Serikali ya Magufuli imejaa watu wanaopenda kushangiliwa

13Apr 2016
Restuta James
Dar
Nipashe
Serikali ya Magufuli imejaa watu wanaopenda kushangiliwa

WAKATI nchi ikiwa kwenye taharuki kubwa kutokana na ‘kasi’ ya utumbuaji majipu unaoendelea kwenye sekta mbalimbali za umma, kambi ya upinzani haioni matokeo ya maana ya utendaji huo.

Dk. Vincent Mashinji.

Ni kwamba kinaona serikali ya awamu ya tano ‘imejaa’ watu wanaopenda kushangiliwa na umma kwa kutaka kufanya vitu vinavyopamba vyombo vya habari, lakini visivyoleta matokeo chanya ya muda mrefu kwa wananchi, kitaifa na kimataifa.

Anayekosoa utendaji wa serikali hii ya ‘utumbuaji’ majipu ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji, ambaye anasema matakwa ya wakati huu ni Katiba mpya na utawala unaoheshimu sheria tu, siyo vinginevyo.

“Mimi ni muumini wa kitu kimoja. Unatakiwa kuwa na core business (kitu kimoja mahsusi), na vingine vinakuwa ni makandokando ya ile business (hicho kitu). Kwa hiyo, watake wasitake, haya ni matakwa ya wakati, ni matakwa ya utaalam, ni matakwa ya kisiasa…kama watashangilia majipu…watu wanataka Katiba; shot of that,” anasema.

“Tunahitaji Katiba. Kingine, (makandokando), tunahitaji mheshimiwa afuate sheria. Kwa nia yoyote aliyonayo kwa taifa hili, kwa nguvu zozote alizonazo kupambana na ufisadi ambao kila mtu anauona ni tatizo, afuate sheria,” anasema Dk. Mashinji.

Dk. Mashinji anasema: “La sivyo, hii nchi ataiingiza kwenye mgogoro mkubwa wa kiuchumi, ataiingiza serikali yake kwenye madeni makubwa na faini kubwa kwa sababu hawa watu wote watamshinda kesi na watamdai…tunaomba utawala wa sheria.”

Anasema ili kuhakikisha Katiba mpya yenye maoni ya wananchi inapatikana, wabunge na viongozi wote wa chama wamepewa jukumu la kuwaelimisha wananchi umuhimu wa Katiba na mambo ya msingi ambayo wananchi waliyapendekeza kwenye rasimu ya pili iliyotolewa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba.

Anasema katika hilo, wananchi wataelimishwa sheria mbalimbali na hususani kwenye Halmashauri na Manispaa wanazoziongoza ili wafahamu sheria wanazozisimamia kwa kujua haki na wajibu wa viongozi na wananchi.

Hata hivyo, anasema utendaji wa serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Dk. John Magufuli, haujajikita katika kujenga mfumo ambao utawabana na kuwashughulikia moja kwa moja wabadhirifu na mafisadi, na kwamba kinachotakiwa kufanywa ni kuwa na Katiba.

Anasema Rais Magufuli anatenda mambo ambayo hayana msingi mkubwa kisheria na kwamba hilo litakwamisha vita vya ‘kutumbua majipu.’

Anasema tatizo kubwa linaloikabili nchi ni mfumo usioweza kuwabana kikamilifu wakwepaji kodi na mafisadi.
“Hapa ni kama hawa jamaa wamedandia treni kwa mbele. Sasa hivi anakamata watu, hebu nikuulize, nchi ina miundo mbalimbali ya usalama kama Usalama wa Taifa, Polisi na Jeshi; na raia wenyewe,” anasema.

Anasema katika msingi huo, haiwezekani makontena zaidi ya 300 yakapotea bandarini au meli ‘zikapotea’ bila vyombo hivyo na hususani usalama wa taifa na Ikulu kujua.

“Kama kweli Ikulu haikujua, kwa nini watu wanaipenda CCM? Haiwezekani wewe ni mwanaume, mke wako anachepuka na mwanaume wa mbali hujui, anachepuka na jirani hujui hadi anaingia kwa house boy hujui, halafu unajiita mwanaume,” anasema.

Anasema: “Escrow sidhani kama utaniambia Ikulu haikujua, lakini walisubiri hadi wabunge wakapiga kelele hadi baada ya kelele nyingi ndipo walichunguza na kuamua kupeleka watu mahakamani.”

Dk. Mashinji anasema tatizo la CCM ni mfumo na kwamba imejiunda kama genge la watu wanaofanya mambo yanayofanana wakijua namna watakavyokutana mbele ya safari.

“Kama kweli mheshimiwa (Magufuli), ameamua kupambana na rushwa, hajui rushwa ninini, tafsiri yake na hajui naliwaje. Akajifunze kwanza hayo,” anasema.
Anasema: “Anachokifanya hakitaifikisha nchi popote.”

