Usalama mdogo viwanja vya soka nchini ni bomu linalosubiri kulipuka

06May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Usalama mdogo viwanja vya soka nchini ni bomu linalosubiri kulipuka

JUZI na jana tulichapisha habari ndefu iliyotokana na uchunguzi wa muda mrefu kuhusiana na viwanja vingi vya soka kutokuwa na usalama kwa watu wanaokwenda kuangalia mchezo huo ambao hupendwa na wengi nchini na duniani kwa ujumla.

Ripoti hiyo ilibainisha kwamba licha ya viwanja hivyo kuidhinishwa kutumika kwa mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu nchini, viwanja hivyo havikidhi vigezo vya usalama vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Kwamba Tanzania haina hata uwanja mmoja wa soka unaokidhi masharti yote ya kanuni za usalama.

Tulibaini kuwa viwanja vingi vya soka viko katika hali mbaya kimiundombinu licha ya wamiliki wake kupata mamilioni ya Shilingi kutokana na mgawo wa asilimia 15 wa mapato ya milangoni ya kila mechi.

Aidha, ilibainika wamiliki wa viwanja hivyo wamekuwa wakitumia fedha za mgawo wa mapato ya mechi kwa shughuli za kiutawala badala ya kuboresha viwanja.

Viwanja vya soka ni sehemu ambayo hutumiwa na maelfu ya watu bila kujali tofauti za itikadi zao za kisiasa, kidini, kijamii na jinsia.

Uchunguzi huo kadhalika ulibaini viwanja vyote vya soka nchini, vikiwamo 13 vilivyoidhinishwa na TFF kutumika kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, havikidhi matakwa ya Kanuni za Fifa.

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), asilimia 90 ya viwanja vyote vilivyoidhinishwa na TFF kutumika kwa mechi za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Daraja la Pili na Kombe la TFF msimu huu, vinamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kwamba kati ya viwanja 13 vilivyoidhinishwa kutumika Ligi Kuu msimu huu, nane (asilimia 62) vinamilikiwa na CCM na vyote havikidhi masharti ya ulinzi, usalama na burudani.

Vilevile imebainika kuwa ukiuondoa Uwanja wa Taifa, viwanja vingine vyote havitoi fursa kwa watazamaji kuingia uwanjani bila bughudha, kukaa kwa raha na starehe na urahisi wa kutoka uwanjani baada ya mechi.

Aidha imebainika kuwa, viwanja vyote vya soka nchini havina vifaa vya ukaguzi, udhibiti wa tiketi, uingiaji uwanjani pamoja na kutokuwa na uzio madhubuti wa kuzuia watazamaji kuwafikia wachezaji na waamuzi, isipokuwa Uwanja wa Taifa.

Suala lililotugusa zaidi ni kuwapo kwa usalama mdogo katika viwanja hivyo, hali inayoweza kusababisha maelfu ya watu wanaokwenda kuangalia soka au shughuli zingine wakadhurika ikiwamo kupoteza maisha.

Kutokuwapo kwa uzio wa kuwatenganisha watazamaji na waamuzi pamoja na wachezaji kunaweza kusababisha watazamaji kuingia uwanjani wakati wowote na kuwadhuru.

Lakini pia viwanja hivyo kutowekewa vifaa vya ukaguzi wa usalama kubaini kama watazamaji wameingia na silaha au vitu vinavyoweza kuhatarisha maisha ya watu ni udhaifu mkubwa ambao unapaswa kutafutiwa ufumbuzi haraka.

Kingine kinachochangaza ni viwanja hivyo kutofungwa kamera za usalama zinazoonyesha matukio yote ndani ya uwanja.

Mamlaka zinazohusika kuanzia wamiliki wa viwanja hivyo, TFF na vyombo vya dola zilitakiwa kuuona udhaifu huo kuwa unaweza kusababisha maafa makubwa. Kwa nini wasijiulize kuwa maeneo mengine kama viwanja vya ndege, hoteli kubwa, katika Bunge hatua za usalama zinapewa kipaumbele?

Isitoshe, hivi sasa dunia nzima inachukua hatua za tahadhari kutokana na kasi ya kutokea kwa matukio ya uhalifu hususan ugaidi. Hali hiyo inatutia hofu na ukweli ni kuwa ni bomu linalosubiri kulipuka ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.