Dar ipanuliwe kuinua uchumi

17Apr 2016
Ibrahim Mkamba
Dar
Nipashe Jumapili
Dar ipanuliwe kuinua uchumi

DAR-ES-SALAAM jiji kuu la kibiashara imezidiwa, imebeba mzigo mzito mno unatokana na kuwa na ofisi nyingi kubwa zilizosongamana kando ya Bahari ya Hindi. Kubwa kuliko zote ni bandari.

jiji la dar es salaam.

Ofisi hii inasababisha kuingia na kutoka kwenye jiji kuu kwa malori makubwa yanayobeba shehena ndani makontena pamoja na matangi ya mafuta ambayo husababisha msongamano mkubwa wa magari kwenye barabara kadhaa za hili jiji kuu.

Dar es Salaam inaweza kupunguziwa mzigo kwa njia mbili kubwa ambazo ni pamoja na kupunguziwa mzigo wa kule kunakoitwa katikati ya jiji, kwa Kingereza cha Uingereza “city centre” na cha Marekani “downtown”.

Njia ya kulipunguzia mzigo na msongamano wa kule kunakoitwa katikati ya jiji ni kupanua mipaka ya mkoa wa Dar es Salaam na kulazimisha ujenzi wa ofisi kubwa mpya kwenye eneo jipya litakalopanuliwa.

Katika utaratibu huo, miji ya Kibaha, Kisarawe na Mkuranga inapaswa iwe ndani ya mkoa wa Dar.Makao makuu ya mkoa wa Pwani yatafutiwe mji mwingine.

Kwa Kaskazini mpaka unapaswa uwe kwenye kitongoji cha Zinga, barabara ya Bagamoyo, uteremke hadi Kitonga Mlandizi iachwe ibakie mkoani Pwani. Ushuke mpaka Masaki Kisarawe na kumalizikia kusini wilayani Mkuranga katikati ya Shugubweni itakayokuwa ndani ya Dar na Kisiju itakayobakia Pwani.

Eneo hilo jipya la nyongeza litapaswa lipimwe kama jiji jipya. Liwe na barabara zenye upana wa kutosha na za idadi ya kutosha, maegesho ya kisasa ya magari, ofisi, maeneo ya wazi ya kutosha na barabara zenye upana wa kutosha na idadi ya njia zinazohitajika kutoka ufukweni wa bahari ya Hindi eneo la Zinga itakayoikatiza barabara ya Bagamoyo.

Barabara hiyo ipitie wilaya ya Kibaha kuikatiza barabara ya Morogoro na kupita wilaya ya Kisarawe mpaka kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi wilayani Mkuranga baada ya kuikatiza barabara ya Kilwa.

Barabara hiyo (Zinga-Mkuranga) itakuwa ndiyo mpaka wa Dar na Pwani.Ukitoka upande wa Morogoro ,unaweza kuingia Dar ya sasa moja kwa moja au ukapinda kulia na kukashika barabara hiyo ya Zinga-Mkuranga kwenda nayo mpaka Masaki Kisarawe, ukakata kushoto kwenda Kisarawe kupitia Dar ya sasa, ukitumia Barabara ya Nyerere au ukapitiliza mpaka Mkuranga na kuingilia Barabara ya Kilwa au barabara zozote mpya zitakazoanzishwa kwenye mpango huo.

Safari ya Lindi na Mtwara kutoka au kwenda Bagamoyo, Morogoro, Tanga, Moshi, Arusha na kwingine kwa uelekeo huo, haitalazimisha kuingia ndani ya Dar ya sasa. Ukipenda utatumia hiyo barabara ya Zinga-Mkuranga. Mpango huu utapunguza msongamano wa ofisi, watu na magari katikati ya Dar es Salaam ya sasa.

Kuhusu kupunguza msongamano wa Dar yote itengenezwe bandari kubwa ya nchi kavu jirani na eneo la Ruvu pale reli ya Tanga inapopita juu ya barabara ya Morogoro. Ziandaliwe heka nyingi eneo hilo ili malori yanayopeleka na kuchukua shehena bandarini Dar na Tanga yachukulie na kushushia mizigo hiyo hapo bandari kuu ya nchi kavu kati ya Ruvu na Vigwaza mkoani Pwani.

Treni ambazo kwa sasa hazifanyi kazi hivyo kuathiri uchumi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), zitaanza kubeba shehena kutoka na kwenda bandari za Dar na Tanga, zikianzia na kuishia bandari kavu ya Ruvu.

Taratibu za kiforodha zitapangiliwa vizuri kuufanya utaratibu huo utekelezeke bila uhalifu, hujuma wala usumbufu.
Utaratibu huo, zaidi ya kuiinua TRL kimapato, utapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari Dar, utazilinda barabara za Dar pia kuinua uchumi wa maeneo ya jirani na bandari kavu hiyo kutokana na biashara kubwa zitakazokuwepo kwenye sehemu hizo.

Sehemu hizo ni Mlandizi, Ruvu, Vigwaza, Chamakweza, Pingu na Chalinze. Ninajua kwamba duniani kote treni ndizo hutumika kusafirishia mizigo na nimeshauri hivyo kwa kuona kwamba reli imetushinda.

Reli imeonekana kuwa na changamoto kubwa baada ya stesheni ya Kilosa kuelekea Munisagara na tatizo kubwa liko kwenye mto Mkondoa ambao huongezeka upana msimu kwa msimu. Ufumbuzi ni kuivusha reli hiyo kwenye mto huo baada tu ya stesheni ya Kimamba ambapo stesheni ya Kilosa itahamishiwa eneo la Magomeni (Rozi), ng’ambo ya mto Mkondoa na kupita huko kuelekea Munisagara.

Njia hiyo ndiyo itakuwa ufumbuzi wa kudumu wa changamoto reli hiyo Kilosa.

Miradi yote inahitaji mipango madhubuti ya muda mrefu, kiasi kikubwa cha fedha ikiwamo mikopo na ufadhili na kuepuka ufisadi. Ikikamilika, tutapaa kiuchumi. Tukiona ushauri huu una tija, tunapaswa tujiulize endapo ipo haja ya kuwa na hifadhi za misitu za Kazimzumbwi Kisarawe na Mabwepande ambazo ziliamuliwa kuwa hivyo miaka ile zilipokuwa mbali mno na Dar. Kupanga ni kuchagua.