MACDONALD MWAKAMELE: Zao la Tanesco anayeng’ara ugenini

29Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
MACDONALD MWAKAMELE: Zao la Tanesco anayeng’ara ugenini
  • NI mtaaramu wa kutengeneza umeme bila ya kuuzima

Kumekuwapo maoni juu ya namna ya kushirikisha juhudi binafsi na sekta ya umma, katika namna ya kuleta maendeleo kati ya taifa kwa utaratibu unaojulikana kama PPP, yaani ubia kati ya sekta binafsi na ya umma.

Macdonald Mwakamele.

Suala hilo hivi sasa limeshatimia kisera na kisheria. Moja ya sekta zinazokabiliwa na changamoto kubwa ni ya nishati na umeme.

Kwa bahati, Macdonald Mwakamele, ni Mtanzania mwenye utaalamu wa kufanya matengenezo ya umeme bila ya kuuzima.

Alipozungumza na Nipashe hivi karibuni ana maoni kadhaa akilishauri Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), iachane na jukumu la kusambaza umeme na badala yake itoe zabuni kwa kampuni binafsi, akiamini ni hatua itakayowapunguzia gharama za uendeshaji.

Ifuatayo ndiyo ilivyokuwa mazungumzo yao ya Ana kwa Ana:

SWALI: Teknolojia ya kufanya matengenezo ya umeme bila kuuzima uliipata wapi?

JIBU: Nilipata elimu na ujuzi huo kutoka kampuni ya Kimarekani, ambayo hutengeneza vifaa na kutoa mafunzo katika nchi za dunia ya kwanza na ya tatu ya AD Chance.

SWALI: Tueleze kama baada ya kuipata teknolojia hiyo, uliwahi kuitumia wapi hapa nchini kwa maana ya kuajiriwa?
JIBU: Ni katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na katika kampuni binafsi na niliajiriwa na Tanesco, lakini baada ya kutaka kubinafsishwa, niliona niwe tayari kujiajiri. Sikutaka kubinafsishwa, kwa kuwa taaluma yangu ingekuwa vigumu kubinafsishwa.

SWALI: Ulifanya kazi hiyo nchini kwa muda gani?

JIBU: Toka mwaka 1988 hadi mwaka 2012.

SWALI: Zipo taarifa kwamba uliwahi kufanya kazi Tanesco na kwamba kuna kiasi kikubwa cha deni ambalo unalidai shirika hilo, je taarifa hizo ni za kweli? Kama ni kweli, ni kiasi gani unadai na umeshalipwa au la? Kama bado nini kinaendelea sasa?

JIBU: Sijui ni wapi zimetoka taarifa hizo? Ila kwa sasa hakuna ninachowadai Tanesco, labda kama kuna madai wanayoyajua wao.

SWALI: Wewe kama mtaalamu wa kufanya matengenezo ya umeme bila kuuzima, ni kwa nini hadi leo teknolojia yako umeipeleka nje ya nchi badala ya kuitumia kuwasaidia Watanzania?

JIBU: Hayo ni maoni ambayo kila binadamu akifanya kazi nyumbani na kueleweka na kama nje hawana utaalamu siyo mbaya kwenda kuwapa utaalamu huo. Ni moja ya fursa ya kupanuka kibiashara. Nchi nyingi zinahitaji kufundishwa kwa kutokuwa na uelewa wa teknolojia hiyo.

SWALI: Ni kitu gani unadhani kikifanyika unaweza kubadili nia yako na kurejea nchini kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu, ikizingatiwa kuwa miongoni mwa malengo makubwa ya serikali ya Rais Dk. John Magufuli ni kuhakikisha nchi inapata umeme wa kutosha utakaoipeleka katika viwanda kuelekea uchumi wa kati?

JIBU: Hili halina pingamizi, tunapokuwa nje kuitwa ‘foreigners’ (wageni), huwa inatupa taabu! Hivyo, kurudi nchini ni muhimu kwa kuwa viwanda vinahitaji umeme na Tanesco inahitaji umeme.

