Samia akiri uwapo wapinzani makini

08May 2016
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe Jumapili
Samia akiri uwapo wapinzani makini

MAKAMU wa Rais, Samia Hassan Suluhu amekiri kuwa baadhi ya vyama vya upinzani vina watu makini hivyo Chama cha Mapinduzi kijipange kikamilifu kupambana nao.

makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu.

Alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma wakati akifungua Baraza la Wanawake wa Jumuiya hiyo (UWT), ambalo moja ya ajenda zake ni kufanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Alisema tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi zaidi ya miaka 20 iliyopita, vyama hivyo vimejijenga kupitia CCM na vimezalisha watu makini.

Alisema jumuiya hiyo inatakiwa kujijenga kuanzia chini ili kuwe na vijana wengi na kuwajengea uwezo ili wawe viongozi wa baadae ambao watapigania Chama hicho.

"Wapinzani wetu wanakua kuanzia chini, wanawafuata vijana kwa ahadi za ajabu lakini wanawaelewa ndiyo maana unaona wanawekeza sana kwa vijana," alisema Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke huyo na kutaka "sasa UWT ijipange kujimarisha kuanzia chini, tuongeze pia wanachama wa jumuiya.

" Samia alisema UWT inatakiwa itafakari imejipanga vipi kuzalisha watu makini kama ilivyo kwa vyama vya upinzani ambavyo vimejijenga kupitia CCM.

"Inabidi tuendane na mabadiliko maana siasa zimebadilika UWT wanatakiwa waangalie wanajielekeza vipi katika mwelekeo wa sasa."

Aliitaka UWT kuhakikisha wabunge na wawakilishi wanawake wanapewa mafunzo maalum ili waweze kuwasemea wanawake na wananchi badala ya kutoa vijembe bungeni.

Aidha, Makamu wa Rais alisema jumuiya hiyo inapaswa kupunguza kuomba fedha na ihakikishe inaimarisha mali ilizonazo kwa kuwa mali nyingi zimelala badala ya kutumika kama vitega uchumi.

Alisema atahakikisha wanawake wanachota maji umbali usiozidi mita 400 kwa kuwa wakati wa kampeni aliahidi kuwatua wanawake ndoo kichwani.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sophia Simba alisema UWT inaunga mkono hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya wala rushwa na wanaotumia vibaya madaraka.

Aidha, Simba alimuomba Samia asiwasahau wanawake kwenye nafasi za ukuu wa wilaya kwa kuwa kuna wanawake wengi wenye uwezo na kwamba baadhi yao wamewahi kuwa viongozi ngazi mbalimbali.

Simba alikuwa Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto katika serikali ya awamu ya nne.