Yanga haikamatiki ligi kuu

01May 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Yanga haikamatiki ligi kuu

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Bara, Yanga ya jijini Dar es Salaam, jana ilizidi kujisafishia njia ya kuelekea kutetea taji lao, baada ya kuilaza Toto Afrika ya jijini Mwanza kwa magoli 2-1 katika mchezo uliochezwa uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Golikipa wa Yanga, Doegratius Munishi 'Dida' akiokoa hatari golini mwake wakati wa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Toto African jana kwenye Uwanja Kirumba, Mwanza. PICHA:DANIEL MKATE

Katika dakika ya 39 kipindi cha kwanza, kona iliyochongwa na mchezaji wa Toto, Abdallah Seseme, ilitua kichwani kwa William Kimanzi na kuiandikia timu hiyo bao la kuongoza.

Baada ya bao hilo, wachezaji wa Yanga walijitahidi kucheza kwa nguvu ili kupata bao la kusawazisha kabla ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, lakini ukuta wa Toto ukiongozwa na Carlos Protus ulizuia mashambulizi ya wachezaji wa Yanga.

Licha ya juhudi za Ngoma, Simon Msuva na Amiss Tambwe, kutaka kusawazisha bao hilo,ziligonga ukuta hadi mwamuzi Ludovick Charles kutoka mkoani Kagera alipopuliza filimbi ya mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza pasipo timu yoyote kufanya mabadiliko, dakika 50, Deus Kasekealiisawazishia Yanga baada ya kuunganisha kwa mguu pasi safi ya Amis Tambwe.

Goli hilo liliwaamsha zaidi wachezaji wa Yanga baada ya kulishambulia lango la wapinzani wao mara kwa mara hali iliyompa wakati mgumu kipa wa Toto, Mussa Mohamed kufanya kazi ya ziada kuokoa hatari golini mwake.

Shambulizi la kushitukiza lililofanywa na washambuliaji wa Yanga, lilisaidia kuipatia timu hiyo ya mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam, goli la pili lililofungwa na beki wa kulia, Juma Abdul dakika 78 kufuatia piga ni kupige langoni mwa Toto African.

Baada ya goli hilo, Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa kwa wakati mmoja wachezaji watatu, nahodha Haruna Niyonzima, Tambwe na Kaseke huku nafasi zao zikichukuliwa na Thaban Kamusoko, Malimi Busungu na Matheu Anthony.

Baada ya mchezo huo, Kocha wa Toto, John Tegete,alimlalamikia mwamuzi wa mchezo huo, Charles kwa kuinyima timu yake penati hali aliyosema inaua mchezo wa soka nchini.

"Wote mmeshuhudia mechi ilivyochezwa, magoli yote yamepatikana kihalali, lakini mwamuzi kwa makusudi ametunyima penati...hali hii inachangia kudhoofisha soka letu," alisema Tegete.

Naye msemaji wa Yanga, Jerry Muro, aliipongeza Toto kwa kucheza kwa kujiamini na kuibana Yanga licha ya kujifunga magoli 2-1.

"Toto ni maswahiba wetu, lakini katika ushindani hatuangalii hilo....tumepambana dakika 90 licha ya kutanguliwa kufungwa, tumeshinda, nawapongeza sana," alisema Muro.

Kwa ushindi huo Yanga wamefikisha pointi 65 na kuzidi kuukaribia ubingwa wanaoushikilia toka msimu uliopita.
Ligi hiyo inaendelea tena leo katika uwanja wa Taifa kwa Simba kucheza na Azam zote za jijini Dar es Salaam.
Yanga sasa imefikisha pointi 65 na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu.

Ligi hiyo inaendelea tena leo wakati Simba inayoshika nafasi ya tatu itakapokuwa na kibarua kigumu mbele ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili.

Kocha wa Simba, Jackson Mayanja, amesema ushindi ni jambo pekee analolifikilia kwenye mchezo huo wa leo huku akisema anatarajia mchezo utakuwa mgumu.

Kocha wa Azam, Stewart Hall, alisisitiza kuwa bado wapo kwenye mbio za ubingwa na ushindi kwenye mchezo wa leo utainua molali kwa wachezaji wake.

Imeandikwa na Daniel Mkate (Mwanza) na Faustine Feliciane (Dar)