 kwa mwaka, wakati uwezo wa viwanda ni kuzalisha tani 320.000 kwa mwaka.
Ni wazi kuna nakisi ya tani 100,000. Lakini Majaliwa alibainisha kuwa sukari iliyokuwapo nchini mwezi uliopita ilikuwa ikifikia tani 37,000.
Hivyo tunalaani mbinu za aina hiyo kwani kimsingi zinamwumiza mwananchi wa kipato cha chini ambaye si rahisi kumudu bei ya sukari iliyopanda ghafla kutoka bei elekezi ya Sh. 1800 na kufikia Sh. 2500 hadi Sh. 3000 kwa kilo moja sasa.
Tunaunga mkono hatua aliyoitangaza Rais Magufuli ya kutaifisha sukari itakayokamatwa mafichoni na kuigawa bure kwa wananchi, Nipashe, kwa sababu hatua hiyo itakuwa fundisho kubwa kwa wafanyabiashara wenye uchu wa kujipatia utajiri kwa njia za mkato.
Uhaba huu, ambao tunaona Nipashe kuwa umetengenezwa na wafanyabishara wajanja, umesababisha wananchi wengi maeneo ya Dodoma na miji mingine kukaaa kwenye misururu mirefu wakisubiri kuuziwa sukari, hivyo wananchi kupoteza muda mwingi wa kufanya shughuli zao za uzalishaji kwa kufuatilia bidhaa hiyo.
Tuitake Serikali, basi, kujaribu kuharakisha mchakato wa kuagiza sukari toka nje uliotangazwa na Waziri Mkuu mwezi uliopita, ili kuziba pengo la upungufu uliopo nchini.
Kufika haraka kwa sukari hiyo, tunaona Nipashe, kutaua ndege wawili kwa jiwe moja kwani kwa sababu itauzwa kwa bei halali ya Serikali ya Sh. 1,800 kwa kilo, kwanza itafanya wafanyabiashara walioficha sukari kutokuwa na sababu ya kuendelea kuihodhi lakini pia kufurika kwa sukari kwenye soko.










