Kilichoivusha Bandari ya Tanga kuwa kituo cha bomba la mafuta Uganda

29Apr 2016
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Kilichoivusha Bandari ya Tanga kuwa kituo cha bomba la mafuta Uganda

WIKI iliyopita ndiyo mbovu na mbichi ilijulikana kuhusiana na uamuzi wa kupitisha bomba la mafuta kutoka nchini Uganda, hadi kwenye bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Sehemu ya bandari ya Tanga. (PICHA NA MTANDAO).

Katika mchuano uliiohusisha bandari za Lamu na Mombasa Kenya, Tanga ilibuka kuwa na vigezo bora vya uchaguzi huo wenye maana kubwa.

Wizara yenye dhamana na mafuta na madini, haifichi shukurani zake kwa Rais Dk. John Magufuli kwa kufanikisha mapambano ya kuhakikisha bomba linapitia nchini.

Kazi ilianzia kwa mashauriano chini ya Rais Dk. John Magufuli na kisha inaandaliwa timu ya kufanya kampeni hiyo kufanikisha kile kilichopatikana wiki iliyopita.

Katika mafanikio hayo, Wizara ya Nishati na Madini inasema kuwa ilikuwa inapigana kufanikisha mambo makuu mawili, ambayo ni ubora wa bandari na njia zitakazopitishia bomba lenyewe.

Anasema karika ushindani huo, waliangalia njia ambazo ni salama na rahisi kupitisha bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga.

KILICHOIVUSHA BANDARI TANGA

Bandari zilizokuwa katika ushindani ni Mombasa, Lamu na Tanga ambayo iliibuka mshindi kwa ubora wa juu zaidi. Mombasa ilitolewa mapema kwenye ushindani na kubaki bandari za Tanga na Lamu.

Vigezo viIivyoinyanyua Bandari ya Tanga ni kina kirefu ilichi nacho, ikilinganishwa na Lamu, Mombasa, Dar es Salaam na Mtwara.

Anasema Bandari ya Tanga ina kina kirefu cha zaidi ya mita 25 ambacho ndicho kinachohitajika kimataifa kuwezesha meli kubwa zenye shehena kuweza kuchukua mafuta.

Pia, Bandari ya Tanga inaweza kufanya kazi kwa siku 365 (mwaka mzima), kutoka na kuwa jirani na kisiwa cha Pemba na vingine vidogo vidogo.

Anasema visiwa hivyo vinasaidia kuzuia upepo mkali, mawimbi na dhoruba kali ambazo zinaweza kusababisha meli kutia nanga.

“Wote mtakuwa mashahidi, wakati watu wanaotoka Afrika ya Mashariki, walikuwa wakija wakati wa upepo wa Mansuli, kwani unawaleta haraka na kuwezesha kuzuia mawimbi makubwa,” inatamka mwongozo mmojawapo.
Kwa upande wa gharama, Tanga haina hitaji ya kuchimbwa ili kuongeza kina, wakati Lamu na Mombasa zilikuwa na hitaji hilo.

Pia ina manufaa mengine kwamba, haikumbwi na upepo wenye wastani wa mwendo kasi zaidi ya mikta 10 kwa sekonde, ambao ndio una uwezo wa kuikinga meli. Upepo huo unadhibitiwa na visiwa vilivyopo kulia kwake.

“Upepo huo huvunjwa vunjwa na kutofika mita 10. Upepo huo mkali ndio unasaidia kuzalisha umeme wa upepo kama wa Singida na Makambako na una kasi kubwa sana na ndio sababu tukaibuka na ushindi mkubwa,” inaeleza taarifa ya wizara.

NJIA YA MAFUTA

Anasema kwa upande njia ambako bomba litajengwa kutoka Uganda mpaka Tanga, pia Tanzania ilikidhi vigezo.
Bomba hilo linaelezwa kwamba litapitishwa kutoka Ziwa Albert Magharibu mwa Uganda hadi kwenye Bandari ya Tanga. Njia itaanzia Gohima kunakochimbwa mafuta hadi bandarini Tanga.

Nchini bomba linatarajiwa kupitia mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Simiyu, Kaskazini mwa mkoa wa Dodoma hadi Tanga na manufaa ya nia hiyo ni kwamba, zitapita kwenye mteremko utakaowezesha mafuta kupita kirahisi.

Ili kuwepo ufanisi ni kwamba, mafuta hayo ni lazima yepitie kwenye tambarare na kuwa na gharama ndogo, ikilinganishwa na kama ingepita Lamu ambako kuna maporomoko na milima.

Kigezo kingine kilichoangaliwa ni uwepo wa barabara na reli za kusafirisha mizigo ya kujenga bomba za kupitisha mafuta.

Inaelezwa mchango mkubwa wa kazi iliyofanywa na Rais Dk. Magufuli, kwamba barabara hizo zimejenga vigezo muhimu katika kufanikisha uteuzi wa bandari ya Tanga, akitoa mfano wa safari kati ya Singida kwenda Handeni ni kilomita 1,444.

USALAMA

Jingine lililoangaliwa ni usalama wa mabomba kupitia Tanzania, ikitumika marejeo ya mabomba ya Tazama Pipelines yanayosafirisha mabomba kati ya Tanzania na Zambia, ambayo ilijengwa mwaka 1968.

Pia, anasema Tanzania ina bomba lingine la gesi kutoka visiwa vya Songosongo mwaka 2004 na uzoefu wa bomba la Mtwara Mnazi Bay lililokamilika mwaka 2006.

Anasema bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es salaam, lenye urefu wa kilomita 542, ambalo litakuwa mara tatu ya bomba litakalojengwa sasa.

Bomba hilo la mafuta linalotarajiwa kukamilika mwezu Juni mwaka 2020.

FAIDA ZA BOMBA

Faida ya mojawapo kutumika kusafirisha mafuta ghafi, pia bomba hilo litatumika kusafirisha mafuta ya nchi jirani za Uganda, Burundi, Kenya, Rwanda na DRC.

Pia, kuna ugunduzi wa mafuta ambayo yameanza kufanyiwa kazi katika Ziwa Tanganyika na uwepo wa bomba hilo unaweza kusafirisha mafuta yake.

Ushuru wa kupitisha mafuta kwa kila pipa ni Dola za Marekani 12.2 (Sh. 26,657) kwa bomba na mapipa 200,000 kwa siku yatasafirishwa. Mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani Bilioni 4.

Anasema pia mtambo wa kusindika LAG unagharimu dola 20 hadi 30 hivyo ni wazi kuwa inakuwa ni nchi ya mapinduzi makubwa.

Vijijini kunaelezwa kwamba, kutawanufaisha wananchi kuunganishiwa umeme vijijini, kupitia kodi zitakazolipwa pamoja na faida nyingine.

Aidha, fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kuwezesha kuunganisha umeme na kupata fursa za kibiashara za kuuza bidhaa mbalimbali kwa watu wanaofanya kazi ya kujenga bomba.