Kuanzia kwenye nafasi ya 11 ilipo Toto Africans yenye pointi 27 kabla ya mechi ya jana dhidi ya Simba, kushuka chini kwa Kagera Sugar yenye pointi 25, JKT Ruvu (24), Mgambo Shooting (23), African Sports (23) na Coastal Union (21) zote zinapigania zisiwe kwenye kundi la timu tatu zitakazoshuka daraja.
Hata hivyo, kwenye vikosi vya timu hizo kuna wachezaji ambao hata kama timu hizo zikishuka daraja, wao hawana wasiwasi kwenda kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
Watapata timu yoyote ile kati ya zitakazobaki Ligi Kuu. Kama si mpya basi Simba, Yanga, Azam FC au zingine zitakazobaki zitawawania kutokana na viwango vyao.
Hii inatokana na kuwa pamoja na vikosi hivyo kuonekana dhaifu, lakini kuna baadhi ya wachezaji wa timu hizo wamejipambanua na kuonyesha soka la hali ya juu kama ilivyokuwa kwa Shomary Kapombe aliyeiacha Polisi Moro naye kuwa mchezaji nyota alipochukuliwa na Simba hadi leo.
Uwezo, vipaji vyao vimewafanya watazamwe kwa macho mawili na timu nyingine zinazosaka wachezaji kwa ajili ya msimu ujao.
Mwandishi wa makala haya anakusanya baadhi ya majina ya wachezaji wa timu hizo ambao kama timu zao zitashuka daraja, tunaweza kuwashuhudia msimu ujao wakiwa na vikosi vya timu nyingine.
1. Fikirini Bakari-Coastal Union
Ni mmoja wa makipa chipukizi walio kwenye uwezo wa juu kwa sasa.
Ana uwezo wa hali ya juu sana na kama atapata mabeki wazuri, anaweza kucheza mechi nyingi bila kuruhusu magoli kizembe.
Ndiye aliyedaka mechi zote za Mkwakwani Yanga ilipofungwa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union, Azam FC ilipolala bao 1-0 kwenye mechi za Ligi Kuu, na pia alisimama langoni Simba ilipobamizwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho.
Hata kama Coastal itashuka daraja, kipa huyu ana nafasi ya kusajiliwa na timu nyingine.
Kuna taarifa kuwa Simba inamuwinda kipa huyu asaidiane na Benno Kakolanya, kipa wa Prisons ambaye naye anawaniwa na klabu hiyo kongwe.
2. Mwaita Gereza-African Sports
Nenda kwenye mechi tatu zilizobaki za African Sports, umtazame beki mmoja wa kulia wa timu hiyo anaitwa Mwaita Gereza.
Ni mmoja wa mabeki chipukizi wenye vipaji vya hali ya juu, ambao hawana majina.
Nadhani makocha wa timu mbalimbali watakuwa wameshamuona beki huyo mwenye uwezo wa kukaba na kupandisha mashambulizi.
Huyu namuweka kwenye kikosi cha wachezaji ambao watapata timu ya kuchezea Ligi Kuu hata kama timu yake hiyo itashuka daraja.
3.Youssouf Sabo-Coastal Union
Ni kiungo raia ya Cameroon aliyejiunga na Coastal Union baada ya kufanya majaribio ya kusajiliwa Yanga bila mafanikio kwenye kipindi cha dirisha dogo la usajili.
Itakumbukwa hivi karibuni alifunga magoli yote mawili, Coastal ikiifunga Simba kwenye Kombe la Shirikisho, lakini pia anaifahamu vyema shughuli yake kwani aliweza kuwafunika viungo wa Yanga na Azam kwenye mechi za Ligi Kuu na kuipa ushindi timu yake.
Hata kama Yanga haitomsajili, lakini kiungo kama huyu hawezi kuichezea tena timu hiyo kama ikishuka daraja, badala yake tutamuona kwenye timu nyingine msimu ujao wa Ligi Kuu.
4. Salum Kanoni-Kagera Sugar
Ni beki mkongwe nchini aliyepata kuichezea Simba miaka kadhaa nyuma. Kwa sasa Kagera Sugar haiko kwenye kiwango chake kilichozoeleka.
Ni moja kati ya timu zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja.Sina shaka kabisa kuwa Kanoni hawezi kubaki kwenye timu hiyo iwapo itateremka daraja.
