Lakini pia kwenye kilele cha msimamo, hesabu za nani atakuwa bingwa msimu huu zimeshajulikana.
Safari ya ligi hadi kufikia hatua iliyopo sasa msimu huu, imepita kwenye changamoto nyingi katika kila eneo.
Kwa mfano, changamoto kubwa kwenye ligi msimu huu ilikuwa malalamiko dhidi ya waamuzi. Ingawa malalamiko dhidi ya waamuzi yamekuwapo karibu kila msimu, lakini hakuna ubingwa kwamba, msimu huu hali ilikuwa mbaya zaidi.
Hata hivyo, tukiachana na malalamiko hayo na changamoto zingine, kuna suala la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipokonya pointi timu ya Azam FC kwa kosa la kumchezesha mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano.
Azam imeadhibiwa baada ya kumchezesha Erasto Nyoni kwenye mechi dhidi ya Mbeya City Februari mwaka huu na kushinda mabao 2-1.
Uamuzi huu pamoja na kwamba uko sahihi kwa mujibu wa kanuni na taratibu za mashindano, lakini ni wazi umewashtua wadau wengi wa michezo.
Ni uamuzi unaoacha maswali mengi kuliko majibu, lakini pia ukiiathiri timu ambayo ilikuwa kwenye mbio za kusaka ubingwa.
Kama wadau na wapenzi wa soka, ingekuaje kama uamuzi huo ungefanyika wakati timu imeshatawazwa kuwa mabingwa?
Kama Azam ingefanya vizuri na kushinda mechi zake na kujikuta ikitwaa ubingwa kabla ya ligi kumalizika, halafu TFF inaipokonya pointi zake nini kingetokea?
Majibu yanaweza kuwa rahisi kwa sababu mamlaka ya usimamizi wa soka zingeamua hivyo kwa kigezo cha kusimama kwenye mstari wa sheria, kanuni na taratibu za mashindano.
Ukweli ni kwamba, uamuzi huu unatupa funzo na umuhimu wa timu zetu kuwa na utaratibu mzuri wa kutunza kumbukumbu.
Hatuwezi kuilaumu TFF kwa kuchelewa kutoa uamuzi, lakini ni wazi kuwa lawama za kwanza lazima ziende benchi la ufundi la Azam.
Tulitarajia timu kubwa kama Azam FC inayojiendesha kisasa isingekuwa mfano wa haya waliyokutana nayo.
Kama wanamichezo, tunaamini kuwa soka la miaka ya sasa linapaswa kuendeshwa kisasa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake.
Lakini tunashangazwa na jinsi klabu zetu zinavyoendeshwa kizembe na kushindwa kutunza kumbukumbu nyingi muhimu.
Viongozi wetu wamekuwa sehemu ya matatizo mengi kwenye klabu. Kutowajibika kwako kikamilifu kumewafanya hata wachezaji wao kukosa nidhamu uwanjani na hata nje ya uwanja.
Mchezaji mzoefu kama Nyoni alipaswa yeye mwenyewe kutunza kumbukumbu zake ili kuusaidia uongozi wake.
Lakini kwa vile tuna aina ya viongozi wanaojali zaidi kupiga kelele kwenye vyombo vya habari kuliko kufuatilia mambo muhimu ya klabu, ndiko leo kunaoiponza Azam.
Dhamira yetu siyo kuishawishi Azam kuchukua adhabu kwa wahusika kutokana na kosa hilo, lakini tunajaribu kuliwaka wazi suala la viongozi wetu kujisahau wakati wa kutimiza majukumu yao.
Kama wanamichezo, tungependa kuzishauri klabu kuwa na utamaduni wa kutunza kumbukumbu mbalimbali za mashindano mbalimbali.
Lakini pia klabu ziandae semina elekezi kwa wachezaji wao ili kujua umuhimu wa kutunza kumbukumbu za matukio mbalimbali yanayowahusu.
Ni wazungumzaji wakubwa kwenye vyombo vya habari, wakijisifu kishabiki, mbwembwe na kila aina ya majigambo.
Lakini linapokuja suala la kuwajibika kikamilifu, hapo ndipo linapokuwa tatizo kubwa. Wanajisahau na kuziingiza klabu zao kwenye migogoro na matatizo.
Viongozi waepuke kuendesha klabu kwa mazoea, badala yake wajenge mfumo mzuri wa mawasiliano utakaowawezesha kutunza kumbukumbu.
Bila kufanya hivyo, tunaamini haya yaliyoikuta Azam yatatokea hata kwa klabu nyingine.










