Wakizungumza na Nipashe juzi katika eneo la majengo mjini hapa, wakiwa kwenye foleni katika duka moja la jumla la bidhaa hiyo, wafanyabiashara hao walisema wanapoteza muda mwingi kuitafuta.
Mmoja wa Wafanyabiashara hao, Simon Mwalimu kutoka Kijiji cha Chalinze Nyama, Wilaya ya Chamwino mkoani hapa alisema amefika Dodoma mjini kwa wiki mbili mfululizo kutafuta sukari bila mafanikio.
“Unaponiona hapa nimepanga foleni tangu saa 12 ya asubuhi kusubiri kuuziwa sukari katika duka hili maana hakuna sukari katika maduka mengine yote yanayouza bidhaa hii kwa bie ya jumla," alisema Mwalimu.
"Lakini nasikitika mpaka majira haya ya saa tano nimeambiwa sukari imeisha. Sasa sijui nitasubiri hadi lini?”
Mwalimu alisema siku za nyuma walikuwa wanauziwa sukari mfuko wa kg 20 kwa bei ya Sh. 40,000 kwenye maduka ya jumla.
Lakini sasa, alisema, bei hiyo imepanda kufikia Sh. 65,000 kwa mfuko wa uzito huo na bado bidhaa hiyo imekuwa haipatikani .
Mfanyabiashara Vicent Benard wa kijiji cha Ibihwa Wilaya ya Bahi alisema ametafuta sukari maduka yote yanayouza ya jumla haipatikani, na kusikitika kupoteza nauli na muda bila kupata bidhaa hiyo.
Naye Abdalah Pindi, mkazi wa Majengo mjini hapa alisema sukari imekuwa ikipanda bei kila siku tangu wiki mbili zilizopita, na sasa inmauzwa kati ya Sh. 3,500 mpaka 4,000 kwa kilo kwenye maduka ya rejareja.
Alisema tatizo hilo la sukari limesababisha baadhi ya kaya kuacha kunywa chai kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumudu bei hiyo.
Pamekuwa na uhaba mkubwa wa sukari wa ghafla nchini kiasi cha kuonekana kwa misururu mirefu ya wafanyabiashara wa rejareja wa bidhaa hiyo mjini Dodoma, na Kagera kupitisha uamuzi wa kuuza sukari katika madula maalumu tu.
Akizungumza na wananchi wa Katesh, Mkoani Manyara alipokuwa safarini kuelekea mkoani Arusha kwa barabara akitokea Dodoma juzi, Rais John Magufuli alitangaza kutaifisha tani zote za sukari zitakazokamatwa zikiwa zimefichwa na wafanyabishara kwenye maghala na kisha kuzigawa kwa wananchi bure.
“Tayari nimeshaagiza vyombo vya dola viwafuatilie wale wote walioficha sukari, hawa ni waujumu uchumi," alisema Rais Magufuli huku akishangiliwa na wananchi hao.
Akilihutubia Bunge la Bajeti April Mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema serikali imeagiza sukari kutoka nje kufidia uhaba uliopo.
alisema nchi inahitaji tani 420,000 za sukari kwa mwaka na kwamba uwezo wa viwanda vya ndani umekuwa ni tani 320,000 na hivyo kufanya kuwepo kwa nakisi ya tani 100,000.










