Kumbe kimya kingi cha Dk. Shein kilikuwa na mshindo mkubwa baada ya kuchukuwa muda wa siku 16 kutangaza baraza la mawaziri tangu alipoapishwa kuwa rais wa Zanzibar Machi 24, mwaka huu tofauti na kipindi chake cha kwanza ambacho hakuchukua muda mrefu alitangaza baraza la mawaziri.
Ilikuwa ni majira ya saa nne asubuhi ya april 9 mwaka huu,ikulu mjini Zanzibar waandishi wa habari walikuwa wakisubiri kwa hamu,uteuzi huo wa baraza la mawaziri na ndipo Dk Shein alipovunja ukimya na kutangaza baraza la mawaziri ambalo lilikuwa na sura mpya wengi wao wakiwa ni vijana.
Dk. Shein alitangaza baraza hilo la mawaziri likiwa na wizara 13 na mawaziri 15 na manaibu waziri saba wakati baraza lililopita lilikuwa na wizara 16 likiwa na mawaziri 19 na naibu mawaziri wanane.
Uteuzi huo umewashangaza watu wengi baada ya kuona sura nyingi mpya za mawaziri na kuachwa ambao wengi ni magwiji ambao walikuwa wamezoeleka katika serikali iliyopita.
Uteuzi huo umesifiwa na watu mbalimbali na kusema kuwa uongozi sio mali ya mtu na uamuzi wa Dk. Shein kuchaguwa mawaziri wapya wengi wakiwa ni vijana umedhihirisha hatua hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kuwa uamuzi wa Dk. Shein ni makini na wenye mwelekeo mzuri wa kuleta tija ndani ya serikali.
“Kuwateuwa mawaziri wenye sura mchanganyiko wengi wao wakiwa wapya, tena ni watu makini naamini watafanya kazi kwa kasi ya ajabu katika kuwatumikia wananchi,” anasema Vuai.
Anasema rais ametimiza ahadi ya kuunda serikali itakayoshirikisha Wazanzibari wote na kitendo cha kuwateuwa Hamad Rashid wa ADC, Juma Ali Khatib TADEA na Said Soud wa AFP kuwa mawaziri ni kielelezo cha kuwaunganisha Wazanzibari bila kuangalia itikadi za vyama vyao.
Vuai alisema serikali iliyopita iliyoongozwa na Dk. Shein ikiwa na mawaziri kutoka CCM na CUF imefanya kazi vizuri katika uwajibikaji na utendaji kazi kwa mujibu wa mazingira ya wakati huo licha ya kuwapo kwa changamoto zilizojitokeza mwishoni.
“Uwajibikaji ulikuwa mzuri, mchanganyiko wa mawaziri katika serikali iliyopita utatofautiana na sasa kwa sababu baadhi ya mawaziri katika serikali iliyopita nia zao hazikuwa safi katika kuwatumikia Wazanzibari,” alisema Vuai.
Saleh Mhina ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Zanzibar (Suza), anasema Dk. Shein amefanya maamuzi mazuri ya kuteua sura mpya kwenye Baraza la Mawaziri na kwamba amedhihirisha kuwa uwaziri sio mali ya mtu bali ni kazi inayoendana na nguvu, malengo na kasi ya utendaji kazi.
“Kama inavyofahamika mipango ya serikali iliyopita ilikuwa ikifika mwaka 2020 kufikia uchumi wa kati na ameshaanza misingi yote katika kipindi cha mwanzo na katika kipindi hiki cha pili apate watu ambao wanaweza kukimbia na kasi hiyo…amenifurahisha sana kwa uteuzi wake wa mawaziri nawaomba mawaziri wasimwangushe,” alisema Mhina.
Aidha, anasema kitendo cha Dk. Shein kuwateua baadhi ya watu kutoka vyama vya upinzani ni kuunda serikali yenye sura ya umoja wa kitaifa.
Alisema Serikali iliyopita ilikuwa nzuri japokuwa ilikuwa na ushindani kwa sababu mambo mengi ambayo yaliokuwa yakifanyika katika baraza la mapinduzi mengine yakiwa ni siri yalikuwa mitaani.
Mwanafunzi mwingine kutoka Chuo cha Fedha, Salha Hamad Hussein, anasema kuwapo kwa sura mpya katika Baraza la Mapinduzi na hasa vijana kunaleta utendaji chanya ndani ya miaka mitano.
Anasema utendaji katika awamu ya kwanza ya Dk. Shein haukuwa wa kuridhisha kwa kuwa siri nyingi za serikali zilikuwa zikivunja na wavujishaji walikuwa ni mawaziri.
Mwanaharakati wa masuala ya kijamii, Yussuf Mchenga, anasema uteuzi wa Baraza la Mapinduzi ni makini na kwamba utaondoa ufanyajikazi kwa mazoea kwa kuwa wananchi wanataka mabadiliko.
Naye Mwanasheria wa kujitegemea, Awadhi Ali Said, anasema serikali iliyopita ni tofauti na serikali ya sasa kwa sababu baadhi ya wananchi kwa kutoridhishwa na upatikanaji wa serikali hiyo ambayo haijazingatia demokrasia.
Alisema chama kikuu cha upinzani CUF hawaitambui serikali hiyo na baadhi ya wahisani kusitisha misaada yao Tanzania kutokana na kutoridhishwa na upatikanaji wa serikali hiyo.
“Serikali iliyopo itakuwa na changamoto ya kulinda amani ya nchi kwa sababu baadhi ya watu hawajaridhika na mwenendo wa upatikanaji wa serikali hii ikilinganishwa na serikali iliyopita ambayo wananchi waliridhia na kutoa ushirikiano mkubwa,” anasema Awadhi ambaye alikuwa rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar.
Mwenyekiti wa shirikisho la vyuo vikuu CCM Zanzibar, Khamis Kheri Ame, alisema Baraza la Mawaziri ni bora kwa sababu kuna watu wenye uwezo na wasomi ambao wameteuliwa kutokana na taaluma zao.










