Daktari: Sumu ya wazee iko kwenye pombe na lishe duni

28Apr 2016
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe
Daktari: Sumu ya wazee iko kwenye pombe na lishe duni

LISHE ni virutubisho vinavyojenga chembe kwenye mwili na kufanya maisha ya watu yawe ya muda mrefu.

Wazee katika Kituo cha Kulea Wazee cha Nshamba, wilayani Muleba, wakifanya mazoezi ya viungo. PICHA: NA LILIAN LUGAKINGIRA.

Pia katika jamii ya wanadamu, wazee ni moja ya kundi linalohitaji kiwango kikubwa kupata lishe bora, kwa sababu wanahitaji kujenga afya zao na kusababisha umri wao kuwa mrefu kwao.

Tatizo la lishe bora kwa wazee, ni changamoto inayosababisha afya zao kudhoofika na baadhi hufikwa na mauti mapema.

Zipo sababu nyingi zinazotajwa kusababisha wazee kukosa lishe bora, ikiwamo hali ngumu ya kiuchumi.

WAZEE WAJIELEZA

Mzee Vedastus Kaiza (70), mkazi wa kijiji Butainamwa Bukoba Vijijini, anathibitisha kuwa ukosefu wa kipato ni chanzo kikuu cha wazee kukosa huduma muhimu za kila siku, zikiwemo za afya na pindi zinapokosekana, inaendana na wao kudhoofika.

Kaiza anasema wazee hufikia hatua hiyo, kutokana na nguvu zao za utendaji kufikia ukomo na wanaanza kuwa tegemezi katika sehemu kubwa ya maisha yao.

Kuhusu uhusaino baina ya wazee na watoto zao, Mzee Kaiza anatamka:“Unaweza ukawa na watoto wasikujali au unao, lakini hawana kipato cha kukutunza.”

Anaongeza:”Au ulizaa watoto, lakini Mwenyezi Mungu akawachukua na tayari wewe umezeeka, lazima uishi maisha ya shida na huwezi kupata uwezo wa kula mlo kamili.”

Kuhusu suala la wazee kutopenda kujishughulisha, Kaiza anasema hilo linategemea uwezo wa mzee huyo kiafya.

Maelezo ya Mzee Kaiza, yanatofautiana na Mzee Theonestina Mwoleka (73) mkazi wa kijiji Bwizanduru, Kata Maruku Bukoba Vijijini.

Anasema tatizo kuwapo asilimia kubwa ya wazee wanaokosa lishe bora kutokana na ugumu wa maisha, linasababishwa na uvivu.

Mwoleka anasema uvivu na matumizi mabaya ya rasilimali, huwafanya watu wengi wenye nguvu wanashindwa kuandaa maisha ya baadaye na pale wanapoishiwa nguvu, hujikuta hawana mahali pa kuanzia, wanaishia kuwa ombaomba.

Anaishauri jamii kuwa na tabia ya kupanga maisha ya baadaye, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza changamoto zinazowakabili wazee na wanaoangukia mazingira magumu ya maishakwa kukosa lishe bora.

“Uvivu husababisha mtu kuzeeka haraka, kwa sababu hawezi kula akashiba. Kwa hiyo, mwili unazidi kunyong’onyea, pia ulevi wa kupindukia unasababisha afya kudhoofika haraka na kuzeeka mapema” anasema.

Anawashangaa baadhi ya wazee wenye umri unaofikia miaka 60 wanashindwa kunyanyuka, ilhali yeye ana miaka 74, ana nguvu na anajitahidi kufanya mazoezi kwa kulima mashamba madogo.

“Mzee inabidi afanye kazi za kawaida, ili mwili uwe na mazoezi na kula mlo kamili, sio lazima kula vyakula vya gharama kubwa,” anasema na kuongeza:

“Anaweza kula vyakula vya asili kama vile mchicha, majani ya kunde, mbaazi, vitu ambavyo mzee anaweza kulima mwenyewe kidogo kidogo.”