Lakini Tanesco haijafahamu kuwa kuwa usambazaji ndilo tatizo na matengenezo siyo lazima uzime umeme. Mimi ninachohitaji ni kutoa elimu kwa vijana ya matengenezo ya umeme bila kuuzima.

Ninahitaji kurudi nchini kusaidia nchi. Ni kama Watanzania walivyofanya kwenda kuzisaidia nchi zingine za Afrika baada ya kupata uhuru, kisha wakarejea nyumbani.

SWALI: Umewahi kwa siku za karibuni kukutana na viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini au Tanesco kujadiliana nao juu ya uwezekano wa kurejea nchini ili serikali inufaike na ujuzi wako?

JIBU: Kukutana nao bado, lakini ni lazima wakafahamu kuwapo kwangu. Sijui ‘pressure’ (msukumo) yao hiyo ya biashara ya umeme wanaichukuliaje!

Nimefanya kazi na Wazungu na Waafrika, ila Waafrika hadi sasa hawajaona uchungu wa kupoteza uniti moja ya umeme, wakati Mzungu anatafuta kila aina ya jitihada isipotee. Kwa kuwa nimefanya kazi na Wazungu, inakuwa vigumu Waswahili kunielewa.

Teknolojia ya kutengeneza umeme bila kuuzima iko Tanzania kuliko nchi zote za Afrika na Afrika Kusini, licha ya kuwa na vifaa vingi vya kisasa, lakini bado iko nyuma kwa Tanzania.

Hata Kenya walikuja kunitembelea katika ‘training centre’ (kituo cha mafunzo) yangu ya Morogoro na hadi sasa wanaitumia kwa maana ya wanatumia mawazo yangu.

SWALI: Moja ya kero kubwa za wananchi ni kukatika ovyo kwa umeme na wakati mwingine kutolewa kwa mgawo kwa maelezo kuwa ni kutokana na matengenezo. Wewe kama mtaalamu wa matengenezo ya umeme bila kuuzima hili unalizungumziaje?

JIBU: Hali hiyo inayotokea nchini ni makusudi matupuya baadhi ya watu kwa kuwa suala hili serikali ilishalimaliza.

Hakuna matengenezo yanayofanyika bila kuzima umeme. Wakiamua inawezekana, bali wanachokifanya ni makusudi.
SWALI: Je, unaweza kuzungumziaje hasara ambayo inasababishwa na hali hiyo kwa Tanesco na Taifa kwa ujumla?

JIBU: Sijui kama Tanesco iliwahi kupata faida. Hali hii inatokana na kupoteza umeme. Tatizo hili lilishatatuliwa wakati wa manejimenti ya Net Group zaidi ya miaka 20 iliyopita. Tatizo ni wahandisi wapya kuwa na upeo mdogo.

Wengi hawajawahi kupanda nguzo na kushika umeme kama mimi. Pia, hali hiyo inasababishwa na biashara ya umeme kuwa ngumu na wahusika kufanya maamuzi yasiyo na tija (yasiyo ya kihandisi).

Biashara ya umeme hawaifahamu vizuri, lakini ni biashara kama nyingine.

Ni sawa na biashara ya kulima na kuuza mpunga au mahindi. Haiwezekani mfanyabiashara ya mahindi akubali gunia aliloweka mahindi lipasuke wakati anayapeleka sokoni bila kuchukua hatua, kwa kuwa bila hatua atashtukia anafika sokoni bila gunia lake kuwa na mahindi ya kuuza.

SWALI: Kuna taarifa kuwa una chuo chako mkoani Morogoro. Tueleze kwa sasa chuo hicho unakitumia kwa kazi ipi na malengo yako ni nini katika siku za usoni?