Anasisitiza kuwa: “Naona bwana mkubwa anapambana na personalities (watu), yuko bize na personalities. Bado hatujaamua kabisa kupambana na rushwa.”

“Mimi ni daktari, ninapoletewa mgonjwa yeyote mwenye ugonjwa sugu unachokifanya siyo kumrudisha kwenye hali ya kawaida kwa mara moja, ukimrudisha kwenye normal anakufa.”

Anatoa mfano kuwa daktari akipokea mgonjwa mwenye presha kubwa ya juu anachofanya ni kuishusha taratibu kwani akilazimisha kuishuka kwa mara moja, mgonjwa huyo lazima atakufa, akieleza kuwa pamoja na jitihada anazofanya Rais Magufuli, hakuna chochote cha maana kitakachozaa matunda.

Anasema mfumo wa biashara uliopo nchini pamoja na soko, hauruhusu ukusanyaji wa mapato utakaotosheleza bajeti na nchi kujiendesha.

“Kama Rais anahamu ya kutumbua majipu, utawala wake ni miaka mitano mwaka mmoja una siku 365 mara miaka mitano ni siku 1,825…hii Tanzania ukutafuta watu kwenye mashirika makubwa waliokula rushwa utakosa mafaili 2,000? Kwa maana hiyo kama yuko serious (makini), atatumia miaka yetu mitano kusoma mafaili ya watu na kuwapeleka mahakamani,” anasema.

“Ameshakata siku 150, hakuna mtu anayejua mpango wa serikali wa maendeleo…sijui watu wanashabikia nini,” anasema Dk. Mashinji.

anasema safari ya utumbuaji majipu inafanyika kwa njia ambazo zitaigharimu nchi akieleza kuwa wafanyabiashara wengi wameorodheshwa na kuhojiwa wakati wamekuwa wakilipa kodi na tozo nyingine kwa mujibu wa sheria.

Anasema: “Kwa hiyo tatizo hapo ni mfumo maana kuna watu waliokuwa wakipokea zile fedha (kodi), kumbe kule ndani wanakolipa ndiko kuna kamchezo kanafanyika. Tunajiuliza ina maana hii nchi haina intelijensia ya kuweza kubaini mambo haya?”

“Kwa hiyo sisi kama chama tunajiandaa na kuwaandaa wananchi…sasa hivi tuko kwenye mgogoro na jumuiya ya wafanyabiashara, tuko kwenye mgogoro na jumuiya ya kimataifa. Hii katika ngazi ya diplomasia ni hatua ya juu sana,” anasema.

Anasema kilichofanywa na washirika wa maendeleo kususia kuchangia bajeti ya serikali wanakiunga mkono ili kuhakikisha heshima ya nchi inarudi kwa watawala kuheshimu maoni ya wananchi hasa kupitia sanduku la kura.
Dk. Mashinji amekosoa pia uhusiano wa Rais Dk. Magufuli na Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, akieleza kuwa kidplomasia unatia doa nchi.

Anasema lazima kuwekwe mipaka ya mahusiano binafsi ya Rais na ya nchi akitolea mfano kuwa hivi karibuni kumekuwapo na mvutano wa ujenzi wa bomba la mafuta kati ya Kenya, Uganda na Tanzania, kwa Tanzania kufanikiwa kuishawishi Uganda kujenga bomba hilo kuanzia Tanga hadi nchini humo, halafu katika mazingira hayo, Rais anakutana na kiongozi wa upinzani wa serikali ya Uhuru Kenyatta, inaweza kuleta tafsiri mbaya.

“Kisiasa inaweza isilete afya nzuri. Kenya wanataka bomba lipite kwao ili wapate kodi, wewe unataka bomba…muda huo huo unakutana na kiongozi wa upinzani, hii inaleta picha gani kwenye jumuiya ya kidiplomasia?” anahoji.

Anasema: “Angeweza kumwambia (Odinga), asubiri kidogo. Rais anatakiwa alinde maslahi ya nchi kwa kauli na matendo yake.”

ZANZIBAR
Kuhusu Zanzibar anasema ‘vita’ ndio kwanza imeanza na kwamba wanachofanya sasa kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ni kuendelea kuzungumza na washirika wa maendeleo kuona namna ya kushughulikia mgogoro huo, lakini ikishindikana kabisa wananchi wataamua.

“Ndio kwanza shoo imeanza. Lakini bado tunazungumza na wadau mbalimbali tuone nini kitafanyika, lakini ikishindikana kabisa wananchi wataamua…najua wengine tutaenda huko tutapigwa mabomu, tutalazwa Segerea, lakini kuna siku mambo yatakaa tu sawa.”

“Hii ni nchi yetu sote, siyo ya kikundi cha watu,” anasema.

“Ukisoma kitabu cha the art of war kinakuambia kuwa adui yako anapofanya makosa usimwingilie, kwa hiyo sisi hautaona tunapiga kelele, lakini tutafanya mambo ya maendeleo ambayo wananchi watayaona kwa macho,” anasema.