Anapinga dhana iliyojengeka kwamba mwili unajengwa na vitu vya gharama kubwa kama vile nyama, samaki na mayai, kwani kuna mbadala unaptokana hata shambani kwake,
ambao humsaidia kujenga afya.

“Unakuta mtu ana shamba limekwishakuwa pori, hakuna chakula chochote cha kumsaidia, wakati kama angejishughulisha vitu vingine hata kama hana kipato anaweza kuvipata kutoka shambani, akipata hela anunue sukari, chumvi na vitu vingine” anasema na kuongeza:

“Mimi tangu mwaka 1986 sijawahi kuugua nikapelekwa hospitali kuchomwa sindano, najitibisha na dawa za asili za Kihaya. Ninapojisikia kuumwa, naiandaa na kunywa, napona kabisa na nina afya nzuri,” anajigamba Mzee Mwoleka.

Pia Mzee Mwolekaa anawataka wananchi ama kupunguza au kuacha matumizi makubwa ya sigara, zinazodhoofisha afya za wazee na kuwafanya washindwe kujihudumia.

DAKTARI

Stephen Baruti ni Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Rwamishenye katika Manispaa ya Bukoba. Anasema uzee unahitaji lishe bora, kwa sababu kadri mtu anavyoendelea kuzeeka, kinachoathirika ni kinga zinazojenga mwili wake.

Dk. Baruti anasema kinga zinapokomaa sana, zinachoka na kuufanya mwili wa mzee uwe duni katika kuzalisha chembehai, hata inaishia kuwa na kinga ndogo.

“Lakini Kwa sababu ‘cells’ (chembehai) huzaliwa, hukua na hufa, unakuta zinazozaliwa zinaendelea kupungua kadri zinavyokua na mwisho zinakufa. Kwa hiyo, zinazokufa ni nyingi, lakini zinazozaliwa ni kidogo. Hapo ndipo mwanzo wa uzee unapoanza,” anasema.

Mtaalamu huyo anaongeza kuwa, lishe ni muhimu na hasa kwa wazee, kwani ikibidi inaongeza nguvu ya kinga ambayo inaelekea kuelemewa.

“Wazee inabidi tuwape vyakula vyenye virutubisho ambavyo vina makundi tofauti kulingana na mahitaji. Siyo lazima ale vyakula vyote, anaweza akawa anapungukiwa vyakula fulani, kulingana na ushauri wa kitaalamu” anasema.

Dk. Baruti anasema, uzee unahitaji kurutubishwa ili kusaidia kuongeza nguvu. Anafafanua zaidi:

“Ukimchukua mzee ambaye alikuwa anafanya kazi akastaafu na ana maslahi makubwa, ni tofauti na mzee wa kijijini ambaye mlo wake ni wa mahesabu. Ukiwaweka pamoja, kuna mzee utamwona maisha yake yanakwenda pabaya kwa sababu ya kukosa lishe.”

Anasema ni muhimu kula vyakula vyenye virutubisho, lakini siuo lazima kula vya gharama kubwa na mzee anaweza kula dagaa, maharage, senene kwa wakazi wa mkoa wa Kagera, nazo zina protini zaidi.

“Mzee anaweza kula matunda ambayo yanapatikana katika mazingira wanayoishi kwa mfano maembe, mapapai, machungwa, nanasi, maparachichi na mengine ya asili.

“Pia, anaweza kula mboga za majani kama mchicha na karoti, zinasaidia kuongeza uwezo wa kuona” anasema Dk. Baruti

Anaongeza kuwa vyakula vingi vina faida, pia hasara. Kwa mfano kuna mafuta yanyojenga mwili na kuleta joto mwilini, lakini mtu anavyoendelea kukua, mwili unaendelea kusinyaa. Kwa hiyo, mishipa ya kupeleka damu nayo inakuwa imejaa mafuta.