JIBU: Ni kweli ninacho, kipo eneo la Mvomero. Ni chuo pekee ambacho kingetoa vijana wengi ambao wangefanya kazi hiyo bila ya kuzima umeme. Lakini, kutokana na watu kadhaa kunipiga vita, ilipowaingiza kazini Net Group baada ya viongozi wa ngazi za juu wa Tanesco kuondolewa, ilijengeka chuki.

Wageni hao waliniita nikapige kazi. Ikapatikana faida na wakanichukia na hasira ziliishia kwangu. Nilijua vitu vya kawaida!

Nilipokea wageni kutoka nchi 27, lakini nikazimiwa umeme kunizuia nisifanye maonyesho. Nilijua yanapita, baadaye ilikuja kampuni ya Kenya Power kwa ajili ya kuona teknolojia, tena wakanizimia umeme.

Kwa matukio hayo niliona suala ka Net Group limeniumiza na nikaona chuo nikiuze na hivi ninavyozungumza kipo sokoni.
SWALI: Tueleze jinsi gani wenzetu huko nje ya nchi unapofanya kazi wanavyokutumia na kunufaika na utaalamu wako.

JIBU: Kenya wamekuja tukazungumza vizuri, wataielewa teknolojia hiyo na na kuitumia. Nchi nyingine zilizoanza kuitumia ni Zambia, Malawi, Botswana na Nigeria, achilia mbali nchi kadhaa za Ulaya. Nashangaa niko Tanzania situmiki wakati ninawapa maarifa yanayosaidia.

SWALI: Unaishauri nini Tanesco ijiendeshe kwa tija na ufanisi ikiwamo, kuondokana na hasara inayodaiwa inaipata kila mwaka?

JIBU: Kwanza Tanesco na taifa kwa ujumla wajue kuwa umeme ni biashara. Waachane na ununuzi wa umeme kwa kuwa hivi sasa nchi ina gesi ya kutosha, hivyo wazalishe umeme wa kutosha na kuuuza nje ya nchi.

Tanesco iachane na kazi ya kusambaza umeme kwa wateja, badala yake iwape zabuni makandarasi binafsi na yenyewe ibaki na jukumu la uzalishaji na usafirishaji.

Kampuni zote zinazozalisha umeme zipewe kibali cha kuuza zenyewe. Makandarasi binafsi wakipewa kazi ya kuuza umeme, hatua hiyo itaisaidia Tanesco isiibiwe na kupoteza umeme kama shirika hilo linavyoathirika.

SWALI: Tumewahi kukusikia ukishauri kwamba ili Tanesco ijinusuru na matatizo inayokumbana nayo haina budi kugawanywa katika vitengo vitatu vya; Uzalishaji, Usafirishaji na Usambazaji. Bado unasimamia mtazamo huo?

JIBU: Nimebadili msimamo kwa sasa kuhusiana na suala hilo. Kwa sasa, shirika hilo linapaswa kubakia na jukumu la uzalishaji na usafirishaji.

Kazi nyingine waachiwe watu binafsi ambao watawatumia wafanyakazi walewale wa Tanesco na watafanya kazi kwa mbinu za kisasa zaidi kuliko ilivyo sasa.

Swali: Kwa nini usiombe fursa ya kukutana na viongozi wa wizara, ukawapa uzoefu wako na kuwashauri mambo mbalimbali yanayoweza kuinufaisha nchi katika sekta ya umeme?

JIBU: Kinachozuia fursa ni kutokana na kupigwa vita na kuambiwa mambo yale yale yasiyo na mashiko. Ila binafsi wakati wowote niko tayari kukutana nao na kutoa ushauri kwao.

Nimetengenezwa na Tanesco, tofauti na wengine.

SWALI: Nini ushauri wako kwa Watanzania na taifa kwa ujumla?

JIBU: Rais Magufuli ameonyesha ukweli katika system (mfumo) kwa kutomsamehe mtu muongo. Tanzania ya sasa inapaswa kubadilika. Kinachoisumbua ni majungu na uongo. Siyo rahisi maendeleo kupatikana katika majungu na uongo.