Wazawa wapewe kipaumbele ununuzi wa viwanda

22Apr 2016
Beatrice Bandawe
Dar es Salaam
Nipashe
Wazawa wapewe kipaumbele ununuzi wa viwanda

TANGANYIKA ilipopata Uhuru wake mwaka 1961, wananchi walipata madaraka ya kisiasa, lakini sehemu kubwa ya uchumi ilibaki mikononi mwa wageni na baadhi ya Watanzania.

Sabrina Kassim, akimimina mbegu za alizeti tayari kwa kusagwa na kuwa mafuta.

Mwaka 1967 lilitangazwa Azimio Arusha lililokuwa na mkakati wa kuhakikisha wananchi kupitia dola wanashika njia kuu za uchumi.

Shughuli zote za uzalishaji na utoaji wa huduma ziliundiwa mashirika ya umma.

Hata hivyo, mashirika mengi yaliendeshwa kwa hasara na yaliendesha shughuli za kiuchumi kwa kutumia mtaji na ruzuku kutoka serikalini.

Kuanzishwa kwa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, kulizingatia kuendeleza na kuipa nafasi kubwa zaidi sekta binafsi pamoja na kuzingatia masharti ya kuendesha uchumi katika mazingira ya nguvu ya soko.

Katika kutekeleza Sera hiyo, kinu cha kusaga nafaka kilichokuwa cha Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) Arusha, kilikodishwa kwa mwekezaji mzawa wa Kampuni ya Monaban Trading and Farming, ili kuhakikisha miundombinu yake inaendelea kufanyakazi.

NMC Arusha, kama yalivyokuwa mashirika mengine ya umma, yaliyokodishwa kwa wawekezaji wa ndani na baadhi yao kuuziwa, shirika hilo halijauzwa kwa mwekezaji anayekiendesha, licha ya kuomba kwa muda mrefu.

Mwenyekiti Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Monaban, Philemon Mollel, anasema alikodishwa kinu hicho tangu Agosti 23, 2007 na kwa sasa kina uwezo wa kulipa kodi kwa serikali Sh. milioni 200 kila mwezi, mishahara ya wafanyakazi 200 walioajiriwa, Sh. milioni 50 kila mwezi na hulipa matumizi ya umeme kwa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Sh. milioni 50 kila mwezi.

Mollel anasema kupitia maazimio ya Bodi ya kampuni yake, matakwa ya mkataba na sera mbalimbali hasa zile za uwekezaji, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) na Mpango wa Kurasishimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), imepanua wigo kwa kuajiri Watanzania wapatao 200 wakiwamo watalaamu na wasio watalaamu katika fani mbalimbali.

Anasema pamoja na uwekezaji mkubwa aliouweka katika kinu hicho, ukiwamo wa kununua mitambo mipya ya kukoboa na kusaga nafaka, kuboresha miundombinu ya mazingira ya kiwanda, mpaka sasa suala lake halijapatiwa jibu.

“Inanivunja moyo kwa sababu mashirika mengine ya NMC katika mikoa mingine yameshauzwa kwa wawekezaji, ikiwamo NMC Shinyanga, Iringa, Dar es Salaam, Tanga na Kilimanjaro,” anasema.

Mollel anasema kampuni hiyo inanunua nafaka kutoka mikoa mbalimbali hapa hapa nchini, na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho kuwa na bei nafuu na yenye ubora.

“Haya yanaleta msisimko chanya kisiasa, kijamii na kiuchumi si kwa wakazi wa Arusha tu bali hata katika mikoa ya jirani na kwa Watanzania walio wengi hasa wale wa kipato cha chini,” anasema.

Anasema alitegemea serikali ambayo lengo lake ni kuona viwanda vyake ilivyovikodisha vinafanya kazi kama ilivyokubaliana kwa mikataba iliyowekeana na wawekezaji, ingetoa kipaumbele kwa wawekezaji wazawa wanaofanya vizuri ili kuwapa moyo zaidi wa kuendeleza viwanda vyake na kukuza pato ya nchi.

Rais John Magufuli wakati wa kampeni za kugombea urais, mwaka jana aliahidi kufufua viwanda ili Tanzania iweze kuwa nchi inayozalisha bidhaa zake zenyewe.

Katika hotuba zake anazozitoa kwa nyakati tofauti amekuwa akisema Tanzania isiwe nchi ya kuletewa bidhaa za nje na kuuzwa kwa bei ya juu huku zingine zikiwa hazina viwango.

Rais Magufuli, amekuwa akirudia kwenye hotuba zake na kuonyesha kusikitishwa na baadhi ya viwanda vilivyokuwa vikitegemewa kwa uzalishaji nchini, kugeuka kuwa malisho ya mbuzi.

Sera ya Uwezeshaji ilikuwa na lengo la kuwawezesha wananchi kujenga uwezo wa ushindani katika soko la ndani ambalo bidhaa za nje zinaingia Soko la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, jumuiya nyingine na soko la dunia.

Vile vile, kuinua ubora wa bidhaa zinazozalishwa, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ujuzi.

Sera hiyo inasema pale ambapo miradi mikubwa ya wawekezaji itaanzishwa, itatoa fursa za kuzishirikisha shughuli za wananchi na itatekelezwa kwa kuwashirikisha wadau husika pamoja na serikali yenyewe.

“Madhumuni ya sera hii ni kutoa mwongozo wa jumla utakaohakikisha,wananchi wanapata fursa za kiuchumi katika sekta mbalimbali. Hivyo,

sera za kisekta kulenga katika kuwainua wananchi kwa kuwapendelea zaidi ikibidi na kuwawezesha kuwa na kauli na ushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi.”

Mwenyekiti Mtendaji Kampuni ya Monaban, anasema sera ya kuchangia huduma za kijamii zikiwamo shule, hospitali na taasisi za dini.

Hata hivyo, Mollel anasema Februari 2010 hadi Juni 2012, lililokuwa Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC), kwa kushirikiana na wadau kadhaa ikiwamo Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo na Chakula na kampuni ya Monaban, walijadiliana kuhusu mstakabali wa mali za NMC Arusha, zilizokodishwa kwa kampuni hiyo.

Anasema msingi wa majadiliano, ulikuwa kuangalia namna kampuni hiyo ingeweza kushirikiana na chombo cha serikali kilichokuwa kimeundwa, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na katika mazungumzo hayo kila upande ulikuwa na kipaumbele chake cha kuomba kuuziwa mali hizo.

“Kwa kuwa tulikuwa tumewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kukarabati kinu, majadaliano hayakuweza kuhitimishwa kwa kuwa muafaka haukuweza kupatikana kuhusu kurekebishwa mkataba wa ukodishwaji,” anasema.

Mollel anasema kimsingi kampuni yake ilionyesha nia ya kununua mali zote za NMC Arusha kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika na endapo serikali ingeamua kuwapatia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, kinu na mali za NMC na kuvunja mkataba, kampuni ya Monaban ingepata hasara ya kibiashara kwa kuwa ilishawekeza zaidi ya Shilingi bilioni sita.