'Droo' imechezeshwa kila mtu akishuhudia na ikaamua Yanga itakwenda kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kupambana na Coastal Union huku Azam FC itamenyana na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.
Mechi zote zitafanyika Jumapili Aprili 24, mwaka huu.
Bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha Tanzania Bara mwakani kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (Caf).
Coastal Union iliingia hatua hiyo baada ya kuifunga Simba mabao 2-1, wakati Azam FC iliitoa Tanzania Prisons kwa ushindi wa magoli 3-1 wakati Mwadui FC iliyoshinda 3-0 iliitoa Geita Gold na Yanga iliwafunga Ndanda FC 2-1.
Mara ya mwisho michuano hiyo ilifanyika mwaka 2002 na JKT Ruvu iliifunga Baker Rangers ya Magomeni katika mchezo wa fainali wakati huo ikijulikana kama Kombe la FAT (Chama cha Soka Tanzania).
Hata hivyo JKT Ruvu haikushiriki kutokana na majina ya wachezaji kuchelewa kutumwa CAF.
Kwa muda mrefu sana wadau wa soka walikuwa wakilalamika juu ya TFF kujifungia wenyewe ndani ya kutoa ratiba yao badala ya kuendesha 'droo' ya wazi.
Wengi walihitaji shughuli hiyo kuwa wazi kuanzia hatua ya kwanza ambayo ilishirikisha timu 64.
Kilichohitajika na wapenzi wengi wa soka ni haki na usawa ili waone 'laivu' nani anacheza na nani, timu gani imepata bahati ya kuanzia nyumbani, lakini haikuwa hivyo.
Badala yake tuliona upangaji wenyewe ni kama timu kubwa za Simba, Yanga na Azam zilikuwa zikichambuliwa na kupangiwa zingine hasa za madaraja ya chini.
Na katika hali ya kushangaza ni kwamba timu ya Yanga haikucheza hata mechi moja ugenini kwenye raundi za awali.
Hii ilianza kuwatia hofu mashabiki wa soka nchini na kuzidi kupaza sauti kuwa upangaji wa ratiba kwenye michuano hii ya mtoano ifanyike kama tunavyoona kwenye mashindano mbalimbali ya aina hiyo barani Ulaya.
Kilio kikasikika na 'droo' ya michuano hiyo ikafanyika kwa uwazi, kila mmoja akishuhudia kwenye luninga.
Kilichotokea hapo ni kilekile ambacho wapenzi wa soka walikuwa wakikipigia kelele.
Uwazi huo umesababisha Yanga kwa mara ya kwanza kuanza ugenini Tanga huku Azam ikitakiwa kusafiri kwenda Shinyanga.
Hapa tunajifunza kuwa panapo ukweli uongo hujitenga na kitu chochote kinachofanyika kwa ukweli na uwazi huondoa mzizi wa fitina.
Uwazi huo umesababisha vigogo wote kuanzia ugenini. Kama watu wangejifungia ndani na kupanga, tungeweza kuletewa ratiba ya kigogo mmoja kuanza nyumbani na mwingine ugenini, isingejalisha kuwa ni Yanga au Azam.
Sina hakika kama tungeletewa ratiba ya vigogo wote kwenda ugenini.
Kama mtindo huu ungeanza mapema, huenda tungeshuhudia vitu tofauti na hivi tunavyoshuhudia sasa.
Inawezekana kabisa timu hizi zote vigogo zingekuwa zimeshatoka kwenye michuano hii kama zingepata mechi za ugenini.
Huenda hata zenyewe kwa zenyewe, Simba na Yanga, Azam na Simba, Yanga na Azam au Simba na Yanga zingeweza kukutana huko mwanzo na kutoana mapema kabisa.
Mashabiki wengi wa soka walidai kuwa ratiba ilionekana kuwa na nia ya kuzivuta klabu hizo kubwa ili zifikie angalau hatua ya nusu fainali.
Mimi nadhani sasa imefikia hatua TFF kuanza kuheshimu maoni ya wadau wa soka ambayo huwa na nia ya kujenga na kuliendeleza soka la Tanzania.
Kwa sababu hii ni mara ya kwanza baada ya miaka mingi ya kutochezwa Kombe la Shirikisho, TFF itakuwa imejifunza kuanzia mwakani, ipange ratiba 'laivu' tangu mwanzo kabisa wa michuano na si kusubiri hatua ya nusu fainali.
Si kwamba itasababisha wadhamini wapate nafasi ya kujitangaza mara kwa mara, lakini hata kuitangaza michuano hiyo ambayo baadhi ya wapenzi bado hawajaijua inavyoendeshwa.
Pia uwazi huo utapunguza malalamiko kutoka kwa baadhi ya timu pamoja na mashabiki wa soka kwa TFF kuwa zipo baadhi ya timu zinabebwa kwa kucheza nyumbani zaidi au kupangwa na wapinzani dhaifu.










