Hata wenyeviti wa vyama vya siasa visivyo hata na mjumbe mmoja wa serikali ya mtaa au kijiji nao walikuwa wanatoa matamko ya kukemea au kuonya. Na katika kukemea kwao, walikuwa wakiegemea upande mahsusi na imekuwa hivyo kwa muda mrefu sasa.
Siyo hivyo tu, baadhi ya watoa matamko walikuwa wanatoa posho kwa wanahabari wanaohudhuria mikutano yao na vyombo vya habari, katika mazingira ambayo wanalilia ruzuku ili waweze kujiendesha na kusimamisha wagombea kwenye ngazi mbalimbali.
Mathalani, wakati kampeni za uchaguzi mkuu zikiwa zimepamba moto mwaka jana, aliyekuwa mgombea wa Chama cha United Peoples Democratic Party (UPDP), Fahmi Dovutwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, alionekana kuegemea upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa alipokuwa kwenye mjadala wa kipindi cha luninga akieleza kuwa wapinzani na hasa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hauna sababu za kuichukia CCM na badala yake, kambi hiyo ifanyekazi ya kuwaletea wananchi maendeleo ili wachaguliwe!
Katika kipindi hicho Dovutwa alikuwa na Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, ambao kwa ujumla badala ya kueleza mikakati yao katika kushika dola, waliishia kuukosoa Ukawa na kuisifu CCM.
Haya yamekuwa yakitokea katika mazingira ambayo tunaamini kuwa lengo la kwanza kabisa la chama chochote cha siasa ni kushika dola.
Mfano wa Dovutwa na Mrema, ambao ni wenyeviti wa vyama kukosoa upinzani na kukisifu chama kinachoongoza dola una tafsiri gani?
Na hapa simaanishi hawa wawasifu Ukawa, hapana. Waeleze sera na mikakati yao katika harakati za kuelekea kushika dola. Lakini ni harakati gani za kushika dola ambazo hazizalishi walau kiongozi mmoja kwenye serikali ya mtaa au kijiji?
Akizungumzia vyama hivyo, Katibu wa Makatibu Wakuu wa vyama visivyo na wabunge/madiwani, Renatus Muabhi, anasema vyama hivyo vinaendelea kujifunza kupitia mataifa yenye vyama vingi vya siasa na pia kutoka kwa vyama vinavyoonekana kuwa ni vikubwa nchini.
Anasema wamekuwa wakionekana wakati wa chaguzi, lakini sasa wamejipanga kuwa mstari wa mbele katika kuishauri serikali.
“Kwa sasa tunakusudia kuisaidia serikali kwa kuishauri katika kupanga maendeleo na ndio maana tumejiunga ili tuwe na sauti moja,” anasema.
Muabhi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), anasema Jumapili iliyopita viongozi wa vyama hivyo walikutana na kuandaa mpango wa kitaifa katika nyanja mbalimbali ambazo wanakusudia kuishauri serikali na kwamba mwishoni mwa wiki hii watakutana tena kwa ajili ya kuupitisha rasmi.
“Tunaangalia rasilimali kama gesi, madini, utalii na nyinginezo na tunakusudia kuishauri serikali…uchumi wa nchi hauwezi kuendelea kutegemea bandari na TRA tu,” anasema.
Anasema: “Kwa kasi tunayoiona ni kwamba tunakusudia kushirikiana sana na serikali kwa sababu kinachofanyika sasa yalikuwa ndio malalamiko ya upinzani na ndio matakwa ya wananchi hivyo lazima tuiunge mkono Serikali ya Awamu ya Tano.”
Kuhusu ruzuku, Muabhi anasema: “Hatupati ruzuku…wanaotusapoti ni wanachama wetu na watu wenye mapenzi mema na sisi. Bado tunafuatilia ruzuku…tunashindwa kusimamisha wagombea kwa sababu hatuna fedha na kama unavyojua hata kama ukiwa mwadilifu huwezi kushindana kwenye kugombea ukashinda kwa sbabau hata hela za kulipa mawakala hatuna.”
Anasema vyama hivyo vitaendelea kupiga kelele ili vipate ruzuku kuweka uwanja sawa kwenye ushindani wa kisiasa.
Kuhusu Zanzibar anasema wamefurahishwa na kitendo cha Rais Ali Mohammed Shein, kuteuwa baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani visivyo na ushawishi mkubwa, akieleza kuwa hiyo ni hatua kubwa kwenye siasa za nchi.
Vyama hivi vinapata wapi nguvu ya kusimamisha wagombea urais wakati hawana diwani? Kujibu swali hili, Muabhi anasema: “Tunaendelea kujifunza, lakini kubwa nililokuambia ni kukosa fedha za kuendesha kampeni na kulipa mawakala wakati wa uchaguzi na ndio maana tutaendelea kuomba ruzuku kwa vyama vyote ili uwanja uwe sawa.”
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana vyama vya CCM na Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa, vilichuana vikali Tanzania Bara na CCM ilichuana na CUF visiwani Zanzibar na ndivyo vyama vilivyokuwa vinapewa nafasi ya kushinda urais na viti vingi vya ubunge na madiwani.
Hata hivyo, vyama kama UPDP, TLP, ADC, ACT-Wazalendo, NRA na Chauma, visivyo na ushawishi mkubwa kwenye medani za siasa nchini vilisimamisha wagombea kwa ngazi ya urais, wakati havina wawakilishi kwenye ngazi nyingine za uongozi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa za Msajili wa Vyama vya Siasa, ni kwamba hadi sasa kuna jumla ya vyama 22 vina usajili wa kudumu wakati vyama vitatu ndivyo vina usajili wa muda.
Ni katika muktadha huo, wadadisi wa masuala ya kiasia wanahoji, wakati wa uchaguzi vyama vyote vinakuwa na fedha, baada tu ya hapo; vinafilisika! Sasa je, fedha za maandalizi ya kutoa matamko huwa zinatoka wapi?










