Akiwa na wageni wake hao, pamoja na mambo mengine, Lowassa alizungumzia uongozi wa Rais John Magufuli na kutoa maoni yake. Alisema:
“Hali ya hivi sasa nchini ni ya hamasa kutokana na serikali mpya na staili mpya, kwa kipindi kifupi atakuwa maarufu lakini hakuna mafanikio ya kiuchumi mbele ya safari”.
Lowassa alitolea mfano, Rais Magufuli amekuwa akichukua uamuzi wa kugawa fedha kwa shughuli mbalimbali wakati chombo cha kufanya hivyo kipo ambacho ni Bunge aliongeza: “Kugawa pesa siyo kazi ya Rais kuna taasisi ambayo ni Bunge yenye mamlaka ya kuidhinisha bajeti.”
Mara tu bada ya Lowassa kutoa ushauri huo, naye msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, aliwaita wanahabari ofisi ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam na kujibu mapigo akisema;
“Inafahamika wazi kuwa Rais Magufuli hafanyi kazi kutafuta kusifiwa na watu’ hajawahi kumfukuza mtu kazi bila kujiridhisha. Amekuwa akiwasimamisha kazi na kuwachukulia hatua upelelezi unapokamilika.”
Alisema, hatua anazochukua Rais ni za kupambana na wahujumu uchumi na kwamba CCM inaendelea kumuunga mkono na Watanzania pia wako pamoja naye.
“Kama kuna watu wanalalamika ni wazi kuna ndugu zao, marafiki wameguswa au biashara zao zitakuwa zimeguswa kwa namna moja au nyingine na utendaji wa Rais,” alisema ole Sendeka. Tutajadili.
Nilifuatilia kwa makini hoja ya Lowassa, vivyo hivyo majibu maelezo ya msemaji wa chama CCM, na kubaini mambo yafuatayo.
Mosi, wasemaji wote wawili walikuwa na muono sawia kuhusu mfumo wa uendeshaji wa serikali ambao Lowassa aliulalamikia akidai umejaa kasoro nyingi hivyo unaruhusu mianya ya rushwa akimjibu, ole Sendeka, naye aliafiki kauli ya Lowassa kwasababu ametolea mfano kwamba hata Lowassa aliwahi kukumbana na kadhia hiyo akiwa Waziri Mkuu alishawahi kumsimamisha mmoja wa wakurugenzi wa Mkoani Kilimanjaro kwa kushindwa kusambaza chakula cha misaada na kusimamia uvunjaji wa majengo ya serikali.
Suala hili la mfumo wa uendeshaji serikalini ni jambo ambalo wadau wengi wamekuwa wakilipigia kelele kwamba umejaa kasoro nyingi. Nilitegemea Sendeka angetumia mwanya huo kubainisha hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano kurekebisha maeneo tata.
Kwa maana nyingine, hapakuwa na haja kutumia nguvu nyingi kutafuta mabaya ya Lowassa eti, naye aliachia nafasi yake ya uwaziri mkuu kutokana na mfumo huo unaopigiwa kelele.
Pili, hoja ya Rais Magufuli kujichukulia uamuzi wa kugawa fedha kwa shughuli mbali mbali wakati chombo cha kufanya hivyo kipo ambacho ni Bunge.
Hoja hii wadau wa siasa pamoja na baadhi ya wabunge kwa nyakati tofauti wamesikika wakihoji mamlaka ya Rais ya kuweza kuagiza hela zielekezwe kwenye mradi tofauti na maagizo ya Bunge.
Suala hili halikuhitaji majibu mepesi kama alivyodadavua msemaji wa CCM ilitakiwa aanishe vifungu vya sheria mbele ya waandishi wa habari ambavyo kwa namna moja au nyingine vinamruhusu Rais kutoa maamuzi kama alivyofanya.
Utafiti nilioufanya kwa kupitia baadhi ya fungu katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nimebaini na kuridhishwa kwamba Ibara ya 137 inaelekeza utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha zilizomo kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali hivyo inamruhusu Rais kuagiza fedha zipelekwe kwenye mradi tofauti.
Ibara hiyo inasema: “Rais atatoa maagizo kwa watu wanaohusika kwamba watengeneze na kuwasilisha kwenye Bunge katika kila mwaka wa fedha wa serikali, makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kipindi cha mwaka wa fedha unaofuata.” Maelekezo zaidi pia yamo kwenye ibara hiyo 137 (2), (3) (a-b).
Kwa mantiki hiyo, majibu ya ole Sendeka yalipwaya. Alipaswa ajielekeze kwenye ibara hiyo na awaaminishe Watanzania kinaga-ubaga mamlaka ya Rais ya kuweza kuelekeza matumizi nje ya mfuko huo mkuu wa hazina ili wananchi wasiendelee kupotoshwa.
Ushauri wangu kwa msemaji wa chama ni kwamba, siyo kila hoja inayotoka kwenye kambi ya upinzani eti mara zote zinalenga kubomoa CCM, la hasha. Ni vyema wakati mwingine maoni hayo yakachujwa mazuri yafanyiwe kazi na yasiyo ya msingi yaachwe.
Mengi aliyoyasema Lowassa binafsi nayaona kama alikuwa akitoa ushauri kwa serikali ya Rais Magufuli. Siyo dhambi Lowassa kuishauri serikali, kwa sababu Hakuna asiyoyajua katika nchi hii. Hapakuwa na sababu za msingi kwa msemaji wa CCM, ole Sendeka, kuibuka na kupinga hoja hizo. Tafakari.
Mawasiliano:0713-399004 / 0767- 399004, jmkibasso@gmail.com