Bado ameendelea kuwa na uwezo wa hali ya juu, huku akiwa na faida ya ziada ya kuwa mtaalam wa kufunga mabao ya penalti.Sitoshangaa kumuona hata akisajiliwa tena na timu yake ya zamani Simba, achilia mbali kwenye timu nyingine za Ligi Kuu.
5. George Kavila-Kagera Sugar
Ni mmoja kati ya mabeki wa kati wakongwe kabisa waliobakia kwenye Ligi Kuu.
Ameanza kucheza Ligi Kuu mwanzoni mwa miaka ya 2000 na hadi leo amekuwa kwenye kiwango kile kile.
Ndiye nahodha wa sasa wa Kagera Sugar. Pamoja na unahodha wake, sidhani kama ataendelea kubaki kwenye timu hiyo ikishuka daraja kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupambana na washambuliaji wakorofi.
6. Fullgence Maganga-Mgambo Shooting
Labda awe ni mwajiriwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ndiyo anaweza kubakia kwenye kikosi hicho ili kulinda ajira yake kama Mgambo Shooting itashuka daraja.
Vinginevyo ni mmoja kati ya wachezaji atakayeondoka kwani kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na klabu kubwa zikiwemo Simba, Yanga, Azam na Mtibwa Sugar.
Kwa muda mrefu ndiye amekuwa straika tegemeo kwenye kikosi hicho cha Mgambo.
Kwenye msimu huu wa ligi ameshapachika mabao sita. Amekuwa akiwasumbua mno mabeki wa timu pinzani kiasi cha timu yake kuogopwa na timu kubwa, ingawa msimu huu imeonekana haipo kwenye kiwango chake kilichozoeleka.
7. Juma Mahadhi-Coastal Union
Moja kati ya hazina kubwa ya washambuliaji wa Kitanzania kwa baadaye ni Juma Mahadhi.
Anatoka kwenye ukoo wa wanasoka, kwani babu yake alikuwa kipa tegemeo wa Simba Omari Mahadhi, huku baba zake wakichezea klabu mbalimbali kongwe kama Waziri Mahadhi, kiungo aliyeichezea Yanga huku Habib Mahadhi akizitumikia Coastal Union na Twiga.
Ni mmoja wa washambuliaji chipukizi hatari na wasumbufu, ambaye ameshafunga magoli matatu kwenye Ligi Kuu hadi sasa.
Alifunga bao la pili kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga na kama ilivyoshuhudiwa kwenye Kombe la Shirikisho, alikuwa akiwapeleka puta mabeki wa Simba.Iwapo timu yake itashuka daraja, wala hatopata tabu ya kupata usajili kwenye timu nyingine.
8. Bolly Shaibu-Mgambo Shooting
Si mchezaji mwenye jina kubwa, lakini kwenye soka kuna kitu kinaitwa takwimu ambazo huwa zinambeba mchezaji.
Takwimu zinaonyesha kuwa si mchezaji wa kubeza, kwani amekuwa msaada mkubwa kwenye timu yake kwenye kupika na kufunga magoli.
Ameshafunga magoli matatu mpaka sasa kwenye Ligi Kuu.
Ni nadra sana kupata aina ya wachezaji wengi wa aina hii nchini, hivyo sidhani kama Mgambo Shooting ikishuka daraja atakabaki.
9. Hassan Matalema-African Sports
Ni mshambuliaji chipukizi anayeonekana anaweza kufunga idadi kubwa ya magoli kama atapata timu bora, yenye viungo wachezeshaji wa uwezo wa hali ya juu. Ameifungia African Sports magoli matatu mpaka sasa.
Ndiye tegemeo lao kwa sasa inapohaha kujinusuru.Kama ikishuka, Matalema ana uhakika wa kubaki Ligi Kuu akiwa na timu yoyote ile kutokana na uwezo wake.
10 Saad Kipanga-JKT Ruvu
Ni mshambuliaji wa zamani wa Mbeya City ambaye kwa sasa anaichezea JKT Ruvu ya Mlandizi mkoani Pwani. Amefunga magoli matatu mpaka sasa. Kuna wakati Simba ilitaka kumsajili, lakini viongozi wa Mbeya City wakaweka ngumu.
Kwa sasa anaonekana kama amepungua makali. Labda kutokana na timu dhaifu anayoichezea, lakini ni mmoja wa washambuliaji hatari sana akiwa kwenye kiwango.
Kwa hadhi na uwezo wake, sidhani kama ataendelea kubaki wa timu hiyo ikishuka.










