Mashindano hayo yaliyoanza juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mbali na wenyeji Tanzania Bara timu zingine zilizoshiriki ni pamoja na Kenya, Uganda, Zanzibar, Djibout, Ethiopia, Eritrea, Somalia, Sudan na Sudan Kusini.
Katika mbio za meta 5,000 wanawake, Wakenya Sandrafelis Tuei na Imaculata Chepkurui walishika nafasi mbili za kwanza baada ya kutumia dakika 16:15.80 na 16:26.97.
Nafasi ya tatu katika mbio hizo ilikwenda kwa Mganda Macyelene Chelangat aliyetumia dakika 16.29.56.
Katika mchezo wa kutupa mkuki kwa wanawake, Josephine Lalani na Victoria Anidi wote wa Uganda walishika nafasi ya kwanza na pili kwa kutupa umbali wa meta 44.95 na 43:19 huku Mwanahamimi Hassan wa Tanzania Bara akishika nafasi ya tatu.
Wilcliffe Kanyamal wa Kenya alimaliza wa kwanza katika mbio za meta 800 kwa kutumia dakika 1:50.43 huku Mekoneni Ayele wa Ethiopia alimaliza wa pili kwa kutumia dakika 1:50.43 na Abdi Fatah wa Djibout alimaliza watatu kwa kutumia muda wa 1:51.73.
Kuruka chini, Lagat Kibet wa Kenya alishika nafasi ya kwanza baada ya kuruka meta 7.47.
Mzanzibar Gulan Khamis alitamba katika meta 100 baada ya kushika nafasi ya kwanza kwa kutumia sekunde 10.57 huku Mkenya Moffat Ngari akimaliza wa pili kwa kutumia dakika 10.60 na Msudan Mohamed A, Mohamed akishika nafasi ya tatu kwa kutumia sekunde 10.79.










