Lengo la mpango huo ambao uliwasilishwa bungeni Jumatano iliyopita na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, ni kufanya mageuzi ya viwanda na kuwaondoa Watanzania kwenye lindi la umasikini.
Mpango huu wa miaka mitano, umeainisha fursa lukuki za uwekezaji kwa Watanzania wanaotaka kufanikisha ndoto hizo za Serikali ya Awamu Tano.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, utayarishaji wa mpango huo umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango Elekezi wa Miaka 15 na mafanikio na changamoto zilizobainishwa katika mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16) na Mkukuta II.
Tofauti na mipango iliyopita, awamu Serikali imefungamanisha na kuwianisha mifumo ya mpango na Mkukuta, sera na mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa.
Serikali imeridhia, hususan Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), Dira ya Afrika 2063, Mpango-kazi wa Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika (2008), Sera ya Viwanda ya Afrika Mashariki na mkakati wa utekelezaji wake, Mwelekeo wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC (2013 – 2018) na Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC (2015 – 2063).
Ili kufikia malengo hayo, Dk. Mpango anasema kiasi cha Sh. trilioni 107 zinahitajika kugharamia utekelezaji wa mpango kwa kipindi miaka mitano sawa na Sh. trilioni 21.4 kila mwaka.
Waziri huyo anasema katika fedha hizo Serikali itachangia trilioni 59 sawa na sh. trilioni 11.8 kila mwaka hivyo kuna ongezeko la fedha ili kutekeleza mpango huo.
Anasema mpango huo una dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu kwa kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika vizuri katika kujenga msingi wa uchumi wa viwanda na kupunguza umasikini.
“Msisitizo katika maendeleo ya viwanda nchini siyo jambo jipya, tangu Uhuru maendeleo ya viwanda yamekuwa yakipewa kipaumbele katika mipango ya vipindi mbalimbali, japo utekelezaji wake umekuwa ukitumia mikakati inayotofautiana kwa kuzingatia mfumo wa sera za usimamizi wa uchumi,” anasema.
Anasema wakati wa Azimio la Arusha, sekta ya viwanda iliendelezwa na sekta binafsi na Serikali na baada ya Azimio la Arusha, Serikali ilitekeleza siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo shughuli zote kuu za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na viwanda zilianza kumilikiwa na kuendeshwa na Serikali.
Aidha, msisitizo ulikuwa kujitegemea na viwanda vililenga kuzalisha bidhaa zinazotumika kwa wingi nchini na hivyo kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje na viwanda vichache vilijikita katika kuchakata mazao ya kilimo kwa ajili ya kuuza nje.
“Ili kuhakikisha viwanda na soko la ndani vinalindwa, sera ya kudhibiti biashara iliwekwa, kuyumba kwa uchumi nchini na kuvunjika kwa mfumo wa kisoshalisti duniani kuliifanya Tanzania kuachana na mfumo wa uchumi wa ujamaa na kujitegemea na badala yake kufungulia milango kwa wawekezaji binafsi na kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji,” anafafanua.
HALI YA VIWANDA NCHINI
Anasema tangu kuanza kwa ubinafsishaji wa mashirika ya umma mwaka 1992, viwanda 106 vimebinafsishwa kwa wawekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi na lengo lilikuwa ni kuongeza ufanisi wa usimamizi, uzalishaji, ajira, kupunguza uagizaji wa bidhaa zinazoweza kuzalishwa hapa nchini na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
Aidha, anasema kati ya viwanda vilivyobinafsishwa, viwanda 34 vinaendeshwa kwa ufanisi na hivyo kuongeza ajira na mapato ya Serikali, viwanda 33 vinaendeshwa kwa hasara na viwanda 39 vya bidhaa mbalimbali kama vile ngozi, chuma, korosho, zana za kilimo, sabuni na mafuta ya kupika vimefungwa kabisa kutokana na changamoto za kiutendaji, mitaji, teknolojia, nishati, malighafi au kutokuzingatiwa kwa mikataba ya mauzo.
“Hatua za uchambuzi kwa lengo la kubainisha mfumo wa kuvifufua viwanda vilivyobinafsishwa zimeanza na zinatarajiwa kukamilika katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango (2016/17),” anabainisha.
Hata hivyo anasema uendelezaji wa viwanda nchini ni jambo la kutiliwa mkazo katika mipango ijayo ili kuwezesha kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025.
“Maendeleo ya viwanda yanashikilia ufunguo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kutokana na uwezo wake wa kutengeneza ajira nyingi zenye faida na kuchochea maendeleo ya teknolojia. Mifano kutoka nchi mbalimbali inabainisha kuwa maendeleo ya viwanda ndio msingi na chimbuko la ustawi wa nchi hizo kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.”
Dk. Mpango anasema Tanzania itatumia uzoefu wan chi nyingine kufanikisha mageuzi ya viwanda nchini hususan katika kuweka mazingira mazuri ya kibiashara, kuweka mfumo mzuri wa kibenki, ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki maalum za maendeleo za kisekta kusaidia upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na kwa gharama nafuu.
Hata hivyo anasema serikali itatumia taasisi zake za kibiashara kama mkakati wa kuingia ubia na sekta binafsi katika kuvutia viwanda vyenye maslahi makubwa kitaifa, kibiashara, kiteknolojia au kuzalisha bidhaa muhimu kwa soko la ndani.
Anasema miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele katika bajeti ni utafiti na ubunifu na pia maendeleo ya miji na uendelezaji wa maeneo ya biashara kubwa na ndogo.
Katika hilo, anasema wajibu wa halmashauri za miji, wilaya na miji midogo ni kulea maendeleo ya viwanda na biashara katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kulinda maendeleo ya viwanda mkakati.
Anataja kuwa zaidi ya watu milioni 10 nchini ni maskini idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.
Waziri huyo anasema katika kuhakikisha kuwa mpango huo unatekelezeka ni lazima Watanzania wabadilike ili kuchochea uchumi na maendeleo ya nchi, akieleza kuwa Tanzania haihitaji kuendelea kuwa ombaomba.
"Tunaadhimisha miaka 55 ya uhuru wetu hivyo kiumri nchi yetu si changa tena ni nchi yenye umri wa mtu mzima anayepaswa kuwa na familia na uwezo wa kujitegemea kimaisha na kiuchumi hivyo basi hatupaswi kuwa tegemezi,” anasema.
Anataja maeneo ya kipaumbele katika mpango wa sasa, ni kukuza uchumi na kujenga msingi wa uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu, kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa mpango.
Hata hivyo, anasema uzoefu wa nchi nyingine unabainisha kuwa mkakati wa ujenzi wa viwanda aghalabu huvutia misaada kutoka nje na mantiki yake ni kuwa nchi haina budi kuwa na mkakati mahsusi wa kukusanya fedha kuwezesha utekelezaji wa mpango kwa ufanisi.
“Mpango unaainisha maeneo mawili ya vyanzo vya fedha, yaani, mapato ya Serikali yakihusisha mapato ya kodi na yasiyokuwa ya kodi, mikopo na misaada kutoka nje na eneo la pili ni sekta binafsi ya ndani na nje,” anasema.










