Nyumba inayopendeza kwa ujumla kunahusisha mkusanyiko wa rangi na vitu mbalimbali vilivyomo ndani yake.
Miongoni mwa hayo yanayoongeza mvuto yamo mapambo matano madogo lakini yataleta mguso wa kipekee ndani ya nyumba yako.
VESI ZA MAUA
Ingawa zinajulikana zaidi kama vesi za maua zinapendezesha nyumba kwa njia mbalimbali. Hata ikiwa yenyewe bila chochote ikiwekwa kwenye shelfu au juu ya meza tayari ni pambo.
Vesi inaweza kutumika kwa njia mbalimbali kuendana na mahali ilipo, kwanza kwa kutunza vitu vingine vidogo mathalani, kalamu, rula na ‘maka peni’ endapo ni ofisini au nyumbani unaweza kuongeza mikasi midogo pia.
Vile vile vesi kwenye meza ya chakula inaweza kuhifadhia vitu vidogo kama vile ‘kosta’ wakati kwenye meza ya kahawa inaweza kubeba rimoti za luninga, chaja za simu, funguo na kadhalika. Kuna vesi zinazowekea mawe ya urembo na pia zipo za maua halisi na hata yale ya viwandani.
MIMEA YA NDANI
Hii pia inaweza kuoteshwa kwenye vesi. Siku za karibuni kumekuwa na mimea mingi ambayo haina usumbufu wa kuoteshwa ndani ya nyumba kwani si mikubwa sana na haihitaji maji mara kwa mara.
Vesi zenye rangi na maumbo ya kuvutia, nyingine zikifafana na kikombe kikubwa na kisosi chake zimekuwa zikitumika kuoteshea mimea midogo yenye majani manene yaliyotuna inayojulikana kama succulents.
Mimea hii imekuwa ikileta mvuto wa kipekee ndani ya nyumba iwe imewekwa juu ya meza, sakafuni au kwenye stendi za maua. Pia mimea hai ndani ya nyumba, kitaalam imekuwa ina faida ya kusafisha hewa ya ndani kwa kunyonya ile chafu na kuachilia iliyosafishwa.
MISHUMAA
Mishumaa ina historia kutoka enzi za Dola ya Roma inayotumika zama hizi inakuja kwa rangi na manukato yenye harufu mbalimbali.Bila shaka ni pambo dogo unalopaswa kuwa nalo ndani ya nyumba.Pia mishumaa inatumika kuleta mwanga wa kimahaba wakati wa mapumziko nyumbani.
VIOO
Kioo ni pambo jingine dogo ambalo zaidi ya kuleta mvuto kinaweza kikaongeza mwanga na pia hisia za ukubwa wa chumba hasa kinapokuwa kimewekwa kimkakati. Vioo vinaendana na mapambo mengi ya ndani na ni kitu cha lazima bafuni na chumbani unapolala.
SANAA
Sanaa ni njia mojawapo sahihi ya kuchangamsha ukuta. Zipo za ina mbalimbali na unaweza kupata inayoendana na mandhari ya nyumba yako. Ukuta mtupu ukining’inizwa mchoro wa karatasi gumu kama turubai unabadilisha muonekano wa awali na kuleta vivutio vipya.
Pia picha za familia zilizowekwa kwenye fremu zilizosanifiwa vizuri zinatoa utambulisho na kuonyesha historia ya familia hiyo. Na uzuri wa ziada wa kazi za sanaa anaweza kutengeneza mchoro wa sura yako au familia yote endapo utataka akufanyie hivyo.
Mawasiliano: www.vivimachange.blogspot.com Simu 0755 200023










