Manuel Pellegrini: Heri Real Madrid kuliko Barcelona

18Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Manuel Pellegrini: Heri Real Madrid kuliko Barcelona

MANCHESTER City itacheza na mabingwa wa kihistoria Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

kikosi cha madrid

Hii ni maraya kwanza katika historia, Man City wanacheza hatua ya nusu fainali, huku kocha Manuel Pellegrini akiwa na dhamira kuendelea kuipa rekodi timu hiyo pekee ya Uingereza iliyobaki kwenye mashindano hayo.

Pellegrini anaona kama ndoto yake ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza inakwenda kutimia na hiyo ni kwa sababu, mabingwa watetezi Barcelona wameondolewa kwenye mashindano.

Pellegrini amesema hana hofu ya kukutana na Real Madrid ya Hispania katika nusu fainali ila anachoshukuru ni Barcelona kuondolewa kwenye mashindano.

Kwa mujibu wa droo iliyopangwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Bayern Munich watakumbana na Atletico Madrid katika nusu fainali nyingine.

Kutokuwapo kwa waliokuwa mabingwa watetezi, Barcelona, ni furaha kubwa kwa Pell. Safari ya Barcelona kujaribu kuandika rekodi ya kutetea taji hilo kwa mara ya kwanza, zilizimwa katikati ya wiki hii baada ya kutupwa nje ya mashindano na Atletico Madrid ya Hispania.

Ivan Rakitic wa Barcelona alifunga bao kwenye Uwanja wa Nou Camp na kuitupa nje ya mashindano Manchester City msimu uliopita.

Bosi huyo wa City alisema: “Sikushangilia, lakini kama ukiniuliza sipendi kukutana na Barcelona, nitakujibu ndiyo sipendi.”

City ilifungwa na Barca mara mbili kwenye michuano hiyo misimu miwili iliyopita.
Pell aliongeza: “Timu moja inapokufunga mara mbili, hiyo ni shida. Lakini nina uhakika kadri unavyocheza mechi nyingi kwenye mashindano ya ligi ya mabingwa ndivyo kikosi kinavyopata uzoefu.”

Pell pia amemuonya kocha wa Madrid Zinedine Zidane kwamba atakumbana na presha kubwa kwa sababu timu yake ndiyo inayoonekana kuhitaji kushinda mataji kila msimu.

Aliongeza: “Wana wachezaji wakubwa, labda naweza kusema kusema ndiyo timu timu bora kabisa kwa sasa duniani. Lakini na sisi pia tuna wachezaji wazuri.

Wakati Pellegrini akichekelea kutokuwepo Barcelona, kocha wa zamani Real Madrid Ancelotti ameionya timu hiyo kuacha kutegemea matokeo ya mechi za marudiano ili kusonga mbele kwenye mashindano.

Mabao matatu ya mshambuliaji, Cristiano Ronaldo yaliiwezesha Madrid kucheza hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kufungwa katika mechi ya kwanza mabao 2-0 na Wolfsburg katika hatua ya robo fainali.

Pamoja na timu hiyo kucheza kiume na kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwenye Uwanja wa Bernabeu, Ancelotti amesema jambo hilo halipaswi kutokea tena kwa timu kubwa kama hiyo.

Alisema kilichotokea kwenye mchezo dhidi ya Wolfsburg, kionekana kama jambo ambalo halipaswi kurudiwa tena.
"Katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa, hakuna bahati, huwezi kutegemea matokeo ya mechi ya marudiano ili usonge mbele.

Kama Real wanaosaka ubingwa wa 10 Ulaya wataonyesha mchezo kama ilivyokuwa dhidi ya Wolfsburg ugenini Ujerumani, wasitegemee kufika mbali.

"Zinedine Zidane na wachezaji wake wapitie kwa makini mechi ya kwanza dhidi ya Wolfsburg. Kutegemea nafasi ya kucheza nyumbani ndiyo wasonge mbele, wanaweza wasipate nafasi hiyo kwenye mechi za nusu fainali.”

Kuondolewa kwa Barcelona kwenye mashindano ina maana kwamba, kikosi cha kocha Luis Enrique kimepoteza ndoto za kuwa timu ya kwanza kutetea ubingwa tangu AC Milan ilivyofanya hivyo kwa mara ya mwishi mwaka 1990, wakati huo Ancelotti akicheza nafasi ya kiungo.

Ancelotti alisema: "Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani ngumu kulinda ushindi wa awali hata kama una wachezaji kama Lionel Messi, Neymar na Luis Suarez.