“Badala ya kufanya moyo kufanya kazi vizuri, mishipa ambako damu inapita inasinyaa na inakuta tayari kuna mgando, badala yake unatengeneza tatizo la moyo, sukari, unene na kushindwa kuona” anasema Dk.Baruti.

WAZEE NA POMBE

Mtaalamu huyo wa afya anasema, si vyema kwa wazee kuendekeza pombe kutokana na kinga inayozalishwa mwilini mwao kuwa ndogo na unywaji una kawaida ya kuendelea kuwachosha. Hapo ndipo inapokaribisha maradhi kama ya figo na bandama.

“Kwa sababu ya uwezo wa kufanya kazi kuwa mdogo ndani ya mwili, hata uwezo wa mapafu kupanuka ni mdogo, ni rahisi magonjwa mengi kulipuka hasa wazee wanaovuta sigara au bangi, wanaweza kupata magonjwa kama kifua kikuu.” anasema.

Dk. Baruti anasema kutokana na kinga ndogo, inaweza kusababisha magonjwa na kupona kwao kunakuwa kugumu, kwa sababu ya umri wao.

Ili afya za wazee ziendelea kuimarika. Dk. Baruti anashauri mazoezi ya viungo, kwamba ni tiba ya kuuondolea mwili uchovu.

Anashauri wazee kwamba hawapaswi kuwa na msongo wa mawazo, pia ni wajibu wa jamii inayowazunguka kuwaona wazee wahitaji kwa kuwapa kipaumbele katika huduma za kijamii.

Dk. Baruti anatoa mfano mzee anapokwenda hospitalini, hapaswi kuachwa apange mstari na kukata tamaa.

“Wazee nao wajitambue na kudai haki zao ili wapewe huduma kama wazee, kutoka kwa jamii na serikali” anatamka mganga huyo.

SERA YA WAZEE

Kutokana na wazee kushambuliwa na magonjwa mara kwa mara na kukosa matibabu sahihi kutokana na hali mbaya kiuchumi inayowakabili, serikali imeanzisha sera ya kundi hilo kupatiwa matibabu bure, ili kuhakikisha afya zao zinakuwa imara.

Hata hivyo, sera hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo uhaba wa bajeti unaosababisha upungufu wa dawa katika hospitali na kufanya huduma ya kundi hilo inatolewa kwa kiwango kidogo, tofauti na ilivyokusudiwa.

Sista Inviolatha Temba, ambaye ni Katibu wa Hospitali teule ya Mugana wilaya ya Missenyi, anasema wagonjwa wanaohitaji kuhudumiwa bure, inaongezeka kila kukicha na kufanya hospitali kutokuwa vizuri kiuchumi.

“Hata makusanyo ya kila siku ya hospitali yanaonekana kuwa kidogo maana makundi ya wazee, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na kinamama wajawazito, ndio kundi kubwa linalofika hospitali mara kwa mara kuliko makundi mengine,” anasema.

Sista Temba anasema ruzuku inayotolewa kwa makundi hayo ni Sh. milioni 75 kwa mwaka, wakati kila mwezi wanatumia Sh. milioni 15 kuhudumia makundi hayo, linalojumuisjha wazee.

“Utakuta kundi la wazee linatengewa shilingi milioni kumi kwa mwaka. Ni kidogo mno na mzee hawezi kuja kutibiwa ukamrudisha kwa madai ya kutokuwa na dawa,” anasema.

Anatumia fursa hiyo kuiomba serikali kuongeza fungu la kuwahudumia wazee ili wapate huduma inayostahili na kupunguza malalamikoyanayotokana na huduma zisizoridhisha kwao.

Mratibu wa Shirika la Saidia Wazee Karagwe (Sawaka), linaloshirikiana na mashirika mengine ya mkoani Kagera kuwahudumia wazee, Livingstone Byekwaso, unakadiriwa kuwa na wazee 125,089 wakiwamo wa kiume 55,154 na wa kike 69,